42 views 5 mins 0 comments

RAIS SAMIA ACHAMBUA SEKTA YA MADINI

In KITAIFA
October 14, 2024

Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA

-GEITA

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema sekta ya madini nchini inachangia asilimia 56 ya fedha yote ya kigeni inayoingia nchini kila mwaka, na hivyo ni sekta muhimu kwa ukuaji wa uchumi,

Kauli hiyo aliitoa jana mjini Geita, wakati akihutubia wakati akifunga maonesho ya saba ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini mkoani Geita Rais Samia alisema kutokana na mchango huo, Serikali imeweka mkazo wa kipekee kwenye sekta hiyo ili kuhakikisha inaendelea kuwa mhimili wa uchumi na kuongeza mapato kutoka nje ya nchi.

Alisema Serikali imeongeza fedha kwenye sekta ya madini ili kuongeza utafiti kwenye maeneo mengi zaidi, kwani mpaka sasa ni asilimia 16 tu ya eneo lenye madini ndilo limefanyiwa utafiti.

Kutokana na hali hiyo Rais Samia alisema Serikali italeta mitambo zaidi ya kuchimbia madini huku kipaumbele kikiwekwa kwa wachimbaji vijana na wanawake.

Kiongozi huyo wa nchi alisema mwaka 2023, sekta hiyo iliingiza takriban asilimia 56 ya fedha zote za kigeni.

“Sekta hii iliingiza takriban asilimia 56 ya fedha zote za kigeni zilizoingia nchini. Nimefarijika kuona hatua kubwa tunayopiga kama Taifa kwenye uwekezaji katika sekta ya madini ambayo ndiyo kinara kwa kuliingizia Taifa letu fedha za kigeni.

“Ni lazima balozi zetu kutangaza fursa ya uwepo wa mitambo ya kisasa ya kusafisha dhahabu kwa kiwango cha ubora wa asilimia 99.99, pamoja ahueni za kikodi tulizoziweka ili kuvutia zaidi wachimbaji katika nchi jirani kutumia mitambo hii.



“Tutaendelea na kazi ya kuwashika mkono na kuwainua wachimbaji wadogo hasa vijana na wanawake, huku pia tukiimarisha mifumo ya ukusanyaji mapato pamoja na kuzijengea uwezo zaidi taasisi zetu kwenye sekta hii muhimu,” alisema

BoT NA UNUNUZI DHAHABU

Rais Samia Suluhu Hassan alisema Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetenga Shilingi trilioni Moja kwa ajili ya kununua dhahabu kwa wachimbaji wadogo kwenye maeneo mbalimbali nchini.

Rais Samia akifunga maonesho ya saba ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yaliyofanyika mkoani Geita, na kuwataka wachimbaji wadogo kufanya biashara na BoT ili kupata unafuu wa kuuza dhahabu zao.

“Tanzania imedhamiria kuwa na akiba yake ya madini ya dhahabu, hivyo hatua hiyo ya Benki Kuu itawasaidia wachimbaji lakini pia kama Taifa akiba ya dhahabu itaimarisha shilingi,” alisema Rais Samia

Pamoja na hali hiyo aliwapongeza wachimbaji wadogo kwa kuongeza mchango katika pato la Taifa kutoka asilimia tisa mpaka asilimia 40 mwaka 2023.

Rais Samia alisema serikali inatoa uzito mkubwa kwenye sekta hiyo kwa kutambua nafasi yake katika kubadili hali za wananchi hususan wachimbaji wadogo.

DKT BITEKO

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko alimpongeza Rais Samia kwa kuendelea kuwezesha, kuikuza na kuimarisha sekta ya madini nchini.

“Wachimbaji wakubwa na wadogo wamekuwa wanatembea daraja la juu kwa sababu ya fursa ulizotoa kwao. Nataka niwaambie wananchi wa Geita na Watanzania kwa ujumla kuwa Mhe. Rais amekuwa akifanya kila jitihada kwa kuwa anataka mnufaike na raslimali zilizopo nchini,” alisema Dkt. Biteko.

Awali Rais Samia alipata wasaa wa kutembelea Soko la Dhahabu pamoja na kufunga Maonesho ya Saba ya Teknolojia na Uwekezaji kwenye Sekta ya Madini Kitaifa mkoani Geita na baadaye kuzungumza na wananchi.

KAULI YA WACHIMBAJI WADOGO

Wachimbaji wadogo wa madini nchini wameiomba Serikali kuondoa ushuru kwenye vifaa vya uchimbaji wa madni ili waweze kuboresha shughuli zao za uchimbaji.



Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Madini nchini (FEMATA) John Bina ametoa ombi hilo mbele ya Rais Samia Suluhu Hassn, wakati akitoa salamu za shirikisbo hilo kwenye hafla ya kilele cha maonesho ya saba ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini mjini Geita.

Bina alisema ushuru unaotozwa na Serikali kwa wachimbaji wadogo unapunguza uwezo wa wachimbaji hao kufanya shughuli zao, na hivyo kiomba Serikali kuuondoa.

Kuhusu suala la Benki Kuu ya Tanzania kununua asilimia 20 ya dhahabu ya wachimbaji wadogo, Bina amesema wamekubalina na jambo hilo ikiwa ni hatua yao ya kuonyesha uzalendo kwa Taifa lao.

/ Published posts: 1435

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram