64 views 10 mins 0 comments

DKT. SAMIA ANAANDIKA HISTORIA RAIS ANAYEWAJALI ZAIDI WAFANYAKAZI. AWEKA REKODI NYONGEZA 35.1% NA 23.3% HAIJAWAHI KUTOKEA.

In KITAIFA
May 05, 2025



_Atatua kero za Wafanyakazi zilizowatesa sana, apandisha madaraja na vyeo 90%, apunguza kodi ya mshahara, aajiri baada ya muda mrefu, apandisha kikokotoo kutoka 33% hadi 40% n.k_

Na Bwanku M Bwanku.

Kila ifikapo Mei Mosi kila mwaka, Dunia huadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani. Ulimwengu hutumia siku hii kujadili masuala mbalimbali yanayowahusu Wafanyakazi ikiwemo matarajio kwao, changamoto zao na namna ya kuboresha masuala mbalimbali yanayogusa maeneo wanayofanyia kazi ili kuchochea ufanisi zaidi.

Na mwaka huu 2025, maadhimisho haya ya Siku ya Wafanyakazi (Mei Mosi) Kitaifa yamefanyika mkoani Singida kwenye uwanja wa Bombadia ambako Rais Samia Suluhu Hassan alikuwa Mgeni rasmi, akizungumza kwenye maadhimisho hayo na kupata nafasi ya kutolea ufafanuzi wa masuala mbalimbali yanayowahusu Wafanyakazi kwa kujibu kero zao mbalimbali ikiwemo kubwa na iliyosubiliwa kwa hamu na Wafanyakazi wote nchini, ya kuongeza mishahara.

Kwenye sherehe hiyo, Rais Samia kupitia Serikali anayoiongoza ametangaza jambo lililokua linasubiliwa kwa hamu na Wafanyakazi nalo ni Serikali imetangaza kupandisha kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa umma kwa 35.1%. Hii maana yake mtu aliyekua anapokea mshahara wa Tshs 370,000 na sasa atapokea Tshs 500,000.

Hiyo ni pamoja na kuwaeleza Wafanyakazi kwamba nyongeza nzuri ya mishahara ikiwemo kuzidi kuboresha maslahi yao jinsi bajeti na ukuaji wa uchumi unavyoruhusu. Ongezeko kubwa la mshahara ambalo haijawahi kushuhudiwa toka Tanzania ianze.

Huu ni mfululizo wa Serikali ya Rais Samia kuvunja rekodi ya kuboresha maslahi ya Wafanyakazi. Mwaka 2022 baada ya kupita takribani miaka 7, Serikali ya Rais Samia ilikata kiu ya Wafanyakazi wa Tanzania kwa kukubali kuongeza mishahara kwa asilimia 23.3.

Miaka 4 ya Rais Samia kunazidi kufungua ukurasa wa maboresho makubwa ya maslahi ya Wafanyakazi na ushughulikiaji wa changamoto zao zilizokua zinalalamikiwa sana. Kwa muda mfupi anazitatua huku kila mwaka akilipua shangwe na ndelemo ndani ya nchi kwa mambo makubwa. Alianza kwa kupandisha 23.3% mwaka 2022 na sasa amevunja rekodi hadi kufikisha 35.1% ikiwa ni ongezeko la zaidi ya trilioni 1.59.

Hatua hii inaweka rekodi pia ya Tanzania kufanya ongezeko kubwa la mishahara ukanda mzima wa Afrika na mataifa majirani zetu. Mataifa mengi majirani hayajaongezea mishahara watumishi wake. Mfano Kenya hawajaongeza na badala yake watatumia nyongeza ya mshahara ya mwaka jana ambayo ni 6%, Uganda hawakuongeza na mataifa mengine mengi.

Lakini nyongeza ya mshahara ni changamoto moja ndani ya changamoto nyingi zinazowakumba Wafanyakazi. Ni ukweli ulio wazi kwamba, changamoto za Wafanyakazi ni zaidi ya kuongezewa mishahara. Kuongeza mishahara ya Wafanyakazi bila ya kutatua changamoto zingine mbalimbali kwenye mishahara yao na mifumo ya utumishi basi nyongeza ya mshahara ni kazi bure.

Ili kumsaidia mfanyakazi, suala la kuongeza mishahara pekee yake halitoshi bila ya kuangalia na kutatua kero zinazosemwa kila kukicha zinazodhoofisha pato ghafi la mshahara wa mtumishi.

Toka iingie madarakani, Serikali ya Rais Samia imetupia jicho kuongeza mishahara lakini kubwa na la msingi zaidi ni kutatua kero nyingi za Wafanyakazi ambazo zimekuwa zikila na kupunguza kwa kiwango kikubwa mishahara yao ikiwemo kodi kubwa kwenye mishahara, tozo ya mkopo wa Serikali kwa Wafanyakazi wenye madeni ya mkopo wa elimu ya Juu, malimbikizo ya mishahara na kuajiri Wafanyakazi wapya ili kupunguza mzigo mkubwa kwa Wafanyakazi na changamoto nyingine nyingi.

Kwahiyo, Serikali ya Rais Samia si tu imefanya makubwa ya nyongeza kubwa ya mishahara iliyovunja rekodi kwa 23.3% na 35.1% lakini zaidi Serikali yake imeweka nguvu kubwa kutatua kero za Wafanyakazi zinazofanya vipato na mishahara yao kuliwa sana.

Kwa Mujibu wa Serikali kupitia Wizara inayoshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu chini ya Waziri wake Mhe. Ridhiwani Kikwete tayali Serikali ya Rais Samia imeshusha kodi kwenye mishahara ya watumishi kwa 1% yaani (PAYE)-pay as you earn kutoka 9% hadi 8% na hivyo kuongeza moja kwa moja mshahara wa mtumishi ambapo fedha inayokatwa kwenye mshahara wa mtumishi imepungua.

Eneo hili la PAYE pekee, serikali inasamehe kiasi cha Bilioni 14 na Milioni 178 kwa mwaka zilizokuwa zinakatwa kwenye mishahara ya Wafanyakazi. Moja kwa moja hapa mshahara wa mtumishi uliimarika.

Ni ndani ya kipindi hiki cha Serikali ya Rais Samia ametatua kero kubwa na ya miaka kwa miaka ya kulipa malimbikizo ya mishahara ya watumishi yenye thamani ya Bilioni 60 na kufanya mabadiliko ya Utumishi yaliyogharimu takribani Bilioni 120. Hapa Serikali ililipa malimbikizo ya mishahara kwa Wafanyakazi 75,000 ambapo Serikali ilitumia zaidi Bilioni 124.3

Amefuta ada ya riba ya Retention Fee ya asilimia 6 Kwa watumishi wote wenye mikopo ya Elimu ya Juu pamoja na tozo ya adhabu ya asilimia 10 ambayo walikuwa wanakatwa Wafanyakazi wenye Mikopo ya Bodi ya Mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu Kwa mwaka. Ambao walichelewa kulipa na ambao bado hawajamaliza mikopo hiyo walikua wanatozwa riba hiyo jambo lililokua linaongeza maradufu deni hilo, makato hayo yameondolewa na kufanya mshahara wa Mfanyakazi uendelee kuimarika.

Hapa Serikali ilisamehe madeni yaliyofikia Trilioni 1 na Bilioni 168 kwa kufuta tozo hizi na tozo za adhabu ambazo nazo zimebaki kwenye mshahara wa Mtumishi.

Kufungua upandishaji wa madaraja na vyeo baada ya kifungo kikali kwa watumishi kutopanda vyeo na madaraja kwa muda mrefu sana. Hadi sasa chini ya Rais Samia zaidi ya 90% watumishi wamepanda madaraja kwa mseleleko bila ubaguzi baada ya wengi kukaa muda mrefu bila kupanda. Bajeti hii inayokuja bado kuna kundi kubwa lingine la Wafanyakazi wanakwenda kupandishwa vyeo.

Kutoa ajira zaidi ya 40,000 ikiwemo ajira kwenye sekta ya afya, elimu, kwenye vyombo vya ulinzi na usalama, TAKUKURU, TRA, Shirika la Reli pamoja na ajira zingine 32,000 zilizotolewa kwa mkupuo kwa walimu na watu wa afya. Kutoa ajira mpya kunawapunguzia majukumu watumishi na hivyo kuboresha hali zao.

Ukipita kwenye mfumo wa Ajira wa Serikali kwasasa (Ajira Portal) unakuta ajira mpya na kila kukicha tumeendelea kushuhudiwa ajira mpya zikitangazwa kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa, serikalini na kila mahali baada ya miaka zaidi ya 6 ya kutoajiri.

Pia, Serikali ilipandisha vyeo na madaraja watumishi 85,000 hadi 91,000 mpaka 198,215. Hatua hizi zote za kutoa ajira mpya na kupandisha vyeo na madaraja ni neema tupu maana ilipunguza mzigo mkubwa sana kwa Wafanyakazi.

Unaweza kuona, licha ya nyongeza hii kubwa ya mishahara lakini Serikali ya Rais Samia imefanya makubwa zaidi kutatua changamoto za Wafanyakazi zilizokuwa zinakula sana mishahara yao.

Ongezeko hili la mishahara na utatuzi wa kero za wafanyakazi ni neema nyingine kwa ukuaji wa uchumi wetu na linakwenda kuchochea shughuli za biashara na mzunguko wa fedha nchi nzima maana litaongeza ununuzi, mzunguko wa fedha mtaani na hivyo kuchochea maendeleo ya watu na shughuli zote za uchumi. Historia inaandikwa Tanzania chini ya Rais Samia na kwa kufuru hii, si dhambi kunena kwa madaha kabisa kwamba, Rais Samia ni Kinara wa maslahi ya Watumishi.

Eneo la mafao kwa mtumishi anayestaafu kwa maana kikokotoo ni eneo lililozua mjadala mkubwa sana na kutesa watumishi wengi. Mijadala imekua mingi sana eneo hili, Serikali ya Rais Samia imeliona na kupandisha mafao ya mkupuo kwa watumishi wanaostaafu kutoka 33% ya mwanzo hadi kufikisha 40% huku akipandisha pensheni anayopokea mstaafu kutoka Tshs 100,000 hadi Tshs 150,000 kwa mwezi.

Kuboresha mazingira ya maeneo ya kufanyia kazi kwa watumishi ili kulinda usalama wao. Rais Samia amedhihirisha nia ya kuwakinga Wafanyakazi wafanye kazi kwa usalama na hapa ameiwezesha Wakala wa Usalama na Afya Mahali Pa Kazi (OSHA) na Kamishna wa kazi kuwa na vifaa vya kisasa na Wataalamu ili tu kukagua maeneo ya kazi kuhakikisha yanakua salama na Wafanyakazi hawadhuriki wanapohudumia wananchi.

Pia, hatua ya kuongeza umri wa utegemezi kwa watoto wa watumishi kutoka miaka 18 hadi 21. Hili lilikuwa jibu la changamoto za wafanyakazi kwa wote wanaowategemea, kwa kuongeza miaka ya kumtegemea mfanyakazi ambapo miaka mitatu si haba kwani iliongeza miaka ya kupunguza utegemezi na kumuepusha mfanyakazi kutumia kipato chake (mshahara) kumhudumia au kuwahudumia wategemezi wake.

Kwa kuongeza umri wa utegemezi wa mtoto serikali imesamehe kukusanya zaidi ya Bilioni 3.5 baada ya watoto 65, 353 kusajiliwa na kipato hiki chote kinabaki kwa wafanyakazi.

Mambo haya yote niliyoyataja pale juu na mengine mengi ambayo sikuyataja yalivyoshughulikiwa imefanya pato la mshahara (NET Salary) liongezeke automatically.

MAKALA HII IMEANDALIWA NA KUANDIKWA NA BWANKU MUSA BWANKU AMBAYE NI AFISA TARAFA WA TARAFA YA KATERERO ILIYOPO BUKOBA MKOANI KAGERA.

/ Published posts: 2097

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram