34 views 4 mins 0 comments

ZRA YAKUSANYA BILIONI 76 OKTOBA

In BIASHARA
November 04, 2024

Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA

-ZANZIBAR

MAMLAKA ya Mapato Zanzibar (ZRA), imeendelea kutikisa wimbi la Makusanyo kwa kuvuka lengo la ukusanyaji mapato katika kipindi cha Oktoba, mwaka huu  kwa kukusanya jumla ya Shilingi bilioni 76.528 kati ya makisio ya kukusanya Shilingi bilioni 74.549

Akizungumza na waandishi wa habari jana Kaimu Kamishna Mkuu wa ZRA Said Ali Mohamed, kupitia Mkutano na Waandishi wa Habari uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi za ZRA zilizopo Gombani, Chakechake, Pemba.

Katika Mkutano huo, Kamishna Said alisema hatua ya ukusanyaji wa Mapato hayo kwa mwezi Oktoba ni ufanisi wa asilimia 102.65 huku kukiwa na ongezeko la bilioni 15.326 kwa Oktoba katika makusanyo ya mwaka 2024 ambapo ZRA katika Oktoba wa mwaka 2023 ilifanikiwa kukusanya jumla ya Shilingi bilioni 61.202.

Aidha alisema kuwa ufanisi wa makusanyo hayo kwa mwezi Oktoba unatokana na sababu mbalimbali ikiwemo uwekezaji mkubwa katika ujenzi wa miundombinu na huduma za kijamii pamoja na kuimarika kwa shughuli za kiuchumi Zanzibar.

“Hali hii inatokana na utekelezaji wa Sera nzuri za kiuchumi za Serikali ya Awamu ya Nane inayoongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kuimarika kwa shughuli za kiuchumi kati ya Zanzibar na Tanzania Bara na kuimarika kwa uzuwiaji wa kodi  kunakofanywa na mawakala wa uzuwiaji hali inayotokana na utekelezwaji wa Sera na miradi mbalimbali ya kimaendeleo visiwani Zanzibar.

“Sababu nyengine za kufikiwa kwa ufanisi huo ilielezwa kuwa ni kuongezeka kwa idadi ya walipakodi pamoja na ufuatiliaji wa karibu kwa walipakodi wenye lengo la kuwakumbusha wajibu wao wa kulipa kodi kwa hiari,” alisema Kaim Kamishna Said

Alisema sambamba na sababu hizo ni kuimarika kwa miundombinu ya Bandari hususan ya Mkoani Pemba ambayo inapelekea kuimarika kwa shughuli za kiuchumi, kuongezeka uwajibikaji kwa walipakodi katika matumizi ya Mifumo ya Ukusanyaji wa mapato ya ZIDRAS pamoja na Mfumo wa kutolea Risiti za Kielektroniki (VFMS) na Kuongezeka kwa utoaji wa elimu ya kodi kupitia njia mbalimbali.

“Aidha, kuimarika kwa ushirikiano baina ya Wizara na Taasisi nyengine zinazofanya kazi na ZRA ikiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Kamisheni ya Utalii na Taasisi zote za Serikali.

“Mbali na hayo katika kuimarisha ukusanyaji wa mapato kwa mwezi Novemba  2024, ZRA imeahidi kuongeza wigo wa kusajili wafanyabiashara, kuendelea kufanya ziara kwa walipakodi ili kutambua na kutatua changamoto za wafanyabiashara na kuendelea kuimarisha uhusiano mazuri na ushirikiano na walipakodi wote,” alisema

Aliitaja mikakati mingine ni kuimarisha vitengo vya ukaguzi kwa lengo la kuzuia ukwepaji wa kodi, kushirikiana na Jumuiya za Wafanyabiashara katika kushajihisha ulipaji kodi wa hiari, kuendeleza weledi kwa watumishi wa ZRA, na kufanya kampeni mbalimbali zenye lengo la kuhamasisha ulipaji kodi wa hiari.

Kamishna Said aliwashukuru wana habari kwa kazi yao muhimu sana ya kuuhabarisha umma hususan kuhusu masuala ya kodi na kuwataka kutilia mkazo suala la kuwahimiza wananchi kudai risiti za Kielektroniki kila wanapofanya manunuzi.

Ikumbukwe kua hii ni mara ya kwanza kwa Kaimu Kamishna Mkuu wa ZRA kufanya Mkutano na waandishi wa Habari kisiwani Pemba kuhusu taarifa ya Makusanyo ya Mapato kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025.

/ Published posts: 1525

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram