23 views 2 mins 0 comments

MCHINJITA AELEZEA ALIVYOKAMATWA NA POLISI KATIKA KITUO CHA MABASI YA UDART

In KITAIFA
May 23, 2025

Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA

Sakata la kukamatwa kwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo Tanzania Bara, Isihaka Mchinjita, katika kituo cha mabasi yaendayo haraka cha kampuni ya UDART kilichopo Kimara, limeibua mjadala mpana kuhusu haki ya viongozi wa Nyanja mbalimbali kutembelea maeneo ya umma na hali ya usafiri kwa wananchi katika jiji la Dar es Salaam.

Mchinjita alikamatwa na Jeshi la Polisi asubuhi ya siku ya Ijumaa Mei 23, 2025, baada ya kufika katika kituo hicho kwa lengo la, kama alivyoeleza, “kuona hali halisi ya usafiri wa mwendokasi na kusikiliza maoni ya wananchi”.

Akizungumza katika ofisi za chama hicho jijini Dar es Salaam mara baada ya kuachiwa, Mchinjita amesema walifika eneo hilo si kwa lengo la kufanya mikutano ya hadhara, bali kuchunguza changamoto zinazowakumba abiria.

Kwa mujibu wa Mchinjita, walikamatwa baada ya mvutano na maofisa wa UDART waliotaka waondoke katika eneo hilo kwa madai ya kukosa kibali, licha ya kuwa katika eneo la umma. Amesema kuwa walihamishiwa kutoka Kituo cha Polisi Kimara hadi Mbezi, wakashikiliwa kwa saa tano bila kufunguliwa kesi yoyote.

Hata hivyo, UDART kupitia Afisa Uhusiano wake, Gabriel Katanga akizungumza na Jambo TV kwa njia ya simu, ilitoa upande wake wa maelezo ikisema kuwa walichofanya viongozi wa ACT hakikuwa sahihi kwani walifika katika eneo hilo bila kutoa taarifa wala kibali cha kufanya tukio la kisiasa au la umma.

Katanga ameongeza kuwa kama ACT wangehitaji kufanya shughuli hiyo kwa utaratibu, wangeweza kupewa usaidizi hata wa askari, lakini walichofanya ni kuvamia eneo la huduma za umma bila maandalizi ya kisheria. Amesema baada ya maelezo polisi, viongozi hao waliachiliwa na kupewa elimu ya namna ya kufuata taratibu pindi wanapotaka kutembelea maeneo ya huduma kama hayo.

Hata hivyo, Katanga amesema kuwa UDART inatambua changamoto za usafiri na tayari hatua zimeanza kuchukuliwa na serikai. Amesema upungufu wa mabasi umesababishwa na mabasi yaliyopo kuwa ya muda mrefu tangu mwaka 2016, na uwezo wake wa kutoa huduma umeanza kupungua.

/ Published posts: 2106

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram