54 views 3 mins 0 comments

SHIKAMOO SIMIYU,YAJA NA MITANO TENA

In KITAIFA
October 07, 2024

Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA

Maelfu ya wananchi wa mji wa Bariadi na vitongoji vyake waliofurika kwenye mkutano mkubwa wa hadhara mjini hapo wamemtuma Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, kufikisha salamu zao kwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa wanamhitaji agombee na aendelee kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa miaka mingine mitano katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Umati huo mkubwa wa wananchi ulionesha matamanio hayo kwa kutamka maneno “mitano tena” huku wakinyoosha mikono juu baada ya kuulizwa iwapo kauli zilizotolewa na viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali kuhusu mafanikio ya utekelezaji wa Ilani ya CCM ya 2020-2025 katika sekta mbalimbali za maendeleo kwenye maeneo yao ni za kweli, na wangependa kutuma salamu gani kwa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuthibitisha kuwa uongozi wake umewagusa.

Akizungumza na maelfu ya wananchi na wanachama wa CCM katika mkutano huo uliofanyika katika Uwanja wa CCM Bariadi, mkoani Simiyu, Balozi Nchimbi aliwaahidi kufikisha salamu hizo kwa uzito ule ule walivyomtuma, kwanza kwa wingi wao walivyojitokeza mkutanoni na pili kwa kunyoosha mikono mingi hewani, vyote vikidhihirisha mapenzi yao kwa CCM na Rais Dkt. Samia, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM.

“Leo kila mtu ameona jinsi ambavyo Simiyu mlivyotikisa. Ni mapokezi ya heshima na ni salamu tosha kuwa CCM inakubalika na Dkt. Samia anakubalika sana, na ujumbe wa salamu zenu nimeupokea nitaufikisha. Tumefurahishwa na taarifa za utekelezaji na usimamizi wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM imetekelezwa na kusimamiwa vizuri sana.”

“Nawapongeza Kamati ya Siasa ya Mkoa, ikiongozwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa, Ndugu Shemsa, pamoja na watendaji wote wa Serikali wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa. Wanafanya kazi nzuri sana,” alisema Balozi Dkt. Nchimbi huku akiitikiwa kwa shangwe na vigelegele.

Aidha, Balozi Nchimbi amewaambia wananchi wa Simiyu kuwa Dkt. Samia alivyopokea dhamana ya kuongoza nchi, wapo waliokuwa hawakuamini kuwa miradi iliyoachwa na mtangulizi wake, Hayati John Magufuli, hasa ile mikubwa ya kimkakati, ingekamilika. Lakini kwa sasa kila Mtanzania ni shahidi kuwa miradi yote inaendelea vizuri katika hatua mbalimbali na mingine imekamilika na inatumika.

Balozi Nchimbi pia amewaambia wananchi kuwa adhabu sahihi ya wanasiasa waliofilisika kisera na hoja, wanaohamasisha vurugu katika jamii kwa siasa za udini, ukabila, ukanda na kuchoma moto vitu, ni kuwanyima kura na kuipigia kura nyingi CCM.

Balozi Nchimbi pia amesisitiza wananchi kuwa mstari wa mbele kwenye kulinda amani ya nchi yetu, na inapotokea mtu yeyote anayetaka kuvuruga amani, akemewe kwa ‘macho makavu’ usoni na akataliwe bila kumuonea haya.

Balozi Nchimbi yupo mkoani Simiyu ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara yake mkoani humo, akitarajiwa kufanya ziara kwa siku tatu kabla ya kuelekea Mkoa wa Shinyanga, akiwa ameongozana na Katibu wa NEC-Itikadi Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa, Ndugu Amos Makalla, pamoja na Katibu wa NEC Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Ndugu Rabia Abdalla Hamid.

/ Published posts: 1414

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram