

Na Madina Mohammed DAR ES SALAAM WAMACHINGA
Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo (JWK) imeishauri serikali kuchukua hatua ya dharura ili kumaliza changamoto ya wafanyabiashara wazawa na raia wakigeni wa Kariakoo.
Mwenyekiti wa JWK, Severini Mushi alisema hayo jana Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Alisema hadi sasa wamebaini kuna changamoto za sheria za biashara za kumlinda mfanyabiashara mzawa.
“Tunaiomba serikali kuchukua hatua za dharura ili kumaliza changamoto hii, na tunaona kuna uharaka wa kupata sheria inayosema wafanyabiashara wazawa wanapaswa kufanya na nini wawekezaji wa kigeni wanapaswa kufanya ili kuondoa chuki zilizopo,” alisema Mushi.

Katibu wa JWK, Renatus Mlelwa alisema licha ya oparesheni ya serikali inayoendelea bado wanakumbana na baadhi ya changamoto ya mfumo wa biashara kwa sababu kwa muda mrefu wamekuwa wakiwatambua raia wa kigeni walioko Kariakoo ni wawekezaji kumbe ni wachuuzi na wamejisajili biashara bila ya kuwa na vibali vya kuonyesha kama wao ni wawekezaji.
Alisema walikaa kikao na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ili kutambua kama raia hao ni wawekezaji lakini walielezwa kwamba wawekezaji wanaowatambua ni wale waliofungua kiwanda na wanazalisha bidhaa na si mtu anayeleta bidhaa iliyokamilika.

“Tunalalamika kwasababu tunaona mfanyabiashara wa kigeni yupo karikakoo anaingiza nchini bidhaa ambazo zimekamilika na anauza wakati ilibidi tufanye sisi wazawa tatizo halipo TIC lipo kwa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) na Idara ya Uhamiaji,” alisema Mlelwa.
Alisema “Tunaiomba serikali iangazie hapo kama kweli tunataka kutatua changamoto kwa sababu kitendo hicho kinatengeneza chuki kwa wafanyabiashara wazawa na wageni, tuna tamani kuona wawekezaji wawe kwenye maeneo yao ya uzalishaji kiwandani na wasifanye biashara hadi kumfikia mlaji wa mwisho kuna tukwamisha wafanyabiashara wazawa kutofanya biashara,”.

Alibainisha kuwa Jumuiya hiyo haimlindi mkwepa kodi bali jukumu lao ni kuhakikisha wafanyabiashara wanauelewa juu ya umuhimu wa ulipaji kadi na waanalipa kodi.
Kwa upande wake Msemaji wa Jumuiya hiyo, Hendry Kanje alisema Januari 30, Mwaka huu Mwenyekiti wa Umoja wa wafanyabiashara wa Kariakoo alimueleza Rais Samia Suluhu Hassan namna wafanyabiashara wakigeni wanavyowasumbua wafanyabiashara wazawa.

Alