Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA
Chama cha Mapinduzi (CCM) kimewataka Viongozi wa Serikali na Chama tawala kutoa ushirikiano kwa viongozi wa vyama pinzani walioshinda katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, kwani nao wameaminiwa na wananchi.
Akizungumza jijini Dar es salaam Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Taifa, CPA. Amos Makalla amesema uchaguzi umeisha chama kinatoa maagizo viongozi wakaungana na kuchapa kazi hili kuwaletea maendeleo wananchi.
“Kampeni zimeisha, uchaguzi umeshafanyika na washindi wamepatikana hivi sasa sisi ni wamoja hivyo nitoe rai kwa viongozi wa Serikali na chama tawala kutoa ushirikiano kwa viongozi wa vyama vyote bila kubagua kwani viongozi wote waliochaguliwa wametokana na imani ya wananchi katika maeneo yao”. Alisema CPA Makala.
Alisema kufuatia matokeo ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa yaliyotangazwa jana na Waziri, Ofisi ya Rais, Tawara za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mohammed Mchengerwa ambapo chama hicho kimeibuka na ushindi wa kishindo kwa asilimia 99 hii imetokana na maadalizi mazuri yaliofanywa na chama hicho hususani kutumia 4R za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kama nyenzo yake kuu.
Aidha CPA. Makala ametoa wito kwa viongozi wote wa CCM waliochaguliwa kwenda kuwajibika kwa wananchi kwa kusoma taarifa za mapato na matumizi na kutoa huduma bora ili kubeba dhamana na imani waliyopewa na wananchi.
“Chama kimepokea ushindi huu kwa furaha kubwa tumefanya kampeni kwa siku saba kuanzia Novemba 20 hadi 26 na tarehe 27 tukaenda kupiga kura ahadi yetu ilikuwa ni kuongozwa na 4R za Rais Samia”. Alisema CPA. Makala
Alisema ushindi huo ni udhibitisho tosha kuwa sababu zilizoipa ushindi CCM kuwa wananchi wanaimani kubwa na chama hicho na kurizishwa na utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi 2020/2025, hivyo nitumie nafasi hii kutoa rai kwa vyama vya upinzani kujiandaa na uchaguzi ujao badala ya kuendeleza migogoro.