104 views 4 mins 0 comments

SIMBA WAKIFUNGWA WAFURAHIE TU: MANARA

In MICHEZO
August 07, 2024

NA Anton Kiteteri


Awambia wanayanga waje waone mpira wa hesabu.


Dar es Salam


KATIKA kuelekea mchezo wa leo wa Ngao ya Jamii kati ya watani wa jadi Simba na Yanga,msemaji wa klabu ya Yanga Haji Manara amewambia wanachama na mashabiki wa Simba wafurahie hata kama watafungwa kwa maana watakuwa wamefungwa na timu bora.


Manara  ambaye ni machachari sana katika kutoa hamasa amesema kuwa Yanga inawaheshimu Simba kwa kuwa ni timu kubwa ila suala la ushindi wa Yanga liko pale pale na wawe tayari kwa matokeo yoyote.


“Simba kesho (leo) wakifungwa wao wafurahie kuwa wamefungwa na timu kubwa,sitegemei mechi imeisha mashabiki wao wahuzunike,wao wafurahie kuwa wamefungwa na timu bora na yenye kikosi bora”,alisema Manara.


Mchezo huo wa ngao ya jamii utachezwa leo kwenye uwanja  wa Benjamini Mkapa majira ya saa 1;00 jioni,ukitanguliwa na mchezo kati ya Azam na Coastal Union mchezo utakaochezwa kwenye uwanja wa Aman Complex majira ya saa 10;00 jioni.


Joto la mchezo huo liko juu sana hasa kwa mashabiki wa klabu ya Simba kutokana na timu yao kuwa mteja kwa Yanga katika msimu wa mwaka  2023/2024 ambapo katika michezo  yote Simba alifungwa.

Katika mchezo wa kwanza Simba alifungwa bao 5-1 huku mchezo wa pili ikiambulia kipigo cha bao 2-1.


Kocha mkuu wa Simba Fadlu Davids akizungumza na waandishi wa habari katika kuelekea kwenye mchezo huo amesema kuwa anaichukulia mechi hiyo kwa umuhimu mkubwa na wanahitaji kushinda ili kuanza msimu wa ligi kwa kutetea kombe hilo ambalo walilichukua mwaka jana.


‘Tunaichukulia mechi hii kama mechi nyingine tunahitaji kushinda ili kuanza vizuri kwa kutetea kombe hili,nina uzoefu wa michezo hii mikubwa ya Dabi,ukiangalia timu yetu ni mpya tutakuja na mbinu tofauti kuhakikisha tunapata matokeo mazuri’,alieleza  kocha Davids.


Kwa upande wake nahodha wa timu hiyo Mohamed Hussein Tshabalala amesema kwa msimu huu wamejiandaa vya kutosha na wana hakika na ana hakika mchezo utakuwa na ushindani mkubwa kutokana na wapinzani wao kuwa kikosi bora.
“Kulingana na maandalizi tuliyoyafanya timu yetu imeimarika zaidi ila tuna imani tunaenda kukutana na timu yenye wachezaji wazuri ,utakuwa mchezo wenye ushindani ila malengo yetu kesho (leo)’,alifafanua Tshabalala.


Kocha mkuu wa Yanga Miguel Gamondi ameeleza kuwa timu yake ipo tayari kwa pamoja na kuahidi kuwapa mashabiki kile wanachokitarajia kutoka kwao.Amesema kuwa anaandaa timu yake  kwa 75% na 25% pekee ndio hutumia kumfuatilia mpinzani wake.


“Tupo imara kiakili na kimwili ,tumejiandaa vya kutosha hakuna tunachohofia ,sijapata wasaa mzuri wa kutazama wapinzani kwani mechi zao nyingi hazikuoneshwa lakini sio changamoto kubwa kwani naandaa timu yangu kwa 75% na 25% ndio natumia kumchunguza mpinzani”,alifafnua Gamondi.


Mchezo huo licha kuwa unatafuta mshindi atakayecheza na mshindi kati ya Azam na Coastal Union ili kupata bingwa wa Ngao ya jamii,pia itakuwa ni  kipimo bora kwa kocha wa Simba Fadlu Davids iwapo atatibu majeraha ya wanasimba ambayo wamekuwa nayo takribani misimu mitatu bila kombe lolote.


Simba inaingia katika mchezo huo ikiwa na presha ya kuishinda Yanga na kufuta uteja wa kufungwa mara mbili mfufulizo na pia ikilenga kurudisha heshima yake iliyopotea kwa kipindi kirefu bila kupata kombe lolote.Kushinda kwa Simba kwenye mchezo wa leo kutajenga imani ya wanachama wake ambayo kwa sehemu kubwa imepotoa kutokana na timu hiyo kutokufanya vizuri kwenye  mashindano yoyote.


Katika mchezo wa Simba day waliifunga APR ya Rwanda bao 2-0 huku Yanga katika kilele cha mwananchi waliifunga Red Arrows bao 2-1 hali ambayo inaongeza ushindani kwenye mchezo huo.Mchezo huo utachezeshwa na mwamuzi  Sasii.

/ Published posts: 1414

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram