8 views 17 mins 0 comments

ZITO KABWE AANIKA MADUDU YA MMILIKI WA KAMPUNI YA IPTL,”NITAENDA KUTOA USHAHIDI WOTE MAHAKAMANI”

In KITAIFA
May 18, 2025
Kiongozi Mstaafu wa chama Cha Act WAZALENDO zitto kabwe Akiongea mbele ya waandishi wa habari Leo jijini dar es salaam

Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA

KIONGOZI Mstaafu wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, amesema Mfanyabiashara na Mmiliki wa Kampuni ya Ufuaji Umeme ya IPTL, Harbinder Seth amemfungulia kesi Mahakamani akidai kuwa amemkashifu na kumvunjia heshima mbele ya Jamii.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 18, 2024 jijini Dar es Salaam, Zitto amesema kuwa sababu ya kufunguliwa kesi hiyo ni kutokana na kuzungumzia sakata la IPTL kupitia ukurasa wake wa X (zamani Twitter).

Kwamba Seth amemtaka Zitto amlipe mabilioni ya fedha ambapo hata hivyo Zitto amesema haogopi kwani alichoandika ni kweli na yupo tayari kwenda Mahakamani kueleza ukweli huo.

“Nipo tayari kwa kesi, nitaweka ukweli wote wazi na mwisho kufukia kabisa huu mzoga unaoitwa Sakata la IPTL. Tuhuma hizo za bwana Seth kwanza si za kweli, kwasababu sijamkashifu na wala kumshushia heshima, lakini ninampongeza sana (Seth) na kumshukuru kwa ujasiri wake wa kunishitaki kwasababu kesi hii itatoa fursa ya kumaliza jambo hili linaloweka wingu kwa muda mrefu sana katika taifa letu,” amesema Zitto.

Hata hivyo Zitto amesema kuwa hakatai kusema maneno hayo ambayo ananituhumu kusema amemkashifu, kwamba maneno aliyosema na yakachapishwa kupitia akaunti yake ya mtandao wa X ni ya kweli na yanaakisi picha halisi na yenye ukweli wa jambo hilo.

“Pili ni maneno niliyoongea kwa nia njema kabisa ya kutaka kupata ufumbuzi wa sakata hili. Tatu maneno yale nimeyasema kwa vile mimi nilibahatika kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya PAC iliyoshughulikia sakata la IPTL maarufu kama Sakata la Escrow. Hivyo nilitumia “priviledge” hiyo kuwaeleza Watanzania wenzangu ukweli wa jambo hili,” ameeleza Zitto na kusisitiza,

“Narudia kusema ni kweli maneno yale ni yangu, na niliyasema kwa nia njema kabisa kwani kwa nafasi yangu kama kiongozi hili nilipata nafasi ya kujua ukweli wa jambo hili na hivyo nina dhima ya kusimamia ukweli ili kulilinda Taifa letu dhidi ya njama zozote zile za kupora rasilimali za Watanzania kwa kisingizio cha uwekezaji. Sasa nitakwenda Mahakamani kujibu Madai dhidi yangu, na kuitumia kama fursa hiyo adhimu kuelezea ukweli wa kadhia hii na kwamba,”.

TAARIFA YA NDUGU ZITTO ZUBERI KABWE KWA WANANCHI KUPITIA VYOMBO VYA HABARI

PROTEA COURTYARD HOTEL TAREHE 18/05/2025

Ndugu, Wahariri na Waandishi wa Habari,

Habari za mchana!
Ndugu zangu, nimewaiteni hapa leo, kuzungumza nanyi na kwa kupitia nyinyi kuzungumza na watanzania wenzangu. Mimi ndugu yenu nimeshitakiwa Mahakamani na Bwana Harbinder Singh Sethi, kuwa nimemkashifu na kumshushia heshima mbele ya jamii kwa vile eti nimezungumzia sakata la IPTL. Amenishitaki na ameomba Mahakama mbali na mambo mengine nimlipe mabilioni ya fedha.

Tuhuma hizo za Bw. Sethi si za kweli na kwamba sijamkashifu wala kumshushia heshima kama anavyodai. Nampongeza sana na kumshukuru Bw. Sethi kwa ujasiri wake wa kunishtaki kwa sababu Kesi hii itatota fursa ya kulimaliza jambo hili linaloweka wingu kwa muda mrefu. Lakini pia litanipa nafasi ya kuweka ukweli wote wazi na mwisho kufukia kabisa mzoga huu unaoitwa sakata la IPTL.

Ndugu Wahariri, Waandishi na Wananchi,

Binafsi, sikatai kusema maneno hayo ambayo ananituhumu kusema nimemkashifu, maneno niliyosema na yakachapishwa kupitia akaunti yangu ya mtandao wa X ni ya kweli na yanaakisi picha halisi na ya yenye ukweli wa jambo hili. Pili ni maneno niliyoongea kwa nia njema kabisa ya kutaka kupata ufumbuzi wa sakata hili. Tatu maneno yale nimeyasema kwa vile mimi nilibahatika kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya PAC iliyoshughulikia sakata la IPTL maarufu kama Sakata la Escrow. Hivyo nilitumia “priviledge” hiyo kuwaeleza Watanzania wenzangu ukweli wa jambo hili. Narudia kusema ni kweli maneno yale ni yangu, na niliyasema kwa nia njema kabisa kwani kwa nafasi yangu kama kiongozi hili nilipata nafasi ya kujua ukweli wa jambo hili na hivyo nina dhima ya kusimamia ukweli ili kulilinda Taifa letu dhidi ya njama zozote zile za kupora rasilimali za Watanzania kwa kisingizio cha uwekezaji.

Sasa nitakwenda Mahakamani kujibu Madai dhidi yangu, na kuitumia kama fursa hiyo adhimu kuelezea ukweli wa kadhia hii na kwamba;

Taarifa zote nilizochapisha katika ukurasa wangu wa X ni sahihi na ni tafsiri ya kesi mbalimbali zilizoamuliwa na Mahakama Kuu, Mahakama ya Rufani, pamoja na Mahakama na Mabaraza ya Kimataifa juu ya Umiliki na Uhalali wa Umiliki wa IPTL.

Kutoka kuanzishwa kwake mwaka 1995, IPTL ilikuwa na wanahisa wawili na ambao ni Mechmar yenye hisa 7 na VIP Engineering yenye hisa 3. Mara tu baada ya Kuanzishwa VIP ilikwenda Mahakamani na kutaka kui liquidate IPTL kutokana na Mgogoro wa wana hisa Pamoja na mambo mengine kuhusu gharama za uwekezaji. Baada ya vita ya muda mrefu VIP ililiondoa shauri hilo Mahakamani kutokana na makubaliano na PAP baada ya kujitambulisha kwa VIP kwamba ilikwisha nunua hisa za Mechmar na hivyo kuifanya PAP kuwa na hisa zote 10 za IPTL.

Mahakama Kuu kupitia kwa Jaji Utamwa wakati huo, ilikubali ombi hilo na hivyo kuipatia PAP uendeshaji wa masuala yote ya IPTL ikiwemo fedha za Escrow. PAP ikaitumia Amri hiyo ya Mahakama kujisajili BRELA na pia ikaweza kugawa hisa za ziada kwa makampuni mawili ya Hi-tide Trade na Eurasia Holdings Limited, zote zikigawiwa hisa moja moja. Na hapo ndipo Bw. Sethi akawa Mwenyekiti wa Bodi (Executive Chairman) na Mkurugenzi Pamoja Wakurugenzi wenza ambao ni Manraj Singh Bharya Pamoja na Magesh Varan Subramanyan. Kwa kifupi sana hivi ndivyo Sethi alivyoingia IPTL.

Kampuni ya Sethi, PAP haikuwahi kununua hisa 7 za Machmar zilizokuwa IPTL. Badala yake Sethi anadai kununua hisa hizo 7 za Mechmar kupitia kampuni ya Piperlink ya huko British Virgin Island. Madai haya yanapingwa vikali na benki ya Standard Chartered Bank Hong Kong (SCBHK), ambayo inadai kuwa yenyewe ndio wamiliki wa hisa 7 za Mechmar.

Benki hii ndio mrithi wa hisa za Mechmar katika IPTL kwani ndio warithi kutoka kwa Wakopeshaji wa IPTL kutoka Malysia. Hivyo, maswali kadhaa yanajitokeza ikiwemo, Iweje Bw. Sethi kupitia IPTL anunue hisa kwa kampuni ya Piperlink wakati kampuni hiyo haina umiliki wa hisa hizo? Iweje umiliki wa hisa uhame kutoka kwa mtu asiye na hisa? Ni wazi kuwa huu ulikuwa ni mpango uliojaa ghilba na utapeli wa wazi.

PAP, kampuni iliyopata hisa za IPTL katika Mchezo huo wa kitapeli ndiyo iliyolipwa fedha za Escrow na Benki Kuu ya Tanzania na baadae kutumia kiasi cha pesa hizo kununua hisa za VIP, kwani ni fedha hizo hizo ndizo zilizotumika kuilipa VIP Engineering dola za Kimarekani Milioni 75. PAP hakuwekeza chochote katika ununuzi wa hisa hizo toka IPTL. Haikulipa shilingi 1 kununua hisa 7 za Mechmar bali ni ujanja ujanja, utapeli na ghilba ndivyo vilivyotumika na Bw.Sethi pamoja na PAP kuhalalisha uchotwaji wa fedha za Escrow na kutumia fedha hizo kujihalalishia utapeli wa kinachoitwa ununuzi wa Hisa.

Benki ya SCBHK ilifungua kesi mbalimbali kupinga umiliki huo dhidi ya IPTL, Tanesco na Serikali ya Tanzania ambapo walidai na kushinda tuzo ya dola za kimarekani milioni 185.

Sakata la Umiliki wa PAP katika IPTL uliendelea kupingwa mpaka Mwaka 2021 ambapo Mahakama ya Rufani ya Tanzania ilimaliza jambo hili kwa kufuta amri zote za Jaji Utamwa na amri nyingine zote na vitendo vilivofuata. Hivyo basi PAP haina uhalali wowote wa Kisheria wa kuwa ni mwanahisa wa IPTL.

Ndugu Wahariri, Waandishi na Wananchi,

Haya niliyoyasema hapa yanathibitishwa na Maamuzi mbalimbali ya kesi zilizofunguliwa dhidi ya Bwana Sethi, IPTL na PAP. Msingi mkuu ni kuwa Bw. Sethi na PAP sio wamiliki halali wa hisa katika IPTL. Kwani hakukuwa na hisa zilizohama kutoka Mechmar kwenda PAP. Kesi hizi zote zilizofunguliwa msingi wa madai yake ulikuwa ni huo. Nitazitaja kesi hizo kwa kumbukumbu zenu;

SCBHK VS IPTL/PAP, London High Court (IPTL iliamriwa kulipa kiasi cha dola za kimarekani Milioni $148m) kwa Benki ya SCBHK. Uamuzi huo haujapingwa na IPTL ya Bw. Sethi lakini vile vile bado haujatekelezwa na IPTL.

SCBHK VS Tanesco- Tanesco iliamuriwa kuilipa Benki hiyo dola milioni 168.

SCBHK VS Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania (GoT). Serikali iliamriwa ilipe dola za kimarekani milioni 185.

Kupitia Mwanasheria Mkuu na Katibu Mkuu Nishati VS Habinder Kesi Namba (90 ya Mwaka 2018). Katika kesi hii Bwana Sethi aliingia makubaliano na kusaini Hati ya Makubaliano na Serikali ili kuifidia Serikali dhidi ya Hasara iliyoipata au itakayoiingia kwa Maamuzi namba 2 na 3 niliyoyaorodhesha hapo juu na kwa kuwa wakati wa uchotwaji wa fedha hizo za escrow kulikofanywa na Bw. Sethi na PAP Bw. Sethi aliweka Saini Hati ya Fidia (Deed of Indemnity) dhidi ya hasara yeyote ile itakayotokana na uchotwaji wa fedha hizo kama kinga kwa Serikali.

Decree ya Mahakama katika kesi hiyo iliweka wazi kuwa Bw. Sethi hana na hatakuwa na Madai yeyote dhidi ya Serikali badala yake anawajibika yeye Pamoja na PAP kuifidia Serikali kutokana na Kinga iliyowekwa kupitia Deed of Indemnity hiyo. Bw. Sethi na PAP hawajatekeleza Maamuzi hayo ya Consent Decree mpaka hii leo. Hivyo yanabaki kuwa ni Maamuzi halali na yenye nguvu kisheria na kwamba kueleza ukweli huu hakuwezi kuwa ni kumchafua au kumkashifu Bw. Sethi. Mwizi kuitwa Mwizi si Tusi, bali ni sifa yake na inamstahili.

Vile vile Serikali ilimshtaki Bw. Sethi kwa uchotwaji na utakatishaji wa fedha kupitia Mkurugenzi wa Mashtaka DPP kulikopelekea Bw. Sethi huyu huyu kukiri Makosa na Jinai hiyo Mahakamani na hivyo kuingia katika Makubaliano na Mkurugenzi wa Mashtaka DPP kupitia utaratibu wa Plea Bargain na hivyo kuamriwa kulipa kiasi cha zaidi ya shilingi Bilioni 26 fedha ambayo alilipa kiasi cha Milioni Mia Mbili na kuachiwa huru akiahidi kumaliza kiasi kilichobaki ndani ya miezi 18 lakini mpaka leo ikiwa ni zaidi ya miaka minne pesa hizo hazijalipwa. Bw. Sethi ni mhalifu mwenye hukumu katika kichwa chake lakini aliyepewa fursa ya kukanyaga sheria na kuwadhihaki Watanzania kwa Kodi zao.

Maombi ya kufungwa kwa Kampuni (Winding up) yaliyopelekwa na Mbia wa IPTL, Eurasia Holdings dhidi ya IPTL. Hivi ninavyozungumza na nyie kuna kesi ya kufuta hii kampuni iliyofunguliwa na ile kampuni niliyosema hapo awali ilikuwa na hisa moja, wale wanahisa wengine sasa wanataka IPTL ifungwe, swali ni je, nini hatma ya kodi zetu ? kupitia fidia ambayo Bw. Sethi na PAP wanapaswa kuilipa kwa Serikali? Hatupigwi mchanga wa Macho na Bw. Sethi na PAP?

Ndugu zangu Wahariri na Wanahabari,

Mtu, anayefanya haya yote na kuliingizia taifa hasara yote hii anatakiwa aitweje? Je kuyaongea haya hadharani ni kumkashifu mtu na kumdhalilisha? Je kuchambua ripoti ya CAG siku hizi imekuwa “defamation”?, Bw. Sethi anapata wapi ujasiri na uthubutu wa kiwango hiki ? Nchi hii imekuwa ya kuchezewa kwa kiwango hiki ?

HATA HIVYO, Sasa niwaambie jinsi ambavyo mtu huyu alivyo hatari kwa Taifa letu. Baada ya kusaini Settlement Deed na Serikali katika kesi yake na baada ya kusaini plea bargain na kukubali kosa na Mitambo ya IPTL kuwekwa chini ya Serikali, Bw. Sethi ameendelea na harakati zake. Hivi sasa amefanya mabadiliko katika bodi ya ukurugenzi na umiliki wa hisa katika kampuni ya IPTL. Kwanza amemweka mtu mmoja anaitwa RAJIV SHASHI NANDHA kuwa Mkurungezi. Lakini pia ameingiza kampuni inayoitwa KARENGA PTY LTD kuwa ndio mwanahisa mkuu (majority shareholder) kwenye IPTL mwenye hisa 150,000. Utafiti wangu unaonyesha kuwa hii kampuni ya KARENGA ni kampuni ya Kiaustralia inayomilikiwa na Bw. Sethi, Mke wa Sethi na Mtoto (Binti) wa Sethi. Hivyo Sethi anaendelea kutaka kumiliki kile alichoambiwa na mahakama sio chake lakini pia kutengeneza mpango wa muda mrefu wa kuendelea kuisumbua Serikali na walipa kodi wa Tanzania kupitia mpango mwingine wa kihalifu.

Anafanya yote haya huku akijua kuna maamuzi ya Mahakama ya Rufaa yanayofuta maamuzi ya Jaji Utamwa yaliyoipa PAP umiliki wa IPTL, Akijua fika kuhusu Makubaliano aliyoingia na Serikali kwenye kesi yake dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), wakati huo huo akiipa kisogo Plea Bargain aliyoingia na DPP na licha ya kesi ya Eurasia ya Kuifunga IPTL inayoendelea Mahakamani.

Niambieni mtu wa namna hii anastahili hadhi na heshima ipi kwa Taifa letu?

Ndugu zangu, suala hili limekua ni Jinamizi linaloitafuna Taifa letu kwa muda mrefu sana, kila njia aliyotumia huyu bwana imeshindikana lakini kila mwaka linaibuka tena na tena. Ni zimwi lililokataa kutula likapita. Watawala wamekuwa na kigugumizi kuzika huu mzoga. Maamuzi ya Mahakama yapo lakini hayafanyiwi kazi. Cha ajabu huyu mtu anatamba tu mtaani. Ifike mahali wenye mamlaka wamalize hili jambo kwa Maslahi na heshima ya Watanzania.

Kibri na Jeuri ya Bw. Sethi inafikirisha. Si mara ya kwanza Bw. Sethi kunifungulia kesi ya namna hii. Nimeamua kwa dhati ya moyo wangu kuwa nitapambana naye Mahakamani na kuweka wazi ukweli wa suala hili ili Watanzania na Dunia isikie.

Ndugu Wahariri na wanahabari, ombi langu kwenu ni kuwa wakati kesi hii inaendelea mje Mahakamani ili UMMA wa Watanzania upate taarifa sahihi juu ya Bw. Sethi na dhamira yake ovu kwa Taifa hili.

Nawashukuru kwa Kunisikiliza.

ZITTO ZUBERI KABWE

/ Published posts: 2063

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram