11 views 2 mins 0 comments

DKT. DIALLO: MAAFISA BIASHARA MAMLAKA YA SERIKALI ZA MITAA HAMASISHENI UPATIKANAJI WA MAWAKALA WA MBOLEA

In BIASHARA
May 29, 2025



Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Anthony Diallo, amezishauri Idara za Biashara za Halmashauri kuhamasisha upatikanaji wa mawakala wa mbolea ndani ya halmashauri zao ili kusogeza huduma hiyo karibu na wakulima.

Dkt. Diallo amesema hatua hiyo itapunguza umbali na gharama wanayokabiliana nayo wakulima  ya kufuata pembejeo hiyo muhimu mbali na yaliko mashamba yao.



Dkt. Diallo ametoa wito huo leo, tarehe 28 Mei 2025, alipokuwa akizungumza na Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Bi. Mary Makondo, katika ziara ya kikazi ya Bodi ya Mamlaka hiyo.

Aidha, Dkt. Diallo ameiomba Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kuratibu zoezi la kutumia soil scanner kupima afya ya udongo ya mashamba ya wakulima ili kubaini mahitaji halisi ya mbolea kulingana na aina ya udongo.



Ameeleza kuwa, hatua hii itasaidia kuepuka hasara inayoweza kujitokeza endapo wakulima watatumia mbolea bila kutambua mahitaji halisi ya  virutubisho ili kukuza mimea katika mashamba yao.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Bi. Makondo, amekiri kupokea na kufanyia kazi maelekezo hayo kwa kutumia maafisa biashara wa mkoa na halmashauri kuhamasisha wafanyabiashara kufungua maduka ya pembejeo karibu na wakulima ili kuwapunguzia gharama na muda wa kufuata mbolea.



Bi. Makondo ameongeza kuwa Mkoa wa Ruvuma unaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa mpango wa ruzuku ya mbolea, huku jitihada zikielekezwa katika kuhamasisha wakulima kujisajili kwenye mfumo wa usajili wa pembejeo za kilimo.

Katibu tawala Makondo amesema katika kipindi cha miaka mitatu ya utekelezaji wa mpango huo wa ruzuku, mkoa wake ulikuwa na lengo la kusajili wakulima 429,991 ambapo mpaka sasa wakulima 418,293 wamesajiliwa na wakulima 288,212 wamenufaika kwa kununua tani  291,917.136 za mbolea kwa bei ya ruzuku. Zenye thamani ya ruzuku Bilion 105 ambazo zimetolewa na Serikali kugharimia ruzuku ya mbolea



Ziara hiyo ya Siku tatu kuanzia tarehe 27 hadi 29 Mei, 2025 kwenye mikoa ya Nyanda za juu Kusini imelenga kufuatilia utekelezaji wa mpango wa ruzuku ya mbolea kwa mazao ya kimkakati ya kahawa na parachichi.

/ Published posts: 2133

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram