

Na Mwandishi wetu WAMACHINGA
WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Dk. Selemani Jafo, amewahakikishia wafanyabiashara wa Tanzania kufanya uratibu mzuri wa shughuli za kibiashara ili kuleta faida kubwa sana katika nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumaliza kikao cha pamoja kilichowashirikisha watendaji wa Wizara ya viwanda na Biashara ya Tanzania na Wizara ya Biashara Maendeleo ya Viwanda ya Zanzibar kikao cha mashirikiano kilichofanyika katika hoteli ya Verde Mjini Unguja.
Alisema, eneo la biashara linaajiri watu wengi hivyo endapo biashara ikiendelea kuimarika itasaidia vijana wengi kuweza kupata fursa ya kujiingiza katika biashara.
Akizungumzia upande wa wawekezaji Waziri Dk. Jafo, alisema, jambo la kuendeleza viwanda ni jambo la msingi kwani watu walioajiriwa kwa upande wa serikali ni wa chache na watu wengi wapo katika viwanda.
Hivyo, alisema ipo kila sababu ya kuhakikisha sekta ya viwanda nchini inaimarika na kuwahakikisha katika kipindi kifupi atahakikisha msimamo wa serikali viwanda vinafanya kazi kwa nafasi yake nzuri zaidi lengo kuu uwekezaji Tanzania iwendelee vizuri.
Sambamba na hayo alisema kupitia nafasi hiyo atahakikisha viwanda vinafanya vizuri na viwanda vinaimarika ili vijana waweze kupata ajira kwa kujenga uchumi wao wa mmoja mmoja.
Akizungumzia suala la wafanyabiashara wa Kariakoo, alisema, ataimarisha na kuboresha eneo kariakoo ili nchi iweze kupata mapato zaidi kwani kumekuwa kunafanyika biashara kubwa katika eneo hilo.
“Tutaanza kufanya kazi kwa kufanya vikao hivyo tunaamini suala hili litakwenda vizuri” alisema.
Hivyo, alisema serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imejipanga uwahudumia wafanyabiashara vizuri, hivyo aliwaomba wafanyabishara hao kufanya biashara katika mazingira mazuri huku akiwahakikisha kukutana nao mara kwa mara ili kuondosha changamoto zilizopo sambamba na kuona kuona biashara inaendeshwa vizuri kwa maslahi mapana ya wafanyabiashara na Taifa hasa katika ukusanyaji wa kodi.
Sambamba na hayo, aliwaomba watendaji wa wizara hizo kuendelea kumpa ushirikiano wa hali ya juu ili kuhakikisha kazi zinafanywa kama ilivyotakiwa na viwanda vinakuwa nchini kwani uchumi wa nchi utaendelea kuimarika kupitia viwanda vilivyokuwepo nchini.
Pamoja na hayo, alisema atakuwa nao bega kwa bega watendaji wa sekta binafsi hasa wawekezaji kwa kuwapa ushirikiano wa hali ya juu sambamba na kukaa nao vikao kwa ajili ya kujadili sekta yao na kufikia lengo la Dk.Samia katika kuinua uchumi wa nchi.
Nae, Katibu Mkuu wizara ya Viwanda na Biashara, Dk.Hashil Abdallah, alisema, atahakikisha wanaendelea kumpa ushirikiano wa kutoka waziri Dk. Jafo, sambamba na kumshukuru Dk. Samia kwa miongozo wanayowapa katika wizara yao.
Hivyo, alisema wataendelea kufanya kazi kwa ushirikiano zaidi ili kuona sekta ya viwanda na Biashara inakuwa zaidi na changamoto zilizokuwepo zinatatulika siku hadi siku.
Mapema, Katibu Mkuu Wizara ya Biashara maendeleo ya viwanda, Fatma Mabrouk Khamis, alisema, atahakikisha wizara hizo mbili zitafanya kazi kwa ushirikino zaidi ili kuona sekta ya biashara inakuwa na kuimarika ili uchumi wa nchi uendelee kuwa mzuri na bora zaidi.