Na Madina Mohammed DAR ES SALAAM WAMACHINGA
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ametoa wito kwa wakazi wa jiji hilo kujitokeza kwa wingi kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika kesho, Novemba 27, 2024. Akizungumza na vyombo vya habari, Chalamila amesema maandalizi yote yamekamilika, hali ya usalama ni shwari, na vyombo vya usalama vimeimarisha ulinzi ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani na utulivu.
Ameonya kuwa yeyote atakayejaribu kuvuruga amani ya uchaguzi atachukuliwa hatua kali mara moja kwa mujibu wa sheria. “Hakuna atakayeachwa salama. Tunataka kila mtu mwenye nia njema awe na fursa ya kuchagua viongozi wanaowataka bila bughudha,” alisema Chalamila.
Aidha, vituo vya kupigia kura vimeongezwa ili kuwezesha wapiga kura wote kushiriki kwa muda uliopangwa, kuanzia saa 1:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni. Mkoa wa Dar es Salaam, ukiwa na mitaa 564, unatarajia kuchagua viongozi wa serikali za mitaa kwa njia ya kidemokrasia, huku uchaguzi huo ukisisitiza misingi ya “4Rs” ya Rais Samia Suluhu Hassan.