35 views 5 mins 0 comments

RAIS SAMIA ATOA ONYO KWA WANAOJIPITISHA MAJIMBONI KABLA YA WAKATI

In KITAIFA
January 20, 2025

Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA

-DODOMA

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amewaonya wanachama wa Chama hicho ambao wameanza kupitisha katika Kata na majimbo kufanya kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka 2025 kabla ya wakati.

Akizungumza katika Mkutano Mkuu Maalum wa CCM uliofanyika jana Mjini Dodoma ukiwa na ajenda ya kupitisha jina la Makamu Mwenyekiti  wa Chama hicho Rais Samia alisema Chama kimepata ushahidi unaonesha baadhi ya watu wakiwakusanya wananchi kwa madai ya kuwawezesha kupitia shughuli za kijamii wakati malengo yao ni kujitambulisha kwa wapiga kura.

Rais Dk. Samia alisema katika mwaka huu wa uchaguzi, Chama kimeanza kuchukua hatua mbalimbali huku akieleza kuwa wale ambao wamejipanga kugombea katika uchaguzi mkuu mwaka huu wasubiri wakati ufike na sio kuanza kampeni kabla ya wakati.

“Tayari tumeshapata malalamiko na ushahidi wa picha za watu wanaofanya misafara kwenda majimboni, watu wanaitisha mikutano ya jimbo kwa kigezo cha kujitolea kwa jamii lakini lengo ni kujitambulisha kwa wanachana.Nawaonya walioanza kampeni kabla ya wakati haujafika waache, Chama hakitasita kuchukua hatua dhidi yao.

Akizungumzia makundi ndani ya Chama hicho,Rais Samia alitumia nafasi hiyo kukemea baadhi ya wanachama wenye tabia ya kuendeleza makundi katika uchaguzi mkuu ambapo alifafanua kuna baadhi ya wanachama wamekuwa wakiendeleza makundi ya uchaguzi licha ya Chama kupitisha jina la mgombea.

“Katika Uchaguzi Mkuu mwaka huu wanachama wanawajibika kuendelea kuwa wamoja zaidi katika kukamilisha ushindi wa CCM kwani maendeleo ya nchi yapo mikononi mwa CCM.Nitoe mwito pia  wa kutodharu vyama vya upinzani au kuingia uwoga dhidi ya vyama hivyo…

“Kwani ni lazima CCM kipambane kulinda heshima ya wananchi ambao wameendelea kukiamini kwa miaka mingi.Maendeleo ya nchi yapo mikononi mwa CCM, tusiruhusu kunyemelewa na kiburi cha kuwadharau wapinzani wetu, tusiingie pepo la kuwaogopa tupambane nao ili kulinda heshima ya wananchi.”

Kuhusu ongezeko la idadi ya wanachama Rais Samia alisema Chama hicho kimeendelea kuimarika zaidi kwani hadi Desemba 2024 idadi ya wanachama ilikuwa milioni 12,104,823 kutoka wanachama milioni tatu.

Alisema wanachama hao wametokana na oparesheni maalum zilizofanywa na jumuiya za Chama hicho na watu walikuwa wakisubiri kujiandikisha katika Chama chao.

Akizungumzia utekelezaji shughuli za chama kuanzia mwaka 2022 hadi mwaka 2024 lakini pia na taarifa ya utekelezaji Ilani ya Uchaguzi ya CCM kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ),alisema mkutano mkuu wa CCM uliopita maazimio mbalimbali yalifikiwa ikiwemo kuiagiza serikali kuchukua hatua za kiutendaji kuimarisha utendaji wa Chama na serikali.

Alitaja baadhi ya maagizimio mengine ni kutoa mafunzo kuhusu falsafa ya ujamaa na kujitegemea katika mazingira ya sasa, kuendeleza mageuzi ya kiuchumi kwa kuzingatia sera, demokrasi pamoja na kuimarisha matumizi ya tehama katika utendaji wa shughuli za Chama.

Rais Dk. Samia alisema Chama kimeendesha mafunzo ya kiutendaji nje na ndani ya nchi ambapo kwa upande wa nje ya nchi mafunzo yalitolewa zaidi katika nchi za China na India.”Tumerahisisha shughuli za kiutendaji wa Chama na jumuiya zake kwa kununua vyombo vya usafiri kuanzia kwenye mashina hadi mikoa.

“Magari 194 yamesambazwa katika ofisi 149 za wilaya, magari 33 ofisi za CCM mikoa yote, magari tisa ambapo matatu kila jumuiya za CCM. Shabaha yetu kuhakikisha wilaya ziliobaki zinapata magari mapya kabla ya uchaguzi mkuu.

“Katika ngazi ya kata na wadi za CCM, tumegawa pikipiki nne kwa kila ofisi ambapo hadi Novemba mwaka jana zoezi hilo limefanyika kwa asilimia 100,” alisema Rais Samia.

“Kwa kutambua msingi wa Chama ni watu waliopo ngazi ya chini ambayo lazima tuwafikie.
Hivyo hakuna sababu viongozi wa chama mikoa hadi kata wasiwafikie wapiga kura,”alisisitiza.

Pia alisema Chama kinajipanga kutafuta usafiri kwa ajili ya mabalozi, na imani yake ni kwamba  vyombo hivyo vitaongeza tija katika utekelezaji majukumu ya kazi katika kuendelea kukijenga  Chama.

Wakati agizo lingine ni kukuza matumizi ya tehama katika chama ambapo CCM kinatekeleza mradi maalum kuunganisha mawasiliano kutoka Chama makao makuu hadi ngazi ya wilaya ambao umekamilika na upo katika hatua za majaribio.

Kuhusu ukubwa wa Chama hicho,Rais Samia alisema wananchi hawana mashaka kuhusu CCM kwani ndiyo Chama kikubwa kuliko chochote nchini kimuundo, oganaizesheni, historia na idadi ya wanachama.

“CCM kitaendelea kufanya mageuzi kimfumo, utendaji na uendeshaji hivyo wanachama na viongozi wanapaswa kutimiza wajibu wao kwa kuzingatia uzalendo na kuacha kufanyakazi kwa mazoea.Mwito wangu tuendelee kuhamaisha wananchi kujiandikisha au kurekebisha taarifa zao katika daftari la kudumu la wapigakura.”

/ Published posts: 1715

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram