Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Mbunge wa Jimbo la Kibakwe, Mhe.George Simbachawene amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa heshima aliyowapa wananchi wa Kibakwe kwa kuwaletea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Mhe. Simbachawene ametoa kauli hiyo leo kwa nyakati tofauti wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Mlunduzi kwenye mikutano ya hadhara iliyofanyika katika Vijiji vya Chinyika, Chaludewa na Chinyanghuku Jimbo la Kibakwe, Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma
Amesema chini ya Uongozi wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan kumekuwa na utitiri wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa katika Jimbo hilo huku akitaja Kata za Milimani ambako ni maeneo magumu kufikika lakini kwa sasa huduma za kijamii zimeendelea kusogezwa kwa kasi.
” Maeneo ya Milimani ikiwemo Kata ya Lufu, Mangaliza na Galigali mwaka 2005 kulikuwa gizani, kulikuwa hakuna barabara punda pekee ndo walitumika kama njia pekee ya usafiri ila kwa sasa kuna barabara za uhakika magari makubwa na madogo yanakwenda bila shida yeyote na sasa zile sehemu korofi TARURA wapo mzigoni wanatengeneza barabara ya zege ” amesema Mhe.Simbachawene.
Mhe. Mhe.Simbachawene amesema “Mambo mazuri zaidi yanakuja, Rais Samia amesema anataka aione Kibakwe yenye nuru kiuchumi nawahakikishieni itabadilika, Maeneo magumu ya Milimani hayakuwa hivi na ninyi ni Mashahidi lakini Rais wetu ametuletea huduma mbalimbali za maendeleo na leo tumepata Barabara pamoja na umeme.
Ameongeza ‘’ hakukuwa na vituo vya afya ila leo vinajengwa, hakukuwa na nishati ya umeme ila leo inafikishwa, mambo mazuri zaidi yanakuja jiandaeni ili kuendana fursa hizo ”
Ameongeza kuwa ” Uwepo wa Taasisi za Umma katika maeneo hayo magumu ya Milimani ikiwemo ujenzi wa Shule za Sekondari unaoendelea Man’galiza Lufu na Galigali kutachagiza maendeleo huku akiwataka wananchi kukaa kimkakati ili wawe wanufaika namba moja wa fursa hizo.
Akizungumzia hatua hizo za maendeleo katika Jimbo zima la Kibakwe Mhe.Simbachawene amesema Kibakwe ya sasa imefunguka kimaendeleo katika nyanja za kiuchumi huku huduma za kimsingi zikiwa zinapatikana mahali popote bila kujali jiografia ya eneo husika.
Amesema ujenzi wa barabara za lami, ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) pamoja na ujenzi wa Vituo vya Afya ni Ushahidi tosha jinsi Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan alivyojitoa kwa wananchi wa Jimbo la Kibakwe.
Katika hatua nyingine, Mhe.Simbachawene amewataka vijana wa Kata ya Mlunduzi hususani Kijiji cha Chinyanghku kuchangamkia fursa ya ajira katika mradi wa maji utakaogharimu zaidi ya Sh.Milioni 900 hadi kukamilika kwake unaoendelea Kijijini hapo.
” Nawaomba vijana mbadilike nendeni mkafanye kazi katika mradi wa maji, ifike hatua wakazi wa maeneo haya muanze kutafuta hela kwa bidii badala ya kubaki watazamaji ilhali vijana wa maeneo mengine wakichangamkia fursa hiyo” amesisitiza Mhe.
Amesema ni aibu kumuona kijana akibeti na kulewa pombe za kienyeji kuanzia asubuhi hadi jioni ilhali kuna fursa ya kuweza kujiongezea kipato amewata wakafanye kazi katika mradi.