
Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA
WITO umetolewa kwa wanawake nchini katika kusherekea maadhimisho ya siku ya wanawake duniani,kujenga mazoea ya kutembelea hifadhi mbalimbali zilizopo nchini kwa lengo la kujifunza na kujijengea uzoefu wa kuangalia vivutio mbalimbali.
Wito huo umetolewa jana jijini Dar es Salaam na Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Zone ya Dar es Salaam kutoka Shirika la Uhifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA),Neema Mollel wakati akiongea na waandishi wa habari alisema kwa sasa hifadhi za taifa zipo takribani 21 na ni hifadhi zenye vivutio na uzuri uliotofautiana.
Amesema wamekuwa mstari wa mbele kushawishi wanawake na watoto kutembelea hifadhi hizo ikiwemo nyumba ya Kumbukizi ya Mwl.Nyerere kwa sababu nyumba hiyo kwa TANAPA ni moja ya kitu ambacho wanakithamini kwasababu muasisi wa eneo hili ndio aliyesababisha uwepo wa maeneo mengi ya Asili.
”Tumekuja kutangaza na kuhamasisha wananchi kutembelea nyumba ya kumbukizi ya Mwl.Nyerere na kutembelea hifadhi za taifa za Tanzania ikiwepo Seregeti,Nyerere,Katavi na nyinginezo kwa lengo la kuwajengea wanawake na watoto wa kike fursa mbalimbali.
”Kipindi hiki tunachoenda kuadhimisha siku ya Wanawake duniani ,tunawaasa watoto wa kike kutorudi nyuma kwani katika utalii kuna fursa nyingi ikiwemo kuendesha magari ya utalii,kufungua makambi ya utalii pamoja na Uwekezaji.”amesema
Amesema bado mtoto wa kike ananafasi katika kufanya mambo makubwa pindi anapopewa wajibu wa kupewa kitu anaweza kufanya kwa ufanisi mkubwa.”Tumeona mifano mingi ya viongozi wanawake wapo wanaendelea kufanya kazi kwa jitihada nasi kutoka hifadhi za taifa tupo wanawake wengi ambao ni viongozi lakini tupo tukiendelea kupiga kazi.
”Mwanamke yupo sio kwa kuwezeshwa tu bali kwa taaluma aliyonayo,niwaase watoto wa kike,wanawake na wakinamama msikate tamaa hasa kuongoza watoto wakike kuendelea kujituma na kufanya kazi kwa bidii ili waweze kupata taaluma ambazo ndo zitawasaidia kuingia katika nafasi mbalimbali.”amesema.
Naye Neema Mbwana Afisa Hifadhi Mkuu Malikale,amesema nyumba ya kumbukizi ya Mwl.Nyerere katika kusherekea siku ya wanawake duniani inapenda kuwaenzi wanawake mashujaa walioshirikiana na Hayati Mwl.Nyerere kuifanya taifa la Tanzania kuwa huru.
”Wapo wanawake wengi walishirikiana na Mwl.Nyerere pamoja na Bibi Titi kuhakikisha Tanzania inapata uhuru,hivyo maadhimisho haya yanatukumbusha kusherekea wanawake hao.
”Jamii imekuwa ikiamini kuwa mwanamke anaweza kufanya vizuri jikoni lakini ukija katika kumbukizi ya Mwl.Nyerere anajua kuwa mwanamke anaweza fanya vizuri zaidi hata katika kujenga nchi yake,familia yake,kuilinda nchi na kuelimisha jamii juu ya uzalendo na umuhimu mwingine ambao unaweza kusaidia kwa pamoja kuwa na taifa imara lililobora zaidi,”amesema