8 views 2 mins 0 comments

WAZIRI MAVUNDE KUZINDUA CHAMA CHA WASAMBAZAJI WA SEKTA YA MADINI TANZANIA (TAMISA) JIJINI DAR ES SALAAM

In BIASHARA
May 14, 2025

Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA

Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde anatarajiwa kuzindua Kamati ya Chama cha Wasambazaji wa Sekta ya Madini Tanzania (TAMISA), uzinduzi ambao utaambatana na kufanyika kwa Kongamano la Kuwaunganisha Watanzania waliopo katika sekta ya madini.



Hayo yameelezwa leo Jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Kamati ya TAMISA, Masoko na Mawasiliano, Dk. Sebastian Ndege katika mkutano na waandishi wa habari uliohudhuriwa pia na Mwenyekiti wa TAMISA Bw. Peter Kumalilwa.



Amesema kwamba uzinduzi huo utafanyika 16/5/2025 Jijini Dar es Salaam utakuwa na matukio mawili, la kwanza ni kuzindua Kamati ya TAMISA na tukio la pili litakuwa ni Kongamano ambalo litazungumzia nafasi ya Watanzania katika utoaji huduma kwenye sekta ya madini.

“Tunafahamu sisi Watanzania madini ni ya kwetu, na tunafahamu ya kuwa tunakila sababu ya kushiriki katika uchumi wa madini na Serikali yetu pamoja na Waziri wetu Mhe. Mavunde amekuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha ushiriki wa Watanzania katika sekta hii,” alisema Dkt. Ndege.

Kwa upande wake Mwenyekiti TAMISA Bw. Kumalilwa amesema Waziri Mavunde amekuwa akiongelea kuwa katika sekta hii ya madini kuna kiasi cha shilingi trilioni 3.1 ambayo inatumika kila mwaka katika manunuzi ambayo angependa Watanzania wanufaike nayo.



“Kuna migodi mikubwa nchini kama mitano, ambayo wao kila mwaka wanafanya manunuzi ya shilingi trilioni 3.1, ambapo sisi Watanzania tunanufaika kwa karibu asilimia 10 tu, kiasi hiki ni kidogo sana,” amesema Bw. Kumalilwa.



Amesema kwa kutambua hilo TAMISA imeweka mikakati ya kuhakikisha Watanzania zaidi wanaanzisha viwanda vya madini na kushiriki kikamilifu katika sekta hiyo ili kuweza kunufaika japo na asilimia 30 ya kiasi cha hicho shilingi trilioni 3.1 za manunuzi ya sekta ya madini.



“Kwa sasa hivi sisi Tanzania tunasheria ya local content, kwa wakati wangu kama Mkwenyekiti wa TAMISA nitahakikisha Watanzania wananufaika na shilingi trilioni 3.1 za manunuzi japo kwa asilimia 20 hadi 30,” alisema Bw. Kumalilwa na kuongeza,

“Tumekuwa tukilalamika sana kuhusu Wachina wanakuja nchini wanachukua kazi zetu, sasa sisi kama TAMISA tumekuwa tukihakikisha kwamba tunawajengea uwezo Watanzania ili waweze kushiriki katika uchumi wa sekta ya madini nchini,” alisema Bw. Kumalilwa.



TAMISA iliyozinduliwa Septemba 15, 2024 na Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, inamalengo makuu ya kutetea wasambazaji wa sekta ya madini, kuboresha uwezeshaji wa biashara, kutetea haki za wasambazaji na kuendeleza utafiti na ukuaji wa teknolojia.

/ Published posts: 2048

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram