23 views 4 mins 0 comments

KATIBU MKUU MKOMI AZISISITIZA TAASISI ZA UMMA KUSHIRIKI KIKAMILIFU WIKI YA UTUMISHI WA UMMA; AWAALIKA WANANCHI KUJITOKEZA KWA WINGI KUPATA HUDUMA

In KITAIFA
May 28, 2025



Na Mwandishi wetu-Dodoma.

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi amezisisitiza Taasisi za Umma zilizoalikwa kushiriki Maonesho ya Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kushiriki kikamilifu maonesho hayo yatakayofanyika katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma kuanzia tarehe 16 hadi 23 Juni, 2025 ili wananchi waweze kupata huduma za papo kwa hapo zitakazotolewa na Taasisi hizo huku akitoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi katika maonesho hayo.

Katibu Mkuu Mkomi ametoa msisitizo huo leo Jumatano, Mei 28, 2025 jijini Dodoma wakati wa Mkutano wake na Waandishi wa Wahabari kuhusu Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kitaifa.

Katibu Mkuu Mkomi amezitaja huduma zitakazotolewa papo kwa hapo kuwa ni vyeti vya kuzaliwa, vitambulisho vya taifa (NIDA), hati za viwanja, kupima afya kutoka Hospitali za Benjamin Mkapa, Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Muhimbili, Taasisi ya Mifupa (MOI) pamoja, huduma ya Gazeti la Serikali na nyingine nyingi.

โ€œNipende kutumia fursa hii kuwakaribisha wakazi wa Jiji la Dodoma na maeneo jirani, Watumishi wa Umma na wadau wa utumishi wa umma nchini kuhudhuria maonesho haya adhimu ili kujipatia huduma hizo amesema Bw. Mkomi.

Amesema katika maadhimisho hayo, Wizara, Sekretarieti za Mikoa na Taasisi za Umma zitafanya maonesho hayo na kutoa elimu kuhusu utekelezaji wa majukumu yao huku Ofisi ya Rais, UTUMISHI na Utawala Bora itaendesha kliniki ya kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma nchini papo kwa hapo.

Huduma hizo za papo kwa hapo zinaenda sambamba na kaulimbiu ya maadhimisho hayo kitaifa isemayo Himiza Matumizi ya Mifumo ya Kidijiti ili Kuongeza Upatikanaji wa Taarifa na Kuchagiza Uwajibikaji
Akizungumzia umuhimu wa wananchi kujitokeza kwa wingi katika maonesho hayo, Bw. Mkomi amesema Maadhimisho hayo ya Wiki ya Utumishi wa umma ni jukwaa la Wananchi kupata fursa ya kufahamu wajibu wao na haki zao ili pindi wanapokosa haki zao waweze kujua namna ya kuzipata.

Vilevile, Bw. Mkomi ametaja faida na malengo ya maadhimisho hayo kwa Taasisi za Umma kuwa zitapata fursa ya kubadilishana uzoefu juu ya mbinu na mikakati mipya ya namna ya kutoa huduma bora kwa Umma pamoja na kupokea ushauri kutoka kwa wadau mbalimbali wakiwemo Wananchi, AZAKI, na Sekta Binafsi juu ya namna bora ya kuboresha utoaji huduma.

Ameongeza kuwa, Taasisi hizo zitapata fursa ya kuonyesha ubunifu waliofanya katika maeneo mbalimbali ya utoaji huduma na kuondoa urasimu usiokuwa wa lazima katika michakato mbalimbali ya utoaji huduma ikiwa ni pamoja na kupata mrejesho na kuutumia mrejesho huo kurekebisha kasoro za utendaji zinazosababisha malalamiko ya wateja ili huduma za Serikali ziboreshwe kukidhi matarajio ya Wananchi

Katika hatua nyingine Bw. Mkomi amewataka Watumishi wa Umma wote, kutimiza suala la kikatiba kuelekea katika Uchaguzi Mkuu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wabunge na Madiwani Mwezi Oktoba, 2025 kujitokeza katika Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ili muda wa uchaguzi utakapofika waweze kuchagua viongozi bora kwa maendeleo ya taifa lao katika maeneo wanayofanyia kazi.

Wiki ya Utumishi wa Umma nchini huanza tarehe 16 Juni kila mwaka na huadhimishwa kwa kufanya mambo mbalimbali ikiwemo maonesho, kutoa elimu na huduma za papo kwa hapo ili kuifikia Siku ya Utumishi wa Umma ambayo husherehekewa na nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) tarehe 23 Juni kila mwaka.

/ Published posts: 2136

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram