
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ameendelea kutoa wito kwa jamii hasa wanawake kuwa chachu ya mabadiliko chanya kwa ustawi wa Taifa.
Akifungua kongamano la kujengea uwezo Wanawake lililoandaliwa na Taasisi ya “Godly Women Ambassadors Tanzania”(GWAT) katika Kanisa La Agape Life Church (ALC) Mbezi Beach, Dar Es Salaam, Julai 14, 2023, Waziri Dkt. Gwajima amesema makongamano kama hayo yanaunganisha nguvu za wadau na Serikali katika safari ya uwezeshaji wanawake.
Ameongeza kuwa, makongamano hayo yanakwenda sambamba na malengo ya Serikali ya kuwawezesha wanawake kiuchumi, ajenda inayosimamiwa kwa dhati na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Ni faraja kuona mama anasimama kwenye nafasi yake, kuweza kufanya jamii kuwa salama na yenye ustawi ndani ya familia, taasisi za dini na maslahi mapana ya Mataifa yetu, likiwamo Tanzania na dunia kwa ujumla.” Waziri Dkt. Gwajima.

Aidha, amesema Serikali kupitia Wizara yake inaendelea kushirikiana na wadau wote wa Maendeleo na Ustawi wa jamii kuhakikisha jamii inakuwa salama dhidi ya changamoto za kimaadili “nawakaribisha sana kwenye wizara yenu ya jamii mje tufanye kazi pamoja kwani malengo yetu yanafanana” Dkt. Gwajima.
Kongamano hilo la kimataifa la siku tatu linalohusu kuwainua na kuwajenga wanawake, linahusisha washiriki kutoka madhehebu mbalimbali ndani na nje ya nchi.