66 views 8 mins 0 comments

RAIS SAMIA ATIMIZA NDOTO YA MIAKA 50 YA TAIFA YA KUWA NA UMEME WA UHAKIKA KUTOKA BWAWA LA MWALIMU NYERERE

In MAKALA
April 06, 2025



_Rasmi mashine zote 9 za kuzalisha umeme Megawatts 2,115 zimekamilika, ndoto ya miaka 50 Rais Samia ameitimiza kwa miaka 4 tu kutoka kuukuta mradi ukiwa chini ya 33% hadi kuumaliza 100%._

Na Bwanku M Bwanku.

Moja ya mradi mkubwa wa kimkakati uliokua ukitekelezwa kwenye nchi yetu ni mradi wa kufua umeme kwa kutumia njia ya maji maarufu kama Mradi wa kufua umeme wa Bwawa la Mwalimu Nyerere kwenye Mto Rufiji kule mkoani Pwani (Julius Nyerere Hydroelectric Power Project- JNHPP).

Mradi huu ni wa 4 kwa ukubwa barani Afrika na umegharimu Trilioni 6.5 ukiwa na mashine 9 ambazo zote kwa pamoja zinazalisha Megawatts 2,115.

Kihistoria, mradi huu ulibuniwa na kuasisiwa mwaka 1975 takribani miaka 50 iliyopita na Rais wa Awamu ya kwanza wa Tanzania Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na kuanza kutekelezwa na Serikali ya Awamu ya 5 chini ya Hayati Dkt. John Pombe Magufuli na sasa kukamilishwa kwa haraka na Serikali ya Awamu ya 6 chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Waziri wa Nishati na Naibu Waziri Mkuu Mhe. Dotto Biteko leo Aprili 05, 2025 alitembelea mradi huo na kulitangazia Taifa kwamba rasmi sasa mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere umekamilika rasmi na mashine zote 9 za kuzalisha umeme zimekamilika.

“Tumekuja leo tukiwa na furaha kubwa kwamba mitambo yote tisa imekamilika inazalisha umeme na nina furahi kuwajulisha Watanzania kuwa ile ndoto na shauku ya kuwa na umeme wa uhakika kutoka kwenye chanzo hiki kikubwa barani Afrika imekamilika, kazi iliyobaki ni kuimarisha miundombinu ya kuwafikishia watanzania umeme

“Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Misri kuuzindua rasmi.” Waziri Biteko ameyasema hayo leo April 5, 2025 baada ya kutembelea Mradi huo akiwa ameambatana na Mawaziri ambao ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Hamadi Masauni

Kwa Mujibu wa Wizara ya Nishati, mahitaji ya umeme kwenye nchi yetu hadi sasa ni wastani wa Megawatts 1908.15.

Kwasasa toka tupate Uhuru mwaka 1961, nchi yetu nzima kutoka kwenye vyanzo vyetu vyote vya kuzalisha umeme vya Kinyerezi, Kidatu, Mtera, Nyumba ya Mungu, Songosongo na kwingine, tunazalisha Megawatts wastani 1800 na zisizodi 2,000 lakini bwawa la Mwalimu Nyerere pekee yake linakwenda kutupa megawatts 2,115 za umeme wa uhakika tena wa maji ambao ni wa gharama nafuu zaidi kuliko aina yoyote ile ya umeme duniani ukiachana na umeme wa jua, upepo, nyuklia, makaa ya mawe, mafuta na gesi.

Umeme wa bwawa hili pekee yake unatosha Taifa zima na kwahiyo kwasasa ukichanganya na umeme tunaozalisha kwenye vyanzo vingine nilivyovitaja pale juu maana yake Tanzania rasmi ina utoshelevu wa umeme kwa matumizi yake ya majumbani, viwanda na kwingine na hivyo tuna ziada ya umeme kufikia zaidi ya Megawatts 1,800.

Na sasa kutokana na nchi kuwa na uwezo wa kuzalisha umeme kwa kiwango kikubwa sasa Serikali iko katika mchakato wa kukamilishaย mazungumzo na nchi ya Zambia na Malawi kwa ajili ya kuwauzia umeme ili Taifa lipate mapato yatakayoenda kufanya shughuli zingine za maendeleo na tayari njia ya umeme ya kuunganisha nchi hizo imeanza kujengwa.

Rais Samia anaweka histora ya kuua upungufu na mgao wa umeme kwa Watanzania uliotokana na kuwa na uzalishaji mdogo wa umeme.

Hivi sasa mitambo yote 9 ya kuzalisha umeme imekamilika na inafanya kazi. Kwa mujibu wa Wizara ya Nishati kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wanaosimamia mradi huu, wakati Rais Samia Suluhu Hassan anaingia madarakani Ijumaa Machi 19, 2021, mradi huu ulikuwa umefikia asilimia 33 tu ukiwa umetekelezwa kwa takribani miaka 4 lakini mpaka sasa kwa miaka minne ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan mradi umekamilika wote.

Kwa mujibu wa Waziri wa Nishati na Naibu Waziri Mkuu, Dkt. Dotto Biteko amesema upungufu wa umeme uliokuwepo siku za hivi karibuni hasa mwishoni mwaka 2023 ulikua kati ya Megawatts 300 hadi 400 lakini mitambo yote 9 ya mradi itazalisha Megawatts 2,115 hivyo kuua kabisa upungufu wa umeme nchi hadi kuwa kiwango kikubwa cha ziada ya umeme cha kuuza nje ya nchi.

Miaka minne tu ya uongozi wa Rais Samia umekamilisha ndoto za miaka 50 ya Taifa kuwa na umeme wa uhakika tena wa maji ambao ni nafuu zaidi. Hatua zote muhimu zikikamilika ikiwemo kujaza maji kwenye bwawa hili kubwa sana, kujenga tuta kuu pamoja na hatua muhimu zaidi ya kuwasha Mitambo na kuingiza moja kwa moja umeme kwenye Grid ya Taifa ili kuondoa changamoto ya upungufu wa umeme iliyokuwepo huko nyuma.

Huu ni mradi mkubwa wa kimkakati ambao kukamilika kwake kunalihakikishia Taifa utoshelevu wa umeme na sio utoshelevu pekee yake bali unafuu wa umeme kwani umeme wa maji ndiyo umeme nafuu zaidi kuliko yote duniani.

Umeme unaozalishwa na maji ndio umeme wa gharama nafuu na rahisi zaidi kuliko umeme wowote ule duniani. Uniti 1 ya umeme inayozalishwa na maji ni shilingi 36 tu lakini umeme unaozalishwa na nyuklia Uniti 1 ni shilingi 65, umeme wa upepo shilingi 103.5, wa jua shilingi 103.5, wa makaa ya mawe Uniti 1 shilingi 114, wa joto ardhini 118, umeme wa gesi Uniti 1 shilingi 147 na wa mafuta ndio wa gharama kubwa zaidi ambao wenyewe Uniti 1 gharama yake ni juu sana kati ya shilingi 440 hadi 600.

Hii maana yake ni kwamba kukamilika kwa mradi huu wa Mwalimu Nyerere tutakuwa na Megawatts za umeme zaidi ya 3,000 na moja kwa moja kujihakikishia kama Taifa umeme wa kutosha na kuua hadithi za mgao wa umeme na uhaba wake, utakaolifanya Taifa kupitia wananchi na wawekezaji sasa kufanya shughuli zake za uzalishaji na zingine bila changamoto yoyote ile.

Kuwa na umeme wa uhakika kama huu wa maji tunaozalisha pale Rufiji, tayali unavutia viwanda na shughuli nyingi za kiuchumi ikiwemo wawekezaji wengi zaidi kuja kujenga viwanda hapahapa. Mwekezaji yeyote anayefikiri kwenda kuwekeza sehemu yoyote ile duniani lazima awe na uhakika wa nishati kwasababu kiwanda ni nishati.

Chini ya Serikali ya Rais Samia hakuna kinachosimama wala kukwama.

Kukamilika kwa mradi huu mkubwa kabisa wa kufua umeme unaleta ukombozi mkubwa sana wa kiuchumi hasa wakati huu nchi yetu ikiwa kwenye ujenzi wa uchumi wa viwanda, shindani na wenye kuleta maisha bora kwa watu ambao kwa kiwango kikubwa unategemea sana nishati ya umeme ya kuwezesha viwanda kupata nishati ya kutosha ili iweze kuzalisha vya kutosha na muhimu zaidi kwa gharama nafuu.

Unapokuwa na umeme wa uhakika, lakini sio wa uhakika tu tena na wa gharama nafuu ya bei kama huu wa maji tunaozalisha Rufiji, tayali unavutia wawekezaji wengi zaidi kuja kujenga viwanda hapahapa. Suala la uhakika wa umeme na nafuu yake ni mambo ya msingi sana na ya kwanza kabisa kwa mwekezaji yeyote anayefikiri kwenda kuwekeza sehemu yoyote ile duniani kwasababu kiwanda ni nishati.

MAKALA HII IMEANDALIWA NA KUANDIKWA NA BWANKU MUSA BWANKU AMBAYE NI AFISA TARAFA WA TARAFA YA KATERERO ILIYOPO BUKOBA MKOANI KAGERA. ANAPATIKANA KWA EMAIL bwanku55@gmail.com

/ Published posts: 2099

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram