

Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA
Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) kwa kushirikiana na JamiiAfrica na taasisi ya kimataifa ya IMS, wamezindua rasmi mradi wa miaka mitatu unaolenga kuwajengea uwezo waandishi wa habari nchini katika maeneo ya usalama na mapambano dhidi ya habari zisizo sahihi na upotoshaji.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika leo Mei 6,2025 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa UTPC, Bw. Kenneth Simbaya, amesema mradi huo umelenga kuimarisha uandishi wa habari unaoweka mbele maslahi ya wananchi.

“Kwa sasa kuna upungufu wa uandishi unaozingatia maslahi ya wananchi. Mradi huu utawakumbusha waandishi umuhimu wa kutoa habari sahihi zitakazosaidia jamii kufanya maamuzi bora,” amesema Simbaya.
Aidha, amebainisha kuwa mradi huo utajikita pia katika kuimarisha usalama wa waandishi wa habari wanapotekeleza majukumu yao, hususan katika mazingira hatarishi, huku Klabu za Waandishi wa Habari zilizopo nchi nzima zikitarajiwa pia kuwa chombo muhimu cha utekelezaji wa mradi huo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa JamiiAfrica, Maxence Melo, amefafanua kuwa mradi huo ulianza kutekelezwa mapema mwaka huu baada ya kutangaza nafasi za ushirikiano mwaka 2024, licha ya kuasisiwa mwaka 2022.
“Mradi huu haulengi uchaguzi, bali unalenga wananchi. Katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi, waandishi wanapaswa kushirikishwa kikamilifu ili kusaidia wananchi kufanya maamuzi sahihi kwa kupata taarifa zenye ukweli,” ameeleza Melo.

Ameongeza kuwa tangu mwaka 2022, JamiiAfrica kupitia programu ya JamiiCheck imekuwa ikiwezesha waandishi wa habari na wazalishaji wa maudhui mtandaoni kutumia mbinu za kisasa katika kupambana na upotoshaji wa taarifa.
“Kwa kushirikiana na UTPC na IMS, tutaandaa shirikisho la pamoja la waandishi wa habari na vyombo vya habari ili kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi na kwa wakati,” amesema.

Miongoni mwa watoa mada katika uzinduzi huo alikuwa Imani Henrick Luvanga, mwandishi wa habari kutoka Crown Media na DW Kiswahili, amesisitiza umuhimu wa mafunzo kwa waandishi kuelekea uchaguzi mkuu.
“Katika zama hizi za mabadiliko ya kidijitali, upotoshaji wa taarifa ni changamoto kubwa. Mradi huu utasaidia sana kuwaandaa waandishi kuepuka kusambaza taarifa za uongo, hasa kwa kipindi hiki ambapo akili mnemba imekuwa ikitumika kupindisha uhalisia wa taarifa,” amesema Luvanga