229 views 2 mins 0 comments

SERIKALI KUONGEZA UZALISHAJI WA MBEGU ZA MITI YA ASILI ILI KUZUIA KUTOWEKA

In KITAIFA
June 28, 2024

Na Happiness Shayo Dodoma

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) amesema kuwa katika kuhakikisha kunakuwapo na vyanzo endelevu vya uzalishaji wa mbegu bora za miti sambamba na ulimaji miti hiyo kibiashara, Serikali kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imeanzisha upandaji wa miti jamii ya Mninga katika mashamba yake ya Miti ya Ruvu lililoko Kibaha – Pwani, Mpepo lililoko Nyasa – Ruvuma na Shamba la Mbegu za miti Kising’a lililoko Mkoa wa Iringa.

Ameyasema hayo leo Bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Sikonge, Mhe. Joseph George Kakunda aliyetaka kujua lini Serikali itazalisha mbegu za Mti wa Mninga ili kufanya mti huo kuwa zao la kibiashara.


Ameongeza kuwa Serikali kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imefanikiwa kuzalisha na kugawa kwa wadau mbalimbali jumla ya miche ya mninga 5,115 kwa kipindi cha mwaka 2021 hadi 2024.



’’Kwa Mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali kupitia TFS ilikusanya jumla ya kilo 237 za mbegu za Mninga kutoka katika vyanzo mbalimbali na  ilifanikiwa kuzalisha na kugawa kwa wadau mbalimbali jumla ya miche ya mninga 5,115” alisisitiza.


Amesema pamoja na jitihada hizo, Serikali imejizatiti kuongeza ukusanyaji wa mbegu, kuotesha na kusambaza mbegu bora na miche ya Mninga kwa wadau mbalimbali kupitia vituo vyake vya uzalishaji mbegu za miti.

Aidha, amesema Serikali itaendelea kuhamasisha taasisi za sekta binafsi pamoja na muungano wa wananchi kupitia vyama mbalimbali vya wakulima wa miti ili waweze kupanda miti hiyo ambayo inaweza kuwa adimu na kutoweka badala ya kupoteza fedha kuagiza mbegu za miche kutoka nchi za jirani kama Zimbabwe.

Katika hatua nyingine, Waziri Kairuki ameweka bayana kuwa Tanzania imekuwa ikipokea wageni kutoka nchi za jirani wakija kujifunza kuhusu upandaji miti na hivyo Serikali itajitosheleza katika mbegu hizo za miti bora ambayo imeanza kupotea kwa mahitaji ya ndani na kuuza nje ili kupata fedha za kigeni.

/ Published posts: 1525

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram