54 views 3 mins 0 comments

TUGHE YATOA RAI KWA WAAJIRI KUWAPA WAFANYAKAZI HAKI YA KUJIUNGA NA VYAMA VYA WAFANYAKAZI

In BIASHARA
August 27, 2024

Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA
——————————————
Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) kimetoa rai kwa Waajiri nchini kuwapa wafanyakazi wao haki ya kujiunga na Vyama vya Wafanyakazi ili kuleta tija katika maeneo ya kazi.

Akitoa salamu za TUGHE katika ufunguzi wa Semina ya Waajiri na Viongozi wa Matawi ya TUGHE iliyoanza jana Jumatatu Tarehe 26 Agosti 2024, Jijini Arusha, Katibu Mkuu wa TUGHE, Cde. Hery Mkunda amesema kuwa Vyama vya Wafanyakazi ni wadau muhimu sana katika kuchangia maendeleo ya Taasisi.



Akizungumzia kuhusu Semina ya Waajiri na Viongozi wa Matawi ya TUGHE, Cde. Mkunda alieleza kuwa tangu mwaka 2018, TUGHE imekuwa na utaratibu wa kuandaa na kuratibu mafunzo ya pamoja yanayojumuisha washiriki toka Viongozi wa Matawi ya Chama na Mamlaka za Ajira au wawakilishi wao.



“Kwa niaba ya TUGHE niwashukuru sana Waajiri na Viongozi wa Matawi ya TUGHE kwa kukubali kuwezesha na kushiriki mafunzo haya ambapo tayari matunda ya uwepo wa mafunzo haya ya kila mwaka yameanza kuonekana kwani Migogoro baina ya Watumishi na Waajiri imepungua sana na pale ilipojitokeza imekuwa ikipata utatuzi kwa njia ya majadiliano mahala pa kazi.”Cde. Mkunda



Mgeni Rasmi alikuwa Mwenyekiti wa TUGHE Taifa, Ndg. Joel Kaminyoge, ambae pamoja na mambo mengine alisisitiza umuhimu wa kuhubiri wajibu na haki sehemu za kazi.

Nae Afisa Mtendaji Mkuu wa ATE, Bi. Suzanne Ndomba-Doran akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina hiyo alisisitiza kuwa mada ya Haki za Msingi za Vyama vya Wafanyakazi ni elimu muhimu kwa Wanachama kwani wanapaswa kufahamu wajibu kwasababu hakuna haki bila wajibu na aliendelea kueleza kuwa Vyama Vya Wafanyakazi vina wajibu mkubwa wa kuleta utilivu,ufanisi na ukuaji wa tija sehemu za kazi na kuboresha mazingira na mahusiano mazuri baina ya Mwajiri na Mfanyakazi.



Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi Khadija Mwenda, ameipongeza TUGHE kwa kuandaa mafunzo hayo na kusisitiza kuwa amesisitiza kuwa kama nchi tunahitaji kuwa na nguvukazi yenye afya njema ili kuleta tija katika maeneo ya kazi hivyo nsuala la Afya na Usalama ni muhimu kuwa Agenda endelevu .



Mafunzo haya ya siku nne yamewakutanisha washiriki kutoka sehemu mbalimbali za kazi zikiwemo Wizara, Idara, Taasisi, Wakala wa Serikali, Mamlaka za Serikali, Bunge, Mahakama, Sekretarieti za Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa na Taasisi za Afya za Serikali na zile za binafasi. Mafunzo hayo yatahitimishwa kwa Washiriki kufanya utalii wa ndani kwa kupata fursa ya kutembelea hifadhi ya  Taifa Ngorongoro.

/ Published posts: 1525

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram