240 views 3 mins 0 comments

SERIKALI ITAENDELEA KUTOA ELIMU KWA WANANCHI WANAOISHI NDANI YA ENEO LA NGORONGORO

In KITAIFA
May 27, 2024

Na Mwandishi wetu WAMACHINGA

Serikali imesema itaendelea kutoa elimu kwa wananchi wanaoishi ndani ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro juu ya faida za kuhama kwa hiari wilayani Ngorongoro, mkoani Arusha, kwenda vijiji vya Msomera wilayani Handeni na Saunyi wilayani Kilindi mkoani Tanga na Kitwai wilayani Simanjiro, mkoani Manyara pamoja na maeneo mengine.

Akizungumza leo 26 mei 2024 juu ya zoezi la kuwahamisha kwa hiari wakazi hao wanaoishi katika Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali, bwana Mobhare Matinyi amesema serikali itaendelea na zoezi la uelimishaji, uhamasishaji na uandikishaji Ili kufanikisha mpango huu wa kuwahamisha wananchi kwa hiari na kwa kujali haki za binadamu.

“Ili kufanikisha mpango huu Serikali na NCAA ziliamua kuweka mkakati maalum wa uelimishaji, uhamasishaji na uandikishaji ukijumuisha viongozi na watendaji wa serikali za mitaa ndani ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro juu ya kuhama kwa kwa hiari na kujali haki za binadamu”. Alisema Bw.
Matinyi.

Alisema tayali Timu ya uelimishaji, uhamasishaji na uandikishaji kwa kushirikiana na wataalamu wa ustawi wa jamii kutoka Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru na imeshawafikia wananchi wengi wanaohusika na zoezi hili kwa kutembelea nyumba za ibada, minada, mikutano ya hadhara na kukutana na baadhi ya viongozi wa kimila, watu maarufu na wenyeviti wa vitongoji na vijiji.

Bw. Matinyi alibainisha kuwa katika mpango Mkakati huu serikali imezigawa kanda tano ambazo ni kanda ya kaskazini, kusini, mashariki, magharibi na kati mwa tarafa ya Ngorongoro ili kuhakikisha kata zote 11 na vijiji vyake na vitongoji zinafikiwa. Wilaya nzima ina kata 28 ambapo tarafa ya Loliondo ina nane na Sale kata tisa.

“Lengo la mikakati yote hii ni kuhakikisha kuwa wananchi wanauelewa mpango huu wa uhamaji wa hiari unaojali haki za binadamu, umuhimu wa uhifadhi, sababu zake, ikiwemo faida ya utekelezaji wake kwa lengo la kuondoa hofu na mashaka kwa wananchi wa Ngorongoro, nchi yetu na jumuiya ya kimataifa”. Alisema na kuongeza kuwa

” Uandikishaji wananchi wanaohama kwa hiari utazingatia nani ni mkuu wa kaya na idadi ya wategemezi, mali na maendelezo yaliyofanywa na kaya, idadi ya mifugo na utambulisho wa makazi kwa kutumia nukta za kijiografia. Taarifa zote hizi huwekwa katika vishikwambi vyenye mfumo uliobuniwa na wataalamu wetu wa Tehama uitwao Ngoromso”.

Akizungumzia Awamu ya pili ya zoezi hilo bw. Matinyi amesema imekuwa na mafanikio makubwa kwani tangu Aprili 2023 hadi Aprili 2024 jumla ya kaya 793 zimeandikishwa kutoka katika kata na vijiji vyote vya tarafa ya Ngorongoro. Vijiji ambavyo vimekuwa na mwamko mkubwa ni Vijiji vya Olpiro na Masamburai vilivyopo katika kata ya Eyasi pamoja na Naiyobi na Kapenjiro kwenye kata ya Naiyobi.

Alisema mpaka sasa kaya 160 tu zilizoandikishwa ndizo bado hazijahama ambapo 67 kati ya hizo zinasubiri uthamini na 93 zinakamilishiwa taratibu za kuhama.

/ Published posts: 1414

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram