33 views 4 mins 0 comments

HUDUMA ZA TELEVISHENI KIDIGITALI ZAIDI KUIMARIKA

In BIASHARA
November 11, 2024

Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA

-DAR ES SALAAM

UTANGAZAJI Tanzania umeendelea kuimarika na mawimbi ya televisheni kijitali kwa mfumo wa ardhini (DTT) sasa yanafikia asilimia 58 ya watu, taarifa ya hali ya mawasiliano nchini inaonesha.

Taarifa ya robo mwaka ya Julai hadi Septemba iliyotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inasema mawimbi ya yanafika asilimia 33 yaย  nchi nzima kijiografia, kutoka asilimia 32 Juni mwaka huu.

Mfumo wa DTT ulianza kutumika Tanzania mwaka 2014 baada ya nchi kuanza kutumia mfumo wa utangazaji wa televisheni kidijitali.

Taarifa hiyo, iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Dkt. Jabiri Bakari inasema mfumo wa utangazaji wa setilaiti, unaofupishwa DTH, umeenea kwa asilimia 100 miongoni mwa watu na pia nchi nzima kijiografia.

Mawimbi ya utangazaji wa redio ya FM yameenea kwa asilimia 78 miongoni mwa watu Septemba kulinganisha na asilimiaย  75.52 Juni mwaka huu, ambapo yameenea kijiografia kwa asilimia 56.5 kutoka 49.94 kipindi hicho.

Taarifa inaeleza kuwa TCRA ilitoa leseni mpya 15 za maudhui ya utangazaji kati ya Julai na Septemba. Hizo ni pamoja na moja ya huduma za redio kimkoa, tano za redio kiwilaya na mbili za redio za jamii.

Redio za jamii zinakusudiwa kutoa huduma katika eneo husika au jamii yenye maslahi yanayofanana, mienendo inayofanana na utamaduni unaofanana, zinatakiwa kutoa maudhui yanayolenga na kufaa wanajamii wa jamii husika kwa madhumuni yasiyokuwa ya kibiashara.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa TCRA pia ilitoa leseni tatu za televisheni ya kulipiwa kitaifa robo mwaka ya Julai-Septemba 2024.

Leseni nyingine zilizotolewa ni moja ya redio mtandao, moja ya watayarishaji na wachakataji wa maudhui ya kutolewa mitandaoni na mbili za blogu za habari na matukio yanayotolewa kwenye tovuti.

Hadi Septemba 2024, TCRA ilishatoa leseni za huduma mbalimbali za maudhui na idadi kwenye mabano kama ifuatavyo: redio (246) na televisheni zisizolipiwa (33), televisheni za waya (63).

Nyingine ni leseni za televisheni za kulipia (29), televisheni mtandao (210), redio mtandao (10), blogu za habari na matukio (66) na posta na usafirishaji vifurushi (146).

Taarifa inaonesha kupanda na kushuka kwa idadi ya watu wanaonunua huduma za televisheni kwa waya.

Waliongezeka kutoka 14,350 mwaka 2020 kufikia 19,739 mwaka 2021 na 22,295 mwaka uliofuata, kabla ya kushuka hadi 16,223 mwaka 2023.ย  Taarifa inaelezea kushuka huku kuwa kunatokana na wateja kuhamia mifumo mingine ya utangazaji wa televisheni.

Wateja 18,820 waliunganishwa Juni 2024. Idadi hii iliongezeka kwa asilimia mbili na kufikia 19,153 Septemba mwaka huu.

Huduma za televisheni kwa waya zimeenea zaidi mikoa ya Kanda ya Ziwa. Shinyanga inaongoza, ikiwa na wateja 4,845 waliounganishwa. Tabora ni ya pili na ina 2,118. Mwanza kuna wateja 2,075 na Dar es Salaam 1,169. Mikoa yenye wateja wachache wa huduma za televisheni kwa waya ni Mbeya ambayo ina 64, Manyara (91) na Tanga (230).

Taarifa hiyo ina matokeo ya ufuatiliaji wa ubora wa huduma za mawasiliano. Kwa upande wa utangazaji, watoa huduma wenye leseni za kitaifa wamekidhi masharti kuhusiana na vipindi.

Masharti hayo ni pamoja na kuwa na vipindi vya aina mbalimbali, vipindi vya elimu na kutoa maudhui ya ndani.



Kanuni za maudhui ya redio na televisheni yanataka watoa huduma wahakikishe angalau asilimia 60 yaย  vipindi vyao vina maudhui ya ndani. Maudhui hayo yanatakiwa kuwa na masuala muhimu yanayoitambulisha Tanzania.

Watoa huduma za maudhui wanatakiwa kutumia lugha sanifu na sahihi. Lugha zinazoruhusiwa ni Kiswahili au Kiingereza na sio kuzichanganya.

Hata hivyo, ufuatiliaji huo umebaini kuwa baadhi ya redio na televisheni hazizingatii masharti ya kutenga jumla ya angalau dakika 90 za vipindi vyao kila siku kwa habari.

/ Published posts: 1525

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram