
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejizatiti katika kupunguza changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi zikiwemo za sekta ya elimu.
Ameyasema hayo leo (Jumatatu, Mei 19, 2025) wakati akizungumza na wananchi katika mikutano wa hadhara iliofanyika Sengerema mjini na Buchosa wilaya ya Sengerema akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza.
Waziri Mkuu amesema miongoni mwa hatua ambazo Serikali imezichukua ni pamoja na kuendelea kutoa elimu msingi bila ya ada na hivyo kuwawezesha watoto wa kitanzania wenye umri wa kwenda shule kupata elimu.
Mheshimiwa Majaliwa amesema kwa sasa Serikali inaendelea na ujenzi wa shule za msingi na sekondari katika maeneo mbalimbali nchini hususani katika yale yenye msongamano mkubwa wa wanafunzi.
โMkakati mwingine mkubwa unaoendelea kutekelezwa na Serikali ni ujenzi wa mabweni, nyumba za walimu, pamoja na kujenga shule za amali ili wanafunzi watakapomaliza shule hizi waondoke na ujuzi.โ
Akizungumzia kuhusu changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama, Waziri Mkuu amesema kwa sasa Serikali inatekeleza miradi ya maji ikiwemo ya kutoa maji katika Ziwa Victoria na kuyasambaza kwa wananchi, hivyo amewataka waendelee kuwa na subira.
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema uhakikishe unakamilisha mchakato wa ujenzi wa mradi wa soko la halmashauri hiyo ili Sengerema iweze kuwa kituo kikubwa cha biashara.
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amewahakikishia wakazi wa wilaya ya Sengerema kuwa Serikali ipo katika hatua za mwisho za kumkabidhi mkandarasi kazi ya ujenzi wa barabara ya Sengerema-Nyehunge ili aanze ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami.