27 views 5 mins 0 comments

TANZANIA YAZALISHA JUMLA YA FUTI ZA UJAZO BILIONI 301.33 ZA GESI ASILIA, PURA yaanika mafanikio miaka minne Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia

In BIASHARA
May 19, 2025
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Mhandisi Charles Sangweni akizungumza katika kikao kazi Kati ya Ofisi ya Msajili wa Hazina, Jukwaa la Wahariri TEF na PURA kilichofanyika Jijini Dar es Salaam Mei 19, 2025.

Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA

MAMLAKA ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imesema katika kipindi cha Machi 2021 hadi Machi 2025, Tanzania imezalisha jumla ya futi za ujazo bilioni 301.33 za gesi asilia.

Hayo yamebainishwa leo Mei 19, 2025 na Mkurugenzui Mkuu wa PURA, Mhandisi Charles Sangweni akizungumza na wahariri na waandishi wa habari kwenye kikao kazi kilichoratibiwa na ofisi ya Msajili wa Hazina jijini Dar es Salaam, ambapo ameainisha mafanikio yaliyopatikana katika miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita.



Mhandisi Sangweni ameeleza kuwa kati ya hizo, futi bilioni 142.35 zilitoka katika kitalu cha Mnazi Bay na bilioni 158.98 kutoka Songo Songo, kwamba hiyo ni sawa na wastani wa futi bilioni 35.59 kwa mwaka kutoka Mnazi Bay na futi bilioni 39.74 kutoka Songo Songo.

“Ikilinganishwa na kipindi cha nyuma, uzalishaji wa gesi umeongezeka, ambapo awali Mnazi Bay ilikuwa ikizalisha wastani wa futi bilioni 32.03 kwa mwaka, huku Songo Songo ikizalisha futi bilioni 25.13 kwa mwaka,” amesema Mhandisi Sangweni.



Kwamba Gesi hiyo imetumika katika matumizi mbalimbali ikiwemo uzalishaji wa umeme, viwandani, majumbani, taasisi za umma na binafsi, pamoja na kwenye magari.

“Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita, mafanikio makubwa yamepatikana katika sekta ya mafuta na gesi asilia nchini Tanzania.  Mafanikio haya ni matokeo ya usimamizi madhubuti wa Serikali, uwekezaji wa kimkakati, pamoja na matumizi ya teknolojia za kisasa katika shughuli za utafutaji, uzalishaji na usambazaji wa gesi,” amesisitiza Mhandisi Sangweni.



Kwamba  mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kutolewa kwa leseni ya uendelezaji katika eneo la ugunduzi la Ntorya hatua inayotarajiwa kuongeza uzalishaji wa gesi asilia nchini, kadhalika ameeleza kuhusu ukarabati wa visima vitano vya gesi, ambao umeongeza uimara na ufanisi wa uzalishaji.

Mhandisi Sangweni ameongeza kuwa PURA imeimarisha uhakiki na ukaguzi wa mikataba ya uzalishaji na ugawanaji wa mapato, hatua inayolenga kuhakikisha kuwa Serikali inanufaika ipasavyo.



Amesema pia kumekuwa na ongezeko la ushiriki wa wazawa katika shughuli za mkondo wa juu wa petroli, ikiwa ni pamoja na usimamizi wa vitalu vya utafutaji.

“Kampuni za kizawa zimeingia ubia na kampuni za kimataifa katika utoaji wa huduma za kitaalamu na kiteknolojia. Aidha, matumizi ya mifumo ya kidijitali katika shughuli za mafuta na gesi yameongezeka kwa kiwango kikubwa,” amesema Sangweni.



Amebainisha kuwa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limeimarika katika ukusanyaji wa data za mitetemo kwa ajili ya utafiti wa mafuta na gesi, na limewezesha pia tafiti za awali za kijiolojia, kijiofizikia na kijiokemia hatua muhimu katika utafutaji wa rasilimali.

Mhandisi Sangweni ameeleza kuwa PURA imeongeza ushirikiano wake na taasisi za udhibiti katika ukanda wa Afrika Mashariki, vilevile, mfumo wa udhibiti wa sekta umeboreshwa kupitia uandaaji na usasishaji wa kanuni na miongozo ya kisheria.



“Majadiliano ya uwekezaji kwa mradi mkubwa wa kuchakata gesi kuwa kimiminika yanaendelea. Pia, idadi ya watumishi imeongezeka kutoka 45 mwaka 2021 hadi kufikia 93 mwaka 2025, hali iliyosaidia kuongeza ufanisi katika usimamizi wa mkondo wa juu wa mafuta na gesi,” ameongeza Mhandisi Sangweni.

Kwamba kwa mujibu wa mikataba ya Ushirikiano wa Uzalishaji (PSA), mwekezaji huwekeza fedha zake mwenyewe katika shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi ambapo endapo atafanikiwa, hupata marejesho ya uwekezaji wake kupitia mgao wa mapato, kodi, tozo na hatimaye Serikali pamoja na TPDC hupokea mgao wao baada ya gharama hizo kutekelezwa.



Amesema PURA imeendelea kufanya uhakiki wa kina wa gharama na mapato ili kuhakikisha Serikali inapata mgao wake stahiki na kwamba kupitia kaguzi hizo, zaidi ya Shilingi bilioni 340 zimerejeshwa kwenye mfuko wa ugawanaji wa mapato kati ya Serikali na wawekezaji fedha ambazo zingeweza kurejeshwa kwa wawekezaji kama sehemu ya mtaji wao.

Kadhalika, Serikali kupitia PURA imeanza maandalizi ya duru ya tano ya kunadi vitalu vipya vya utafutaji wa mafuta na gesi, ikiwa ni mara ya kwanza tangu mwaka 2013. Zoezi hili linatarajiwa kuvutia wawekezaji wapya na kufungua ukurasa mpya wa maendeleo katika sekta ya mafuta na gesi nchini.

/ Published posts: 2081

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram