
Na Mwandishi Wetu
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo amesema kuwa Serikali imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji hususan kwenye ujenzi wa viwanda vya kutengeneza vifaa tiba, ikiwemo vinavyotumika katika kutoa huduma ya afya ya kinywa na meno hapa nchini.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri Jafo katika ufunguzi wa maonesho ya Afya ya Kinywa na Meno katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Idara ya Diplomasia ya Uchumi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi John Ulanga amesema ukuaji wa sekta hiyo hapa nchini ni lazima uende sambamba na matumizi ya vifaa vya kisasa ili kuenda sambamba na maendeleo ya nchi nyingine.
“Tanzania inaweza kuwa kinara wa utoaji huduma za afya ya kinywa na meno ikiwa uwekezaji mkubwa utafanyika katika vifaa tiba,”
“Na hii sio tu itasaidia ukuaji wa sekta hiyo hapa nchini, bali pia itasaidia wataalamu wetu kutambulika kimataifa,” amesema katika maonesho hayo yaliyoandaliwa na Chama cha Madaktari wa Kinywa na Meno Tanzania.
Amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, imeweka kipaumbele katika kuboresha huduma za afya, hususan afya ya kinywa na meno na kufanyika kwa maonesho hayo ni kielelezo tosha cha ukuaji wa sekta hiyo hapa nchini.
“Nimefurahia sana kuona teknolojia za hali ya juu katika maonesho ya vifaa tiba hapa nchini,”
“Matumizi ya vifaa tiba vya kisasa yanasaidia utoaji huduma bora na za kisasa na kutufanya kuwa washindani katika soko la kimataifa,” amesema.
Aidha, Balozi Ulanga alihamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki maonesho hayo, akibainisha kuwa uchunguzi wa afya ya kinywa na meno unafanyika bure kwa ushirikiano kati ya Serikali na wa afya ya kinywa na meno hapa nchini.
Aliongeza kuwa maonesho hayo ni ya kipekee na ni sehemu ya utalii wa kimatibabu kwa kuhusisha wataalamu mbalimbali kutoka nje ya nchi.
“Nimeona washiriki kutoka nchi mbalimbali duniani ambao wanashiriki maonesho haya na kubadilishana uzoefu na wataalamu wetu wa hapa nchini,”
“Hii ni muhimu sana katika ukuaji wa sekta hii na kuvutia wawekezaji wengi zaidi,” amesema.
Amewapongeza waandaaji wa maonesho hayo na kusema kuwa yanafungua milango ya fursa kwa wadau wa sekta ya afya, wakiwemo watoa huduma, wauzaji wa vifaa tiba na wataalamu wa afya ya kinywa na meno.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Dental Expo, Dkt. Ambege Mwakatobe, alieleza kuwa tukio hilo ni muhimu sana kwa jamii, kwani hutoa fursa adimu kwa wananchi kukutana na madaktari bingwa wa kinywa na meno.
Hata hivyo, amewataka wadau kuendelea kutoa elimu ya huduma ya afya ya kinywa na meno kwa wananchi.
“Tanzania ina zaidi ya watu milioni 60, lakini ni nusu tu ya idadi hiyo waliowahi kupimwa afya ya kinywa na meno. Hii inaonesha umuhimu wa kuendelea kutoa elimu na kuongeza upatikanaji wa huduma hizi muhimu. Tunawahimiza wananchi wajitokeze kwa wingi kupata huduma hizi bure,” alisisitiza Dkt. Mwakatobe.
Alieleza pia kuwa licha ya kuwa ni mara ya kwanza kwa maonesho hayo kufanyika nchini, muitikio wa wananchi umekuwa mkubwa.
Aidha, wataalamu kutoka mataifa mbalimbali duniani kama Ujerumani, Uingereza, Marekani pamoja na nchi za Afrika zikiwemo Kenya, Uganda, Afrika Kusini na Zambia wameshiriki katika maonesho hayo.
Naye Afisa Biashara Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), Bw. Chrispin Luanda, alisema kuwa TANTRADE inaunga mkono jitihada za Serikali na sekta binafsi kwa kuhakikisha kuwa mazingira bora ya uwekezaji katika sekta ya afya yanaimarishwa.
“Tunawaalika wawekezaji kuchangamkia fursa zilizopo katika sekta ya afya, hasa kupitia ushirikiano baina ya sekta binafsi na Serikali, kwa lengo la kuboresha huduma na kukuza uchumi wa nchi,” alisema Bw. Luanda.
Mbali na maonesho hayo, washiriki wakiwemo madaktari pia wanapata fursa ya kuhudhuria semina kuhusu maeneo mbalimbali ya huduma za afya ya kinywa na meno na kujionea vifaa vya kisasa zinavyotumika katika matibabu ya kinywa na meno.
Maonesho haya yanatarajiwa kuwa chachu ya mabadiliko katika uboreshaji wa huduma za afya ya kinywa na meno nchini, na kuchochea ushiriki wa sekta binafsi katika maendeleo ya viwanda vya vifaa tiba.