43 views 2 mins 0 comments

ESSA NA TPDC YASAINI MAKUBALIANO YA USAMBAZAJI WA GESI ASILIA NA KUAZISHA KIWANDA CHA UZALISHAJI MTWARA

In BIASHARA
May 19, 2025

Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA

Kampuni ya Essa kutoka Indonesia na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) leo wamesaini makubaliano ya awali ya usambazaji wa gesi asilia kwa ajili ya kuanzisha kiwanda cha uzalishaji wa mbolea mkoani Mtwara.

Kiwanda hicho kinatarajiwa kutumia gesi asilia kama malighafi kuu katika uzalishaji.

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini iliyofanyika Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Kampuni ya Essa, Bw. Rahul Puri, amesema hatua hiyo ni muhimu katika kuelekea makubaliano rasmi ya usambazaji wa gesi, ambapo watashirikiana na TPDC kuhakikisha mahitaji ya gesi kwa ajili ya uzalishaji wa mbolea yanatimizwa kikamilifu kwa wakulima wa Tanzania.

“Mradi huu si wa Kampuni ya Essa peke yake, bali ni wa Watanzania wote. Tunashirikiana na taasisi kama TFRA, TFC, TPDC na TIC kuhakikisha mradi unafanikiwa na uzalishaji wa mbolea unakuwa wa kutosha kwa matumizi ya ndani na kuuza nje ya nchi,” alisema Bw. Puri.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mipango na Uwekezaji wa TPDC, Bw. Deric Moshi, alisema makubaliano hayo yanalenga kuiwezesha Kampuni ya Essa kufanya maandalizi ya awali na kuwasilisha kiwango halisi cha mahitaji ya gesi pamoja na bei, ambapo TPDC itakuwa msambazaji mkuu wa gesi hiyo.

Aliongeza kuwa TPDC imejipanga kuhakikisha upatikanaji wa gesi ya kutosha kwa ajili ya kiwanda hicho na vinginevyo, kufuatia maendeleo ya uendelezaji wa visima vya gesi vinavyoendelea nchini.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Anthony Diallo, alisema kiwanda hicho kitakuwa suluhisho la kudumu kwa changamoto ya upatikanaji wa mbolea nchini, kwani malighafi nyingi zinapatikana ndani ya nchi.

“Kwa sasa Tanzania inaagiza takribani tani milioni moja za mbolea kutoka nje ya nchi. Kiwanda hiki kitasaidia kupunguza matumizi ya fedha za kigeni na kuongeza uzalishaji wa ndani,” alisema Dkt. Diallo.

Balozi wa Indonesia nchini Tanzania, Mheshimiwa Yogo, alisisitiza kuwa mradi huo utaimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya Tanzania na Indonesia kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.

/ Published posts: 2076

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram