48 views 5 mins 0 comments

MBOWE ATOA KAULI KUNG’ATUKA CHADEMA

In KITAIFA
December 12, 2024

Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA

-DAR ES SALAAM

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amevunja ukimya kuhusu hatima ya kung’atua kwake ndani ya chama hicho huku akiweka wazi kwamba bado yupo sana na hatastaafu siasa kwa sasa.

Kutokana na hali hiyo amesema kuwa amefanyakazi ya kuimarisha upinzani nchini kwa zaidi ya miaka 30 lakini bado hajaona haja ya kukaa pembeni yeye na wenzake ndani ndani ya chama hicho.

Hayo aliyasema jana Jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uamuzi wa Kamati Kuu ya Chadema iliyokutana hivi karibuni.

“Wengine wanalinganisha, wanakuambia hata Nyerere aling’atuka, Nyerere alikuwa mtumishi wa umma, Rais wa nchi analipwa mshahara, analipwa marupurupu, hafungwi, hashtakiwi, hanyang’ang’anywi mali, anatukuzwa, anaishi kwenye nyumba za umma, sisi wa Chadema unaotuona hapa wote hawa wanajitolea.

“Unasema mbowe ondoka, watakaoniambia Mbowe ondoka ni wana-Chadema, hawa watakaoniambia Mbowe gombea ni wanachama hawa, na viongozi wangu hawa yutaelewana mambo yetu ya ndani yanawahusu nini?, mimi nashangaa tu huko mitandaoni pilipili usiyoila inakuwashia nini?,” alisema na kuhoji Mbowe

Kutokana na hali hiyo alisema kuwa bado katiba ya chama hicho ipo wazi na hamzuii mwanachama kugombea nafasi yoyote.

“Katiba yetu ya chama (Chadema) haimzuii mtu yeyote kugombea nafasi, watakaoamua ugombee au usigombee ni viongozi wenzako na wanachama wenzako kwa maelewano, kuna watu wanatamani usiku na mchana waone Chadema tunagombana, tunang’oana meno tunapigana vichwa, hivi nimekaa na Lissu (Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti Chadema Tanzania Bara wanashangaa wamekaa wawili kweli?,” alisema na kuhoji

Akizungumzia kuhusu Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Mbowe alisema kuwa wagombeao wa chama chao ambao walienguliwa upande wa uenyekiti wa Kijiji ni 6,263 kati ya 10,438 ambao ni sawa na asilimia 60.

“Baada ya sarakasi zote za kufunga ofisi, kunyima Wagombea fomu, kuwaengua kwa mizengwe na kuacha kuwateua Chama kilibaki na Wagombea wafuatao, Wagombea wa Uenyekiti wa Mtaa walikuwa 2,686 (63%), Wagombea wa Uenyekiti wa Vijiji walikuwa 4,175 (34%) na Wagombea wa Uenyekiti wa Kitongoji walikuwa 19,805 (31%) ambapo idadi ya jumla ya Wagombea wote wa nafasi za Uenyekiti walikuwa 26,666 (33.2%)”

“Wagombea wa Chadema ambao walienguliwa kwa mizengwe na Wasimamizi wa Uchaguzi ni kama ifuatavyo, Uenyekiti wa Mtaa 1,152 kati ya 3,838 (30%), Uenyekiti wa Kijiji ni 6,263 kati ya 10,438 (60%)

“Uenyekiti wa Kitongoji ni 28,110 kati ya 47,915 (59%) ambapo Jumla ni 35,525 kati ya 62,191 (57%),” alisema

Akizungumzia mvutano unaodaiwa kuwapo kati yake na Makamu Mwenyekiti wake, Tundu Lissu alisema hakuna hali kama hiyo jambo ndani ya familia kuipishana ni jambo la kawaida na si vinginevyo.

“Kuhusu swali kwamba kuna mvutano na Makamu wako (Lissu) anagombea Uenyekiti na kuna Mgombea mwingine na je, nitagombea?, Chama hiki hakijawahi kumnyima mtu yoyote nafasi ya kugombea na anayesema Mbowe unagombea mwenyewe ananionea sijawahi kugombea mwenyewe wala sijawahi kumzuia Mtu kugombea”

“Kuhusu kuwa mimi sijasema nagombea si msubiri muda useme, vitu vingine vinapikwa ndani jamani viacheni vipikwe viive, wengine wanasema Mbowe umekaa sana miaka 20, hivi miaka 20 ya kukomaa, ebu wewe jaribu kukomaa kwa miaka 20 fanya kazi yangu uone ngoma yako itakavyokuwa , wengine wanasema hata Nyerere aling’atuka, Nyerere alikuwa Mtumishi wa Umma.

“…analipwa mshahara, hafungwi, hanyanga’anywi mali, anatukuzwa , anaishi nyumba za Umma, sisi wa Chadema wote hawa wanajitolea, wanasema Mbowe ondoka, watakaoniambia Mbowe ondoka Wanachadema hawa na Viongozi wangu hawa, tutaelewana ugomvi wa ndani yanawahusu nini!?,” alisema na kuhoji

Alisema anashangazwa na taarifa za mitandaoni ambazo zimekuwa zikichambua hali ndani ya chama tofauti na walivyo.

“Mimi nashangaa mitandaoni Watu wapo nje, pilipili usioila yakuwashia nini?, ebu tuachieni Chadema yetu tutaipanga kwa kadri tunavyopenda ndani ya Chadema , kuna watu wanatamani kuona Chadema tunagombana, mtasubiri sana.

“Hii ngoma nimeipiga miaka 33 non stop na sina mpango wa kuacha ngoma hii, yaani hii ngoma napigana nayo, hatutaki biashara ya kustaafu siasa wakati uonevu unaendelea katika Taifa hili, unaniambia nikastaafu tunayoyapigania yametimia?

“Mnawaambia wastaafu kwasababu unaona fulani amechoka yaani mimi Mbowe nimechoka?, muangalieni Rais Mstaafu ana miaka mingapi na Mbowe nina miaka mingapi?,” alihoji Mbowe

/ Published posts: 1636

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram