99 views 7 mins 0 comments

SAMIA ARUSHA KOMBORA KWA WAPINZANI

In KITAIFA
September 26, 2024

Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA

RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan, amevunja ukimya na kurusha kombora kwa vyama vya upinzani nchini.

Kutokana na hali hiyo amesema kuwa viongozi wa vyama hivyo sasa wamekosa pa kupenyea na badala yake wanaibuka na hoja za kutaka kuvuruga Taifa.

Akizungumza na wananchi jana Wilayani Mbinga mkoani Ruvuma, Rais Dkt. Samia, alisema kuwa suala la amani na utulivu ni kipaumbele kwa nchi.



“Amani na utulivu ndiyo inayotufanya hata majumbani tucheke, tukae vizuri tuangalie michezo ya kwenye runinga, kukiharibika hayo yote hayapo.

“Niombe sana, wale wanaokuja kuwashawishi kwa neno lolote lile kwa sababu yoyote ile kuharibu amani na utulivu wa eneo lenu msikubaliane nao, ninataka kuwaambia kuwa wameishiwa, hawana pa kupenya, wameshaona mbele mambo magumu kwao, sasa wanalolifanya ni kuharibu amani na utulivu wa nchi yetu ili wananchi waishi kwa mashaka, muone nchi yenu siyo njema, ndiyo lengo lao, niwaombe sana msikubaliane nao.

“Ndugu zangu wananchi ili tuendelee kupata tunayoyapata haya miradi ya kila aina, vituo vya umeme na mambo mengine msiende kufanya makosa (kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, Novemba 2024), kwanza dumisheni uhuru na utulivu katika wilaya yenu hii. Amani na utulivu ndiyo itakayowawezesha kufanya shughuli zenu za maendeleo, ndiyo itakayowawezesha muweze kwenda shambani kulima vizuri, kuvuna vizuri na kuja kuuza hapa (Kituo cha manunuzi ya mahindi cha Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA)) kwa raha kabisa,” alisema Rais Samia

Akizungumzia kuhusu Serikali itaendelea kupeleka fedha za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alisema hayo mbele ya wakazi wa Mbinga alipotembelea kituo cha manunuzi ya mahindi cha Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Matika Mbinga Mjini Mkoani Ruvuma.

“Serikali imeendelea kuleta fedha nyingi sana kama ilivyotajwa hapa na Waheshimiwa wabunge kwa ajli ya maendeleo na huduma za jamii kwa jamii yetu iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga.

KERO ZA WANANCHI

“Hivyo niwatake watendaji kusimamia miradi na watendaji ni pamoja na madiwani, muendelee kuweka nguvu kusimamia miradi ili yale yanayowakera wananchi yaweze kuondoka. Utumishi wetu mimi na nyinyi kuhudumia wananchi, sisi ni watumishi wa wananchi na si mabwana wa wananchi, si watawala wa wananchi, sisi ni watumishi kwa wananchi.

“Ndiyo maana serikali inashusha fedha nyingi ili zifanyiwe kazi wananchi hawa waondoshewe shida zao,” alisema Rais Samia

Mkuu huyo wa nchi alisisitiza kwa kuitaka Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kuhakikisha jengo jipya la ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji linatumika kwa malengo yaliyokusudiwa, likiwemo kuboresha mazingira ya kazi na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Rais Samia amewasihi maafisa wa halmashauri kutumia ofisi hiyo kwa weledi na kwa kutatua kero za wananchi kwa upendo na uwajibikaji.

“Madhumuni ya serikali kujenga nyumba hizi ni kuleta mazingira mazuri kwa maafisa wetu wanaofanya kazi ndani ya halmashauri hii,” alisema Rais Samia.

Aidha alisisitiza kuwa majengo hayo ya kisasa yamewekwa miundombinu bora kwa lengo la kurahisisha utendaji kazi, na kutoa wito kwa watumishi kuwatumikia wananchi kwa weledi ili kuhakikisha huduma zinazoendana na ubora wa jengo hilo zinatolewa.

“Ofisi hizi zitumike kuondoa kero za wananchi. Mkurugenzi Mtendaji na watumishi wote muweze kulitunza jengo hili kama lilivyo leo, kila tukija lionekane hivihivi,” alisisitiza.

