75 views 7 mins 0 comments

RAIS SAMIA ASHUSHA NEEMA KWA WALIMU

In KITAIFA
October 06, 2024

Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA


-ARUSHA

RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan amepongeza kitendo cha walimu 5000 Jijini Arusha wa Shule za Msingi na Sekondari Jijini Arusha kupatiwa mitungi ya gesi ya Oryx na majiko yake kwa lengo la kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia .

Akizungumza kwa njia ya simu wakati wa hafla ya ugawaji wa mitungi na majiko hayo yaliyotolewa na Mbunge wa Arusha Mjini kwa uratibu wa Kampuni ya Oryx Gas Tanzania , Rais Samia amesema anapongeza walimu hao kupatiwa mitungi ya gesi na yeye ameahidi kuongeza majiko kwa siku za baadae.

“Nimepiga simu niwapongeze walimu kwa Mkutano mzuri , Mbunge (Mrisho Gambo)  ameniambia leo (jana) mna mkutano wa nishati safi ya kupikia kwa hiyo niwapongeze kwa kuibeba hiyo ajenda. Niwaahidi tu mchango wangu katika hilo ndugu walimu  katika majiko yatakayotoka mimi nitakuja kujazia baadae,” alisema Rais Samia huku akiwaeleza pia walimu kuwa ajenda zao na changamoto zao anazifahamu na wanaendelea kuzifanyia kazi.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Omari Kipanga,  aliyekuwa mgeni katika maadhimisho ya walimu jijini Arusha kwa niaba ya Waziri wa Elimu  Profesa Adolf Mkenda alisema wanamshukuru Rais Samia kwa jitihada anazofanya za kuendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

“Katika siku hii ya leo (jana) ya kuadhimisha siku ya walimu kauli mbiu yetu  inahusu masuala ya nishati safi ya kupikia na kama mnavyofahamu Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amezungumza na sisi leo lakini tunakumbuka Mei mwaka huu alizindua kampeni hii ya utumiaji wa nishati safi ya kupikia na malengo yetu kama Serikali ni kuhakikisha itakapofika mwaka 2034 asilimia 80 ya Watanzania wawe wamefikiwa katika matumizi ya nishati safi ya kupikia.

“Hivyo tunamshukuru pia Mbunge wa Arusha Mjini Mrisho Gambo pamoja na Oryx kwa kutoa mitungi ya gesi kwa walimu 5000 ili watumie nishati safi ya kupikia.Kama nilivyosema  kampeni ya Rais aliyotangaza Mei 8,2024 ni kwamba kila Mtanzania atumie nishati safi ya kupikia …

“Na sisi Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia tumelibeba jambo hili na tumeanza na taasis zote za elimu ambazo  zinahudumiwa watu zaidi ya 100 kuanza kutumia nishati safi ya kupikia,kwa hiyo katika shule zetu zote sasa hivi za sekondari na msingi,taasisi zote za elimu kwa sasa wanaunganishwa na nishati safi ya kupikia,” alisema Kipanga

Pia alisema walimu 5000 wa Arusha ambao  wamepatiwa majiko ya gesi wanaandaliwa utaratibu wa kupatia elimu ya matumizi sahihi ya nishati  waweze kuishusha kule chini kwa wananchi na wote tutumie nishati safi ya kupikia.

“Niwape taarifa  Dkt. Samia Suluhu Hassan alishatoa elimu ya nishati safi ya kupikia  kwa Wabunge wote na katika Bunge lililopita kila Mbunge alipewa majiko 200 kwa ajili ya kwenda kugawa katika majimbo yao na lengo kubwa ilikuwa kuhamasisha wanasiasa lakini kama mnavyofahamu jambo lolote haliwezi kwenda kama hakutakuwa na utashi wa kisiasa,hivyo Rais anatuongoza katika Kampeni hii,” alisema Kipanga.

Awali akizungumza mbele ya walimu pamoja na viongozi wa ngazi mbalimbali Mkurugenzi Mkuu wa Oryx Gas Tanzania, Benoit Araman alisema wameratibu kutolewa kwa mitungi hiyo kwa walimu kwa kuwa wanaamini unapotumia gesi ya kupikia huleta maendeleo makubwa katika jamii.

“Leo hii inaonyesha wazi kwa kampeni hii kukamilika na mkakati wa kuiboresha nchi chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan na Serikali yake.

“Naomba niwagusie waalimu na maprofesa sio tu kwa sababu tunawasherehekea leo siku ya Walimu bali naamini ninyi nyote ni kiungo muhimu kwa jamii na Taifa letu. walimu na maprofesa  mnahakikisha  watoto na vijana wetu wanapewa zana zinazohitajika maishani,ambayo ni elimu,” alisema

Kutokana na hali hiyo, alitoa ombi maalum kwa walimu kuwa mabalozi wa Nishati Safi ya kupikia na kwamba wakizungumza  kuhusu nishati safi ya kupikia kwa wanafunzi wao na katika mikutano ya wazazi itachangia kwa kiasi kikubwa kueneza nishati safi nchini Tanzania.

Alisisitiza kuwa hiyo Inamaana watakuwa wanaisaidia  serikali katika kufikia lengo lake na kuongeza Oryx Gas  ipo katika Mkutano huo kwa ajili ya kuelimisha, kutoa mafunzo na kuwakumbusha kuhusu umuhimu  wa nishati safi na jinsi ya kutumia LPG.

Araman alitaja baadhi ya faida ya nishati safi ni kuboresha afya kwani nchini Tanzania wananchi 33,000 wanakufa kila mwaka kutokana na kuvuta pumzi ya moshi na chembechembe zinazotokana na mkaa na kuni, hivyo kupika kwa gesi ya kupikia oryx itaondoa changamoto hiyo.

Pia kutumia nishati safi husaidia katika ulinzi kwani wananchi wataacha kuharibu mazingira kwa kukata miti kwa ajili ya kuni na mkaa lakini kwa upande wa elimu jamii inapotumia nishati safi ya kupikia hata watoto hawapata muda wa kutosha wa kusoma kwani hawatakuwa wakitumia muda mwingi kwenda kutafuta kuni porini.

Kwa upande wake Mbunge wa Arusha Mjini Mrisho Gambo, alisema wanatambua mchango walimu wote na katika kusherehekea siku ya walimu wameona kuna kıla sababu ya kuwapa zawadi ya jiko la gesi kwa kila mwalimu na wao wakawe mabalozi wa nishati safi.

“Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amezindua mpango wa nishati ya kupikia na bado mpango huo ukaweka malengo mpaka kutoka 2034 asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia.

“Kazi ya Rais ni kuonesha njia na sisi wasaidizi wake ni kumuunga mkono na leo tunakabidhi majiko ya gesi kwa walimu na hii ni kumuonesha mwalimu tunampenda na tunamtambua na sasa wakawe mabalozi wa nishati safi ya kupikia.Tunawashukuru Oryx kwa kumuunga mkono Rais Samia kwani gharama za majiko haya 5000 ni Shilingi milioni 417.5 ,” alisema



Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Omary Kipanga (watatu kushoto) Mbunge wa Arusha Mjini Mrisho Gambo (katikati) Mkurugenzi Mkuu wa Oryx Gas Tanzania Benoit Araman ( wa pili kulia) wakiwa makini kumuangalia mmoja ya walimu jijini Arusha akipika kwa kutumia gesi ya Oryx jana wakati wa maadhimisho ya Siku ya Walimu yaliyotumika pia walimu 5000 kupatiwa majiko ya Oryx kwa lengo la kuhamasisha nishati safi ya kupikia nchini. Na Mpigapicha Wetu

/ Published posts: 1440

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram