23 views 5 mins 0 comments

DKT BITEKO AINADI MARA

In KITAIFA
November 21, 2024

Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA

Asema CCM Inaweza Kazi, Ipewe Kura*

Rais Samia Ang’ara Miradi ya Maendeleo*

Wabunge Waeleza Mafanikio ya CCM Mara*

Wananyamongo Waahidi Ushindi CCM Uchaguzi wa Serikali za Mitaa*

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa ambaye pia ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewataka wananchi wa Nyamongo  na Mkoa wa Mara kwa ujumla kufanya kampeni za kistaarabu na kuwapigia kura  viongozi wa CCM katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaofanyika Novemba  27, 2024.

Dkt. Biteko ameeleza  kuwa maendeleo hayaletwi kwa matusi na kuvunjiana heshima na kuwa wananchi wa Nyamongo waushinde ubaya kwa wema, aidha wamefika  eneo hilo kwa lengo la kuwaomba wananchi wawachague viongozi ambao wataungana na Serikali katika kuwaletea maendeleo.

Dkt. Biteko  ameyasema hayo leo Novemba 20, 2024 wakati akizindua kampeni  za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Mkoa wa Mara zilizofanyika katika Uwanja Nyamongo Wilaya ya Tarime.

“ Mwaka huu tuna Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni uchaguzi mkubwa wa kumchagua mtu atakayejua hali na maisha ya watu katika ngazi ya mtaa na ambaye atabeba shida za watu na kuzitatua,” amesema Dkt. Biteko.

Amebainisha kuwa uchaguzi huo ni muhimu na sio wa majaribio hivyo ni lazima wananchi wachague viongozi ambao sio walalamikaji na kuwa maendeleo yanaletwa  kwa kufanyakazi.

“ CCM tumekuja hapa  kuwaomba kura zenu si tu kwa sababu msimu wa kuomba kura umefika, ila tunaweza kufanya kazi, tumeshaifanya na tunacho cha kuonesha,  mwaka 2020 tulikuja na ilani na kusema tutakayoyafanya na tumeeleza hapa tuliyoyafanya,” amesisitiza Dkt. Biteko.

Amesema kuwa licha ya kufanya siasa ni lazima viongozi wajue wajibu wao ni kuwaletea wananchi maendeleo akitolea mfano namna kijiji kilivyolipwa shilingi bilioni nne ikiwa ni fidia kwa wananchi.

Amefafanua kuwa Rais Samia ana dhamira ya dhati ya kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo na kuwa na maisha nafuu hivyo wananchi wa Nyamongo wamuunge mkono kwa kuchagua wagombea wa CCM.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesema kuwa kuna fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi kwa jamii (CSR) zinazohitaji kibali kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na kuwa amemuelekeza Katibu Mkuu TAMISEMI kuhakikisha zinapatikana ili wananchi wa eneo hilo waweze kunufaika kwa kupata miradi ya maendeleo.

Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mara, Patrick Marwa amesema kuwa Rais Samia ameendelea kuhakikisha mkoa huo unapata fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali hivyo wananchi wachague wagombea wa CCM wa vitongoji na wenyeviti wa Serikali za Mitaa ili kuendeleza jitihada za Rais Samia za kuwaletea maendeleo.

Pia, baadhi ya wabunge wa mkoa huo wamezungumza kwa nyakati tofauti kuhusu miradi ya maendeleo iliyotekelezwa na Serikali inayoongozwa na CCM katika majimbo yao.

Mbunge wa  Jimbo la Butiama na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Jumanne Sagini amesema kuwa hivi karibuni jimbo lake limepata Chuo Kikuu cha Serikali, shule mpya za msingi 12 na shule za sekondari nane huku akihimiza wananchi wa Nyamongo kuchagua wagombea wa CCM katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara, Mhe. Ghati  Chomete amemshukuru Rais Samia kwa kutoa fedha zaidi ya shilingi trilioni moja kwa ajili utekelezaji wa miradi mbalimbali mkoani humo.

Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Mhe. Sospeter Mhongo amesema kuwa awali Mkoa wa Mara haukuwa na maendeleo na kuwa hivi karibuni CCM na Serikali yake imehakikisha uwepo wa maendeleo ikiwemo upatikanaji wa  umeme huku Serikali ikiendelea na utekelezaji wa  mradi wa kufikisha umeme kwenye vitongoji.

Mbunge wa  Jimbo la Tarime Vijijini, Mhe. Mwita Waitara amempongeza Dkt. Biteko kwa jitihada zake za kusaidia mkoa huo huku akitolea mfano juhudi zake za kuhakikisha wananchi wanapata chanzo cha maji kutoka katika mgodi.

Aidha,  ameishukuru  Serikali kwa kutoa fedha kiasi cha shilingi bilioni  36 katika jimbo hilo ambazo zimetumika katika  maeneo mbalimbali ikiwemo ya elimu na afya.

Ameongeza kuwa ujenzi wa barabara ya Nyamongo hadi Mugumu ni muhimu kwa kuwa utasaidia kukuza utalii sambamba na shughuli za  uchumi.

Vilevile katika ufunguzi wa kampeni mkoani Mara,  wagombea wa CCM wamepata fursa za kunadi sera zao kwa wananchi.

/ Published posts: 1525

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram