134 views 5 mins 0 comments

MHE.MPANGO ATOA MAELEKEZO 10 YA KUBORESHA SEKTA YA NYUKI,APONGEZA WIZARA YA MALIASILI

In KITAIFA
May 20, 2024



Na John Mapepele.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango ametoa maelekezo kumi yatasaidia kuimarisha sekta ya nyuki ili iweze kuchangia mapato ya Serikali na kwenye uchumi wa taifa kwa ujumla.


Mhe. Mpango ametoa  maelekezo hayo leo Mei 20,2024 kwa wadau mbalimbali wa sekta hiyo   kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya nyuki duniani iliyofanyika jijini Dodoma  ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, yeye mwenyewe na Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Mizengo Pinda  wamepewa tuzo maalum na Wizara ya Maliasili na Utalii  kwa kuthamini na kutambua mchango wao kwenye sekta.


Katika maelekezo yake ameitaka Wizara  ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana Wizara ya TAMISEMI kuyatambua  maeneo  maalum yenye fursa  za kipekee katika eneo la mkoa wa Dodoma  na Singida  ili kuyahifadhi kisheria  na kuwaelimisha  wananchi wanaoishi  katika maeneo hayo ambayo yana sifa ya uoto  wa vichaka vya Itigi ambavyo duniani vinapatikana Tanzania na Zambia pekee.


Mhe. Mpango ameitaka Wakala waHuduma za  Misitu Tanzania (TFS) na Mfuko wa Misitu Tanzania(TAFF) kuwawezesha wananchi  kwa kuwapatia mafunzo ya ufugaji nyuki  na kuwapatia mizinga ya kisasa ili waweze kufuga kisasa.

Pia ameelekeza Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania(TAFORI) kufanya tathmini mpya ya sekta ya Misitu na Nyuki ili kuja na  mipango ya kuendeleza sekta hizo.


Aidha, ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii  kwa kushirikiana na wadau wa sekta hiyo kuja na mpango  maalum wa ufugaji wa nyuki,kuendeleza program ya upandaji wa miti ambapo pia ameelekeza TAMISEMI kupitia Halmashauri zake zenye  fursa ya ufugaji nyuki kote nchini kuajiri wataalam watakaotoa huduma ya ugani kwa wananchi na Wizara inayohusika na Kilimo kuandaa mkakati wa uchavushaji katika  mazao.


Kuhusu Wizara ya Fedha , Mhe. Mpango  ameitaka kuangalia namna  ya kupunguza kodi kwenye vifaa  katika mnyororo wa uchakataji wa asali, huku pia akiielekeza  Wizara inayohusika na Mambo ya Nje  kuzielekeza Balozi za Tanzania  katika nchi mbalimbali duniani  kutafuta masoko  ili kupata fedha za kigeni kupitia zao hili la asali.


Wakati huohuo amevitaka vyuo vya mafunzo ya nyuki nchini na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA)kuwatumia wajasiriamali wanaofanya  vizuri  ili kuwafundisha wadau wengi zaidi.

Ametoa rai kwa watanzania wote   kuhamasika   na kuanza kutumia  mazao yatokanayo na nyuki ili kuboresha  afya zao, pia wasanii na waandishi wa habari  kuwatembelea.


Awali, akimkaribisha  Mhe. Mpango, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki  amesema Sekta hiyo kupitia nyuki imekuwa na mchango mkubwa katika eneo la uzalishaji wa mazao ya chakula.

Matokeo ya tafiti mbalimbali zilizofanyika ndani ya Nchi zinaonesha kuwa zaidi asilimia 80 ya mimea ya chakula inayolimwa hapa nchini huchavushwa na nyuki.


Aidha, amesema takwimu zilizopo zinaonesha kuwa sekta ya nyuki pia inachangia takribani ajira 2,000,000 hasa kwenye eneo la ufugaji nyuki, usindikaji na biashara ya mazao ya nyuki katika soko la ndani na nje ya Nchi.
 

Amefafanua kuwa katika maadhimisho ya mwaka huu wizara  yake imedhamiria kuhakikisha kuwa jamii inatambua mchango wa nyuki kwenye afya na maendeleo ambapo, Kaulimbiu ya Kitaifa ya maadhimisho hayo ni “Nyuki kwa Afya na Maendeleo, Tuwatunze.” (#APIMONDIA 2027 Tanzania Ipo Tayari)”.


Maadhimisho hayo pia yamehudhuriwa na   Mhe.  Suleimani Jaffo Waziri wa Ofisi ya Makamu wa RAIS, Muungano na Mazingira, Mhe. Najma Giga, Makamu Mwenyekiti Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Wawakilishi wa wa Wakuu wa Mikoa wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, Dkt. Hassan Abbasi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii na Naibu wake CP. Benedict Wakulyamba, Wakuu wa Wilaya za Dodoma, Wakuu wa Taasisi,Viongozi wa dini na Viongozi wa vyama vya siasa, huku yakitanguliwa na maonesho maalum ya wadau wa sekta ya nyuki.

/ Published posts: 1435

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram