34 views 4 mins 0 comments

BILIONI 11 KUSAMBAZA UMEME KWENYE VITONGOJI SHINYANGA

In KITAIFA
November 07, 2024

Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA

Kunufaisha kaya 2,970 kutoka kwenye vitongoji 90 ndaniya wilaya tatu, RC Macha asema umeme ni kipaumbele cha Rais Samia


-SHINYANGA

SERIKALI kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inatekeleza mradi wa Shilingi bilioni 11.18 wa kusambaza umeme katika vitongoji 90 utakaonufaisha kaya 2,970 mkoani Shinyanga.

Hayo yalisemwa jana na Msimamizi wa Miradi ya REA Kanda ya Magharibi, Mhandisi Robert Dulle wakati akitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha wakati wa kumtambulisha mkandarasi aliyeshinda zabuni ya kutekeleza mradi huo ambayo ni Kampuni ya wazawa ya Derm Group (T) Limited ya jijini Dar es Salaam.

“Tunamshukuru Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kiasi cha Shilingi 11,184,759,397.2 kitumike kusambaza umeme katika vitongoji 90 mkoani hapa, leo (jana) hii tumefika hapa kumtambulisha mkandarasi na tayari maandalizi ya awali ya kutekeleza mradi yameanza,” alisema Mhandisi Dulle.

Akizungumzia kuhusu utekelezaji wa mradi wa kufikisha umeme katika vitongoji mkoani humo, Mhandisi Dulle alisema kati ya vitongoji 2,703 vilivyopo mkoani humo, vitongoji 930 vimefikishiwa umeme na kwamba vitongoji 90 vitakavyopata umeme awamu hii vitaongeza idadi ya vitongoji vitakavyokuwa na umeme Shinyanga.

Alisema mradi unatekelezwa kwa kipindi cha miezi 24 ambapo utekelezwaji wa mradi ulianza Septemba 3, mwaka huu na utakamilika ifikapo Agosti 19, 2026 na kwamba vitongoji vitakavyobaki vitaendelea kusambaziwa umeme kulingana na upatikanaji wa fedha.

Mhandisi Dulle alibainisha kuwa mradi unatekelezwa katika majimbo sita kutoka katika Wilaya za Shinyanga, Kahama na Kishapu na kwamba kila jimbo vitongoji 15 vitanufaika.

“Mradi huu unalenga kupeleka umeme katika majimbo ya Shinyanga, Solwa, Kishapu,  Msalala, Ushetu na Kahama,” alisema Mhandisi Dulle.

Aidha, aliainisha hali ya upatikanaji wa umeme maeneo ya vijijini mkoani humo sambamba na miradi iliyokamilika na inayoendelea kutekelezwa ambapo alisema kati ya vijiji 506 vilivyopo mkoani humo, vijiji 485 vimefikishiwa umeme ambayo ni sawa na asilimia 96.

Aliongeza kuwa vijiji hivyo 21 vilivyobaki vipo wilayani Kahama na kwamba vipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji wa mradi wa REA awamu ya tatu mzunguko wa pili (REA3R2) chini ya Mkandarasi Tontan Project Technology LTD JV Group Six International.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha aliipongeza REA kwa kutekeleza majukumu yake kwa uwazi na kwa utaratibu iliyojiwekea wa kutambulisha wakandarasi kwa viongozi wa Mkoa na Wilaya kote nchini.

“Ujio wenu hapa ni habari njema sana kwa mustakabali mzima wa maendeleo ya Mkoa wetu; pamoja na huduma zingine za jamii huduma ya umeme imepewa kipaumbele kikubwa na Serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, umeme ni injini ya uchumi hili halina ubishi na sasa matumizi ya umeme yameongezeka, mahitaji kwa ajii ya majumbani na pia kiuchumi,” alisema Macha

Aidha, alisema kuwa Mkoa wa Shinyanga unaendelea kukua kwa kasi na kwamba kwa sasa shughuli za kiuchumi zimeongezeka ikiwemo uwepo wa viwanda vidogo na vikubwa ambavyo vyote vinahitaji umeme.

“Hapa Shinyanga mbali na madini pia tunashughulika na kilimo cha mpunga na tungependa kuona mkulima akiongeza thamani ya mazao yake hukohuko unapozalishwa mpunga kwa kukoboa na kupata mchele na hapa faida itaongezeka sambamba na kuandaa ajira na fursa zingine vijijini,” alisema.

Pamoja na hali hiyo alimtaka mkandarasi huyo kuhakikisha anatekeleza mradi kwa ubora na anakamilisha kwa wakati kwani tayari miundombinu ipo hivyo hakuna changamoto yoyote itakayokwamisha utekelezaji wa mradi.

Naye Meneja wa Miradi wa Kampuni ya Derm Group Ltd, Mhandisi Justinus Mutalemwa alimuhakikishia Mkuu wa Mkoa huyo kuwa wamejipanga kikamilifu kutekeleza mradi ambapo alisema wamekamilisha hatua muhimu za awali ikiwemo ukaguzi wa eneo.

/ Published posts: 1525

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram