

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), leo, Aprili 3, 2025, limesaini mkataba na na kampuni ya Kituruki, M/s Mercan Tekne Deniz Araclari Ltd (Mercan Yachting), kwa lengo la kununua boti mbili (2) za utafutaji na uokoaji (Search and Rescue – SAR) ili kuboresha usalama wa usafiri majini katika mwambao wa bahari na maziwa makuu hapa nchini.
Hafla ya utiaji saini mkataba huo imefanyika katika makao makuu ya TASAC, ambapo Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Bw. Mohamed Salum, na Mwanzilishi Mwenza wa Kampuni ya Mercan Yachting, Bw. Hüseyin Akduman, walisaini mkataba huo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Bw. Salum amesisitiza dhamira ya TASAC ya kuimarisha usalama wa usafiri majini na shughuli za uokoaji katika mwambao wa bahari na maziwa makuu na kufafanua kuwa boti hizo zikikamilika moja itapelekwa katika Ziwa Tanganyika na nyingine katika mwambao wa Bahari ya Hindi.

Bw. Salum alitumia fursa hiyo kuielekeza Kampuni ya Mercan Yachting kutengeneza boti hizo kwa kufuata viwango vya kimataifa.
“Ununuzi wa boti hizi ni muhimu katika kuboresha usalama wa usafiri majini hapa nchini hasa katika shughuli za utafutaji na uokoaji wakati wa matukio ya dharura, hivyo tunategemea ziwe na ubora na viwango vya kimataifa ili ziweze kutumika kwa muda mrefu,” amesema Bw. Salum.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Mauzo kutoka Kampuni ya Mercan Yachting, Bw. Buğrahan Biçer, amesema kuwa kampuni hiyo ina uzoefu wa zaidi ya miaka 38 hivyo wanazingatia ubora katika utengenezaji wa boti zao.

“Tangu tuanze shughuli za utengenezaji boti mwaka 1988 tumeweza kuhudumia nchi 44 kutoka mabara manne (4), hivyo, tunazingatia suala la ubora na usalama wakati wa utengenezaji wa boti zetu,” amesema Bw. Biçer.
Ameongeza kuwa Kampuni ya Mercan Yachting inatengeneza aina mbalimbali za vyombo vya majini, ikiwemo boti za michezo ya maji, boti za abiria, pamoja na boti za uvuvi.

Uwepo wa boti hizi utaisaidia TASAC katika kuboresha usalama wa usafiri majini pamoja na utekelezaji wa sheria na kanuni za usalama majini nchini Tanzania.