Rais Samia pia ameongeza kuwa lengo ni kuhakikisha kuwa wananchi wanaokuja kutafuta huduma katika ofisi hiyo wanatoka wakiwa wameridhika, tofauti na walivyoingia.

“Tunataka wakiingia wamekasirika kwa shida, wakitoka wafurahi, wapendeze kama linavyopendeza hili jengo,” alisema Rais Samia.

WITO KWA WAKULIMA

Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, alitoa wito kwa wakulima kubadilika na kuepuka kuuza mazao yao kwa walanguzi kwa bei ndogo, ili waweze kupata faida nzuri kupitia vituo vya serikali.

“Ahadi yetu kwenu ni kuendelea kuondoa hizi shida za wananchi. Serikali inajitahidi kuboresha hali ya wakulima kila inapobaini changamoto, lakini pia aliwasihi wakulima kubadilisha mtazamo wao kuhusu masoko.

“Kwa mfano, serikali imeweka vituo kadhaa vya kununua mahindi kwa bei kubwa. Sasa anapokuja mlanguzi kule kwako akakuta bei ya chini na wewe ukakubali kumpa, isilaumiwe Serikali,” alisema Rais Samia.

Rais Samia liongeza kuwa ni muhimu kwa viongozi wa wilaya kuwafahamisha wakulima kuhusu hatua ambazo serikali imechukua ili kuhakikisha wanapata bei nzuri ya mazao yao na faida ya jasho lao.

“Ninaomba muende mkawafahamishe ili wakulima sasa waweze kuuza kwa bei nzuri, wapate manufaa ya jasho lao, warudishe gharama zao,” alisema

Akielezea umuhimu wa wakulima kuuza mazao yao kwa NFRA badala ya walanguzi, Rais Samia alisema, “Unapokwenda kuuza kwa bei ile ya mlanguzi hupati kitu, unarudisha tu gharama zako ulizoingia, lakini jasho halirudi. Faida haipo. Hutaweza tena kununua mbolea na pembejeo msimu ujao, lakini ukija ukauza NFRA, unapata faida itakayokuwezesha kuweka pesa kidogo za kuweza kununua mambo mengine mbali na matumizi yako binafsi.”

ANGALIZO

Mkuu huyo wa nchi aliwasihi wakulima wa mahindi na kahawa kutumia fedha wanazopata kutokana na mazao hayo kwa uangalifu na kuweka akiba kwa ajili ya maendeleo ya baadaye.

Aliwataka wakulima kuhakikisha wanapanua mashamba yao na kuepuka kutumia vibaya mapato wanayoyapata kutokana na mazao yao.

“Kahawa mnauza bei nzuri sana, niwaombe sana pesa zile tusichezee, ngoma zikaisha. Pesa tuweke akiba kwa mambo ya baadaye, tutanue mashamba zaidi. Leo tunatoa ruzuku, lakini huko mbele pengine tutasema sasa wakulima jitegemeeni,” alisema Rais Samia.

Rais Samia pia amewasihi wakulima kuuza mazao yao kupitia mfumo wa serikali ili kuhakikisha wanapata bei nzuri na kuepuka kudhulumiwa na walanguzi.

“Serikali katika kuwaonea huruma imeleta mtandao wa ununuzi wa mahindi, ninaomba kauzeni kwenye mtandao wa serikali, msije mkatoa mahindi mkaumizwa, mtakuwa mnajiumiza wenyewe. Ukienda kuuza serikalini NFRA unapewa 700 kwa kilo, wakati wakulanguzi wanawapa Shilingi 300 kwa kilo. Hiyo ni kujidhulumu wenyewe,” alisema

Rais Samia alisisiiza umuhimu wa wakulima kutumia vizuri fedha wanazopata ili kuwekeza kwa ajili ya maendeleo ya baadaye.

“Niwaombe tena fedha msiziharibu, maendeleo yanakuja, Mbinga inabadilika, mtataka kufanya uwekezaji. Kwa hiyo, fedha msizichezee,” alisema Rais Samia.

/ Published posts: 1440

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram