Na Madina Mohammed DAR ES SALAAM WAMACHINGA
Msanii wa Filamu Nchini, Steven Mengere ametoa shukrani za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.Samia Suluhu kwa kutambua Tasnia ya Filamu na kuja na ahadi ya kuwapeleka wasanii na waigizaji nchi za nje kwa ajili ya kujifunza Sanaa katika nyanja mbalimbali.
Akizungumza katika Mkutano uliofanyika jijini Dar es Salaam uliojumuisha wadau wa filamu na wasanii mbalimbali, amesema kuwa chama cha Waigizaji na wasanii kwa ujumla wanashukuru kwa kitendo cha Rais kuwatambua na kuja na lengo la kuchukua wasanii kisha kuwapeleka nje ya nchi kwa ajili ya mafunzo na kujifunza namna ya uandaaji wa filamu na kazi za sanaa kwa ujumla.
“Ni furaha iliyoje kuona mkuu wa nchi kutambua thamani ya wasanii na waigizaji kisha kuja na nia njema ya kutanua uwanda wa filamu na sanaaa kwa ujumla!. Sisi kama wasanii tumeona ni upendo uliopitiliza kwetu.” alisema Mengere.
Kwa upande wa Mwanamziki na muandaaji wa filamu nchini, Asha Baraka, amesema kuwa kitendo cha mama wa nchi kuja na wazo la kupeleka wasanii nje wakajifunze sanaa zaidi ni kitendo cha kuheshimu na kushangaza kwani mafunzo hayo yataleta mapinduzi ya sanaa nchini kwetu.
Hata hivyo, Msemaji wa chama cha waigizaji nchini, Jimmy Mafufu, amewaomba wadau wa sanaa nchini kutoa ushirikiano kwa Rais ili kuweza kuboresha sanaa ambapo nafasi hiyo ya mafunzo itafanya nchi yetu kutambulika nchi za kigeni.
” Nawasihi wasanii kutoa ushirikiano ili kurahisisha Mapinduzi na ubora wa Sanaa katika nchi yetu ya Tanzania ambapo fursa hii ni adhimu katika kiwanda cha uaandaaji na mchakato mzima wa kazi za kisanii.” amesema Mafufu.