37 views 3 mins 0 comments

TARURA YAVIWEZESHA KIUCHUMI VIKUNDI VYA KIJAMII- LUDEWA

In KITAIFA
October 10, 2024

Na Mwandishi Wetu

Wanaoishi na VVU wajiunga Bima ya Afya (NHIF) kupitia miradi ya TARURA

Ludewa,Njombe

Vikundi vya Kijamii vinavyofanya kazi za ujenzi na matengenezo madogo madogo ya miundombinu ya barabara wilayani Ludewa wameishukuru Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa kuwapatia kazi ambazo zimeweza kuwainua kiuchumi.

Wakiongea wakati wa ziara ya Ujumbe kutoka Jamhuri ya Siera Leone waliofika Kata ya Lugarawa na kutembelea vikundi vinavyofanya kazi za ujenzi na matengenezo ya barabara katika kata hiyo wanakikundi hao wamesema tangu waingie mikataba na Tarura wamenufaika katika nyanja mbalimbali ikiwemo ukuaji kiuchumi.

Mwenyekiti wa kikundi cha โ€˜Tujipimeโ€™ ambacho kina wanachama 22 wanaoishi na VVU Bw. Manyanya Mkinga amesema tangu kikundi chao kuliposajiliwa mwaka 2019 wamefanikiwa kupata manufaa mbalimbali kupitia zabuni za TARURA wanazopata.

โ€œTuliona tukiungana hatuwezi kunyanyapaliwa wala kujinyanyapaa wenyewe hivyo kwa kazi hizi tunazopata za TARURA kwakweli tumeweza kuboresha maisha yetu, licha ya kuishi na VVU tumefanikiwa kufanya kazi kwa ukamilfu, tunawashukuru sana TARURA kwa kutuwezesha kupata kazi.” Amesema Mkinga.

Ametaja manufaa waliyoyapata tangu walipoanza kufanya kazi za TARURA mwaka 2020 ni pamoja na ujenzi wa nyumba za kuishi, ununuzi wa mashamba (parachichi na nyuki), kusomesha watoto pamoja na kujiunga na Bima ya Afya ya (NHIF).

Bw. Mkinga amesema kwa sasa wanaendelea na kazi ya ujenzi wa daraja mfuto (Vented Drift), kufyeka barabara Km.5, kujenga mitaro mita 5 na kinga maji kwenye mitaro katika barabara ya Mundindi-Ngogoma waliyoanza kujenga Septemba na wanatarajia kuikamilisha mwezi Oktoba mwaka huu.

Naye, Mwenyekiti wa kikundi cha Twili Lupangala Road Works Bw. Gutfred Mbilinyi amesema kwamba walianzisha kikundi hicho baada ya kuhamasishwa wa TARURA  na wameweza kunufaika binafsi na wameweza kuanzisha miradi ya kikundi ikiwemo mashamba, ufugaji pamoja na ununuzi wa bodaboda tatu ambapo Malengo yao ya baadae ni kununua gari la kubeba  mizigo.

Kwa upande Kiongozi wa Ujumbe huo ambaye pia ni Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Matengenezo ya Barabara wa nchi hiyo Bw. Mohamed Kallon amesema wamefurahi kuvitembelea vikundi hivyo na kujionea kazi wanazofanya vikundi hivyo ambapo mapato wanayoyapata yameweza kuwanufaisha kwa kujenga nyumba, kununua bodaboda na kusomesha watoto wao na kwa kikundi cha wanaoishi na VVU amefanya jambo zuri ambalo inawasaidia kupata riziki zao.

Wakati huo huo Mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa TARURA ambaye ni Mkurugenzi wa Barabara Mhandisi Venant Komba amesema ujio wa ugeni huo umekuwa na mafanikio makubwa kwa pande zote mbili.

Amesema Siera Leone wamevutiwa na hatua ya Tanzania kuwa na Taasisi ya kitaaluma inayosimamia shughuli za Barabara za wilaya, mfumo maalumu wa utunzaji wa taarifa za barabara, teknolojia ya mawe, ushirikishwaji wa wananchi wanapofanya usanifu pamoja na namna vikundi vya kijamii vinavyosaidia ujenzi na matengenezo ya miundombinu.

/ Published posts: 1414

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram