Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA
-Awataka viongozi ngazi za Mitaa na Kata kuunga mkono juhudi za Mhe Rais kwa kuisemea vizuri miradi hiyo.
-Atoa Rai kwa wakazi wa DSM kushiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa Novemba 2024
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, leo Septemba 27, 2024 amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa Kituo Cha Afya Kilakala, ujenzi wa zahanati Kurasini, ujenzi wa Ofisi ya Kata Miburani na ujenzi wa bweni Shule ya Sekondari Kibasila.
RC Chalamila ametoa shukrani hizo Leo Septemba 27,2024 wakati wa ziara ya kukagua miradi ya maendeleo na kuongea na wananchi wa Jimbo la Temeke Wilaya ya Temeke.
Vilevile RC Chalamila amewataka viongozi wa ngazi zote za serikali kuisemea miradi hiyo ili wananchi waweze kutambua kazi nzuri inayofanywa na Serikali yao chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Aidha RC Chalamila ametoa ufafanuzi kuhusu matukio ya utekaji na mauwaji ambayo yalitokea katika baadhi ya maeneo ikiwemo Temeke ambapo amesema matukio mengi yanafanyika katika jamii zetu hivyo mlinzi namba moja ni jamii yenyewe, ili kutokomeza matukio haya jamii iwe mstari wa mbele kusimamia ulinzi na usalama katika maeneo yao.
Mwisho RC Chalamila amewahamasisha wananchi kushiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa 2024 kwa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika daftari la mpiga kura pamoja na kugombea nafasi za uongozi.