Na Madina Mohammed DAR ES SALAAM WAMACHINGA
Mwanasheria wa Chama Cha Alliance For Democratic Change (ADC), ambaye pia Mjumbe wa Kamati ya Rufaa wa chama hicho, John Mbogo amesema wamejipanga kufanya mabadiliko madogo katika Katiba na Kanuni zinazohusu mchakato wa uchaguzi ili kuondoa migogoro kutokea baada ya kufanyika chaguzi ndani ya chama hicho.
Akizungumza makao makuu ya chama hicho buguruni jijini Dar es Salaam amesema Kamati hiyo imejipanga viziri kuendelea na mchakato wa maridhiano kati ya pande zote mbili mara baada ya kupitia rufaa kutoka kwa moja ya wanachama ambayo ilikuwa na hoja saba za kupinga uchaguzi na matokeo yake kufatia kukiukwa kwa Katiba na Kanuni za uchaguzi katika uliofanyika Juni 29 mwaka huu.
Katika uchaguzi huo, Shabani Itutu alifanikiwa kushika nafasi ya uenyekiti kwa kupata kura 121 na mpinzani wake, Doyo Hassan Doyo akipata kura 70, na ndani ya saa 48 kama katiba inavyotaka, Doyo akakata rufaa kupinga matokeo na uchaguzi huo.
“Ndani ya chama kuna taratibu tunazifanya ya kufanya mabadiliko na katika kikao cha nyuma cha mkutano mkuu, tulichokifanya mojawapo na agenda tulizokubaliana ni kubadilisha kanuni, miongozo na katiba yetu.
“Pia tumekubaliana kufanya mapitio ya changamoto tulizoziona katiba chaguzi mbalimbali kwa maana hiyo tutegemee kuwa na kupata katiba bora kama hii ambayo imeweza kuigwa na vyama zaidi ya nane katika kujiendesha hivyo kutakuwa na kitu kipya kwenye mabadiliko ya katiba yetu”, Alisema Bw. Mbogo.
Awali mjumbe wa kamati hiyo, Said Miraji alifafanua kuwa walipokea rufaa ya Doyo akiwasilisha malalamiko yake kwa awamu mbili, ya kwanza yaliwasilishwa Juni 30, 2024 na mengine yaliwasilishwa Julai Mosi, 2024 ambayo kwa pamoja yalikuwa ndani ya muda sahihi kisheria.
Miraji alifafanua kuwa baada ya kupokea rufaa hiyo iliwasiliana na upande wa pili na wao wakawasilisha mapingamizi ya kusikilizwa kwa rufaa kwa hoja kuwa , Doyo anaingilia uendeshaji wa kazi ya kamati kinyume na sheria za nchi kwa kuzungumza na vyombo vya habari.
Ameongeza kuwa licha ya kupokea taarifa hizo kamati yake kupokea na kuwasilisha nyaraka kwa wahusika kwa pande zote na kutoa muongozo kuhusu kusikilizwa kwa shauri hilo na Julai sita mwaka huu, kwa mara ya kwanza iliwaita na kuketi kwa pamoja na kukubaliana kufanya upatanisho kabla kuanza kusikilizwa kwa malalamiko.
“Ndg waandishi pande zote mbili zimeridhia kufanya upatanishi kwa maslahi ya mapana ya ADC, hivyo tutawatangazia ndani ya siku tano zijazo namna kamati ilipofikia na maamuzi yake na mchakato wa mariadhiano haya unatokana na misingi mikuu sita ya katiba yetu,” amesema.
Pia alitoa wito kwa vyama vingine vya siasa nchini kufuata mfano wa ADC wa kuunda Kamati ya Rufaa, Usuluhishi, Upatanishi inayowahusisha watu wa nje ya chama wasiokuwa na maslahi ndani ya chaguzi au uongozi ili kutoa haki pale mmoja anapohisi haki yake imedhurumiwa.