13 views 2 mins 0 comments

ELIMU YA NISHATI SAFI YA UMEME KUPIKIA YAWAKOSHA WAANDISHI WAENDESHA OFISI NCHINI

In KITAIFA
May 16, 2025



Na. Mwandishi Wetu Arusha.

Waandishi Waendesha Ofisi kutoka taasisi mbalimbali nchini wamelipongeza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kuwapatia elimu sahihi ya matumizi ya Nishati Safi ya umeme kupikia hali itakayosaidia kuondokana na matumizi ya Nishati zisizo salama ikiwemo kuni na Mkaa.

Wamebainisha hayo tarehe 15, 2025 baada ya kutembelea Banda la TANESCO katika maonesho yanayoendelea katika viwanja vya Ngurudoto Wilaya ya Arumeru Mkoani Arusha.

Wamesema kutokana na kukosa elimu sahihi ya matumizi ya Nishati ya umeme kupikia wengi wao walikuwa wanaogopa kutumia umeme kupikia wakihofia gharama kubwa kutokana na matumizi ya vifaa vya umeme ambavyo havijathibitishwa.

Wameeleza kuwa katika Banda la TANESCO wamejionea vifaa vya kisasa vya umeme vya kupikia ikiwemo majiko maalum (Induction) pamoja na ‘pressure cooker’  vinavyotumia umeme kidogo na kuwahamasisha kuanza kutumia Nishati safi ya umeme kupikia.

“Leo nimepatiwa elimu nzuri kuhusu matumizi ya Nishati ya umeme kupikia na nimekuta wanayo majiko mazuri ambayo ukiyatumia yanaokoa muda na pia yanaokoa umeme ukilinganisha na yale majiko ya zamani,” amesema Adventina Kajuna Mwandishi Mwendesha ofisi ELCT Kagera.

Afisa Masoko Kutoka TANESCO Bi. Adelina Lyakurwa amesema Shirika hilo limeamua kushiriki katika Mkutano huo kwa lengo la kuhamasisha washiriki wa mkutano  pamoja na wananchi mbalimbali waliojitokeza katika maonyesho ya Mkutano huo kutumia Nishati safi ya umeme kupikia kwani ni gharama nafuu zaidi kuliko Nishati zingine.

“TANESCO tumetumia fursa ya Mkutano huu wa Waandishi Waendesha Ofisi Tanzania kutangaza Ajenda Nishati Safi ya Kupikia ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo, tumewahamasisha washiriki wa Mkutano huu pamoja na wananchi waliojitokeza kutumia Nishati Safi ya Umeme kupikia kwani ni haraka, nafuu na inaokoa mazingira,” Amesema Adelina Lyakurwa Afisa Masoko TANESCO.

Aidha, katika Mkutano huo TANESCO imeibuka kidedea kwa kutwaa tuzo  ya kupeleka idadi kubwa ya washiriki kwenye mkuutano wa 12 wa mwaka 2025 wa Waandishi Waendesha Ofisi (TAPSEA) ambapo zaidi ya Waandishi Waendesha Ofisi zaidi ya 90 kutoka TANESCO wameshiriki Mkutano huo na wametumia fursa hiyo kuishukuru kwa kuwawezesha kushiriki katika Mkutano huo.

Tuzo hiyo imekabidhiwa na Makamu wa Rais wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango na kupokelewa na Afisa Masoko kutoka Tanesco Adelina Lyakurwa pamoja na Lucy Kishari Mwandishi Mwendesha Ofisi TANESCO Mkoa wa Morogoro.

/ Published posts: 2061

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram