184 views 5 mins 0 comments

DOYO ACHAFUKWA AMSHUSHIA LAWAMA HAMAD RASHID KUWA CHAMA CHA ADC SIO CHA UKOO

In KITAIFA
July 01, 2024

Na Mwandishi wetu WAMACHINGA DAR ES SALAAM

Aliyekuwa Mgombea waย  nafasi ya Mwenyekiti wa Taifa wa Chama Cha Alliance For Democratic Change (ADC) Doyo Hassan Doyo amesema hayatambui matokeo ya uchaguzi yaliyomtangaza Shaban Itutu kama Mwenyekiti wa Chama kutokana na uchaguzi huo kutozingatia katiba ya Chama hicho.

Doyo Hassan Doyo ambaye alionekana kutokuwa na upinzani wowote ndani ya Chama hicho na kupewa nafasi Kubwa ya Ushindi wa nafasi ya Mwenyekiti wa Taifa ametoa kauli ya kutoutambua uchaguzi huo uliofanyika June 29 mwaka huu Jijini Dar Es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa Habari ambapo amemtupia lawama aliyekuwa mwenyekiti wa Chama hicho Hamad Rashid Kwa kuvunjwa Kwa kanuni za uchaguzi.

Amesema yeye pomoja na wanachama wengine zaidi ya 70 tayari wameshakata rufaa ya kupinga matokeo hayo kwenye kamati ya rufaa ya ADC ili kupata haki ambayo hawakuipata katika Uchaguzi huo ambao amedai uligubikwa na sintofahamu Kubwa.

“Jana saa 10 kasoro tulipeleka notisi kwa Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi na dakika chache baadaye tukawasilisha rufaa ya kupinga matokeo Kwa mujibu wa kanuni za chama chetu kwani aliyekuwa Mwenyekiti Wetu Hamad Rashid alivunja kanuni za uchaguzi na anataka kukigeuza chama kuwa kikundi Cha familia yake”amesema Doyo.

Akizungumza kuhusu sababu kuu zilizomfanya kuyakataa matokeo ya uchaguzi huo na Kukata rufaa amesema kuwa ni pamoja na kitendo Cha Hamad Rashid kungoza kikao kama Mwenyekiti wa muda na kusimamia tangu mwanzo Hadi mwisho wa zoezi la uchaguzi bila hata kumtangaza mshindi wa nafasi ya Mwenyekiti wa Taifa wa Chama Jambo ambalo limekwenda kinyume na katiba ya Chama hicho ya mwaka 2019.

“Yaan haiwezekani eti Msimamizi wa muda wa uchaguzi amekaa pale ukumbini mpaka saa 3 usiku na haya ninayoyaongea,bahati nzuri Naibu msajili wa vyama vya Siasa aliyashuhudia maana alikuwepo pale,Hamad Rashid ndiye aliyeongoza mkutano mkuu,Kwa hiyo Kwa Habari ya kuvunjwa kwa katiba ameshuhudia Naibu msajili kuwa aliyesimamia Mkutanoย  hakuwa anatakiwa kusimamia ” ameongeza Doyo na kuongeza,

“Sasa Madai yetu ni Nini?Madai yetu tunatamka rasmi kuwa uchaguzi ule ni batili,hatuutambui na matokeo yake na waliyotangazwa na tunataka uchaguzi ule urejewe,tukipige tena,ukiwa chini ya Msimamizi wa msajili wa vyama vya Siasa ndiye tunayemuamini peke yake,na kama mpinzani wangu akifikisha asilimia 20 njoni mnitukane kwani pamoja na njama zote nimepata kura 70 siyo suala dogo”amesisitiza Doyo huku akionyesha sura ya tabasamu.

Hata hivyo Doyo amelalamikia hujuma alizofanyiwa na Hamad Rashid ambaye alimuamini na hakujua kuwa Iko siku atamfanyia hujuma ili asiwe Mwenyekiti wa Chama na kuongeza kuwa,

Kwa kuwa yeye amekata rufaa Kwa mujibu wa katiba ya chama hicho Bado anasalia katika nafasi yake aliyekuwa nayo kama Katibu Mkuu wa chama mpaka pale rufaa yake itakaposikilizwa na Kutolewa maamuzi kwani Wana ushahidi wote ukiwemo wa picha jongefu (video) wa jinsi uchaguzi ulivyokwenda kinyume na katiba ya Chama huku akimtuhumu Hamad Rashid Kuweka safu ya uongozi ikiongozwa na mtoto wake,dereva wake na mkwe wake Jambo ambalo amedai ADC siyo chama Cha familia

“Mimi Nina Kadi namba 2 ya chama yaani ni miongoni Mwa waaasisi wake Sasa Leo mtu asije akataka kukigeuza chama kama genge la familia yake,chama hichi na Cha wote na sijakata rufaa Kwa kuwa eti nimeshindwa uchaguzi Bali ni Kwa sababu Katiba ya Chama ilivunjwa katika zoezi Zima la uchaguzi”amesema.

Kwa upande wake aliyekuwa Mgombea wa nafasi ya Makamo mwenyekiti wa ADC, Zanzibar Bi Shara Amrani Hamis amemshushia lawama aliyekuwa mwenyekiti wa Chama hicho Hamad Rashid Kwa kutowapa Wapiga kura faragha na badala yake baadhi ya wasimamizi wa uchaguzi walikuwa wakiwafuata Wapiga kura wakati zoezi la upigaji kura likiendelea wakiwaambia wamchague Fulani katika uchaguzi huo.

Bi Shara ameongeza kuwa Hamad Rashid alimpigia simu kutaka asigombee nafasi hiyo ili nafasi hiyo agombee mtoto wake Jambo ambalo ni kinyume Cha taratibu,kanuni na katiba ya chama ambayo inampa mwanachama yoyote fursa ya kugombea.

Naye Mwenyekiti wa Vijana wa Chama hicho amesema kuwa wamekata rufaa ya kukukataa uchaguzi huo kwani ulitawaliwa na nguvu za Mwenyekiti aliyemaliza muda wake huku baadhi ya watu akiwemo yeye kuahidiwa kupewa vyeo ili kuzibwa midomo Jambo ambalo wamelikataa kwa kudai kuwa hawana uchu wa madaraka na wanataka haki itendeke.

Amesema wanaamini kuwa kamati ya uchaguzi itatenda haki Kwa Hassan Doyo kwani ushahidi wote wa jinsi Uchaguzi huo ulivyokiukwa unaonekana dhahiri.

/ Published posts: 1435

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram