GST kujenga Maabara ya Kisasa jijini Dodoma*
GST ni Moyo wa Sekta ya Madini
Kufanya Utafiti wa kina kufikia asilimia 50
Na Madina Mohammed DODOMA WAMACHINGA
Waziri wa Madini Mhe.Anthony Mavunde amewataka Watumishi wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kuchapa kazi kwa bidii ili kutimiza Vision 2030 ambayo ndana yake kubwa ni Madini ni Maisha na Utajiri.
Mavunde ameyasema hayo leo Aprili 24, 2024 jijini Dodoma katika kikao cha kujadili namna bora ya utendaji kazi kilichowakutanisha Watumishi wote wa GST.
Akizungumza kuhusu umuhimu wa GST, Waziri Mavunde amesema GST ina mchango mkubwa katika ukuaji wa Sekta ya Madini huku akisisitiza kwamba GST ni Moyo wa Sekta ya Madini nchini, kutokana na umuhimu huo Serikali imeendelea kuiwezesha zaidi GST ili itekeleze majukumu yake kwa ufanisi unaotarajiwa.
Aidha, Waziri Mavunde amesema heshima ya GST ipo mikononi mwa watumishi wa GST hivyo, amewataka watumishi wote kufanya kazi kwa bidii, kuilinda na kuisimamia Sekta ya Madini kwa maendeleo ya Taifa.
Mavunde amewataka watumishi wote kujituma na kufanya kazi kwa weledi katika kutekeleza majukumu ya GST na kusisitiza kwamba hatakuwa tayari kumvumilia mtu yoyote ambaye hatakuwa tayari kuchapa kazi kwa bidii ili kufikia maono na matarajio ya Wizara na wadau kwa ujumla.
Pia, amesema umoja na mshikamano ndiyo kitaisaidia Taasisi hiyo kusonga mbele na kuwataka watumishi wote kufanya kazi kama timu moja.
“Kwa umoja wetu naomba tuhakikishe tunafikia malengo tuliyojiwekea ya kufanya utafiti wa kina wa asilimia angalau 50 ifikapo mwaka 2030,” amesema Waziri Mavunde.
Waziri Mavunde amefafanua kuwa kutokana na umuhimu wa Taasisi ya GST, Serikali itaendelea kuhahakisha watumishi wa GST wanajengewa uwezo kutoka kwa Taasisi za Kimataifa zenye uzoefu mkubwa katika shughuli za utafiti ili kuongeza ujuzi kwa wataalam wa Taasisi hiyo.
Akielezea juu ya mafanikio ya utafiti wa madini, Waziri Mavunde amesema mpaka sasa GST imefanikiwa kufanya utafiti wa kina wa High Resolution airborne Geophysical Survey kwa asilimia 16 pekee ambapo utafiti wa Low Resolution umefanyika kwa asilimia 100, hivyo wizara itaendelea kufanya utafiti wa kina kwa lengo la kuongeza taarifa zinazoonesha uwepo wa madini nchini.
“Baada ya Vision 2030 nchi mbalimbali zimeonesha nia ya kufanya kazi na GST ambapo tumechuja na tumepata kampuni na taasisi tutakazo fanya nazo kazi, kwa sasa tumeanza utafiti wa majaribio wa kurusha ndege nyuki na tunaendelea mpaka tutakapo timiza malengo yetu,” amesema Waziri Mavunde.
Pia, mesema azma ya Wizara ni kuboresha maabara ya GST ili maabara hiyo iwe kiongozi wa shughuli za uchunguzi wa madini nchini
Waziri Mavunde amebainisha kuwa Rais Samia amesikia kilio cha watanzania hivyo ameamua kuwezesha kujenga maabara kubwa na ya Kisasa yenye vifaa vya kisasa itakayojengwa katika eneo la Kizota jijini Dodoma ili kwendana na kasi ya ukuaji wa Sekta ya Madini nchini na matarajio ya wadau kwa ujumla.