Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA
Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini nchini Tanzania unatarajiwa kuwa jukwaa muhimu la kukuza uwekezaji, kubadilishana maarifa, na kuimarisha ushirikiano katika sekta ya madini.
Mkutano huo ni wasita (6), utakaofanyika kuanzia tarehe 19 hadi 21 Novemba 2024 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC),ambapo Utafunguliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ukienga kuendeleza sekta hiyo inayokua kwa kasi, huku ukileta manufaa ya kiuchumi na kijamii kwa Watanzania na dunia kwa ujumla.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Waziri wa Madini Anthony Mavunde amesema Mkutanao huo utavutia zaidi ya washiriki 1,500 kutoka Tanzania na nchi mbalimbali Duniani.
Mkutano huo utakuwa na mada mbalimbali na watoa mada zaidi ya 50 kutoka ndani na nje ya nchi, wakiwemo mawaziri wa madini kutoka nchi za Afrika, wawakilishi wa kampuni kubwa za madini duniani, na mabalozi wa nchi 31.
Mavunde alisisitiza kuwa mkutano utatoa fursa ya kujifunza kuhusu sera, mikakati mipya ya serikali, na kujadili masuala ya kisheria na kiuchumi yanayohusiana na madini. Huu ni wakati muafaka kwa wawekezaji na wafanyabiashara kujifunza kuhusu fursa zinazozidi kutokea nchini Tanzania, hususan katika viwanda vya uchakataji madini.
Sekta ya madini inachangia kwa kiasi kikubwa uchumi wa Tanzania. Katika Mwaka wa Fedha 2022/23, sekta hiyo ilichangia zaidi ya asilimia 56 ya mapato ya kigeni kupitia mauzo ya bidhaa za madini nje ya nchi, na asilimia 15 ya kodi za ndani zinazotokana na shughuli za madini. Pamoja na mchango huo mkubwa, Serikali ya Tanzania inataka sekta ya madini ichangie asilimia 10 ya Pato la Taifa ifikapo mwaka 2025.
Pia, Mavunde alitangaza hatua nzuri kwa wachimbaji wadogo. Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) linatarajia kuleta mitambo mingine 10 ya uchorongaji madini, na Serikali itabeba sehemu ya gharama za uchorongaji, hivyo kupunguza mzigo kwa wachimbaji wadogo.
Katika mkutano huu pia kutakuwa na hafla ya “Usiku wa Madini” tarehe 20 Novemba, 2024, ambapo tuzo zitatolewa kwa wadau waliofanya vizuri katika sekta ya madini. Hafla hii pia itakuwa na maonesho ya bidhaa za madini, ikiwa ni pamoja na vito vya thamani na madini ya viwandani, ili kuonyesha fursa zilizopo na umuhimu wa madini katika maisha ya kila siku ya Watanzania.
Mkutano huu ni fursa ya kipekee kwa Tanzania kuimarisha sekta ya madini, kuongeza thamani ya rasilimali za madini, na kuvutia uwekezaji wa kimataifa. Serikali inaendelea kutunga sera rafiki kwa wawekezaji na kuhakikisha kuwa sekta ya madini inakuwa chachu ya maendeleo ya uchumi na ustawi wa kijamii.
Kwa ujumla, mkutano huu ni hatua muhimu katika kuhakikisha kuwa Tanzania inafaidika kikamilifu na rasilimali zake za madini, na kuendelea kuwa kivutio cha uwekezaji duniani.
Kaulimbiu ya mwaka huu, “Uongezaji Thamani Madini kwa Maendeleo ya Kiuchumi na Kijamii”, itasisitiza umuhimu wa kuongeza thamani ya madini ili kuleta faida zaidi kwa taifa.
Mkutano huo utahitimishwa siku ya tarehe 21 Novemba 2024 na Rais wa Zanzibar, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi.