28 views 3 mins 0 comments

HUDUMA ZA POSTA ZAZIDI KUIMARIKA KIMATAIFA

In BIASHARA
November 04, 2024



Na MWANDISHI WETU

-DAR ES SALAAM

HUDUMA usafirishaji wa mizigo na vipeto kimataifa kupitia Shirika la Posta Tanzania inaongezeka licha ya kushuka kwa kiasi kikubwa kati ya mwaka 2019 na 2021, kwa mujibu wa uchambuzi wa taarifa ya hali ya mawasiliano kufikia Septemba mwaka huu.

Taarifa ya robo mwaka ya Julai hadi Septemba 2024 iliyotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inaonesha kuwa vitu vilivyosafirishwa na Shirika la Posta Tanzania (TPC) kwenda  nje ya nchi viliongezeka kwa asilimia 74 kati ya mwaka 2021 na 2023.

Ripoti hiyo ya robo ya kwanza inaeleza kuwa vitu 979,625 vilipostiwa kimataifa mwaka 2023 ikilinganishwa na vitu 564,528 mwaka 2021, ambapo kwa mwaka huo ilishuhudiwa kuanza kuongezeka kwa vitu kwenda nje baada ya kupungua miaka iliyotangulia.

“Vitu 2,873,312 vilisafirishwa kimataifa mwaka 2019. Idadi hiyo ilipungua na kufikia 564,528 mwaka 2021. Sekta ya Posta Ulimwenguni pote imekumbwa na changamoto zinazotokana na kuenea kwa kasi kwa teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA).

“Hali hii imewapa watumiaji wa huduma za posta mbadala wa mawasiliano. Aidha, mawasiliano ya kielektroniki yameongeza ufanisi kwenye shughuli za watumiaji. Janga la homa ya mapafu – UVIKO 19 pia limechangia kuzorota kwa huduma za posta. Hii ilitokana na kuvurugika kwa mifumo ya usafirishaji vitu vya posta,” ilieleza ripoti hiyo ya roo ya TCRA

Hata hivyo, watoa huduma wa posta wanatumia TEHAMA kwenye shughuli zao. Wengine wameanzisha huduma mbadala.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, Dkt. Jabiri  Bakari, hivi karibuni alisema kwamba TCRA inahimiza watoa huduma wa posta na vifurushi kutumia teknolojia za kisasa zenye ufanisi.

“Hizi ni pamoja na mifumo ya kidijiti na mifumo inayojiendesha  yenyewe ambayo hurahisisha utendaji na kuboresha upatikanaji wa huduma za  Posta.

“TCRA imetoa leseni 146 kwa watoa huduma za posta na usafirishaji vifurushi. Leseni hizi ziko kwenye makundi sita ambayo pia ni aina ya soko la huduma husika,” alisema Dkt. Bakari

Hata hivyo ripoti hiyo inaonyesha kwamba makundi ya watoa huduma za usafirishaji vifurushi, na idadi ya leseni kwenye mabano, ni Kimataifa (6), Afrika Mashariki (2), ndani ya Tanzania (47), ndani ya mji au jiji (16) na Kati ya miji (74).

“Leseni nyingi za kati ya miji zimetolewa kwa wasafirishaji, yakiwemo mabasi ya abiria.   TCRA inafanya ukaguzi kila robo mwaka kutathmini uzingatiaji wa kanuni za leseni na ubora wa huduma. Vipimo ni pamoja na kuzingatia kasi ya kufikisha vitu vinavyotumwa na wateja.

“Tathmini ya robo mwaka ya Julai-Septemba iliyohusisha watoa huhduma 19 imegundua kuwa watoa huduma saba, au asilimia 37, tu ndio waliofikisha vitu kwa wakati uliowekwa kikanuni,” ilieleza taarifa hiyo

Kampuni zilizozingatia matakwa ya kanuni ni Air Tanzania, Precision Air, Tanz Movers, Advanced Logistics, Delex Courier & Logistics Limited, Ellymo Company Limited na Segax huku kampuni 12 zikishindwa kukidhi mahitaji ya kanuni za ubora wa huduma.

/ Published posts: 1525

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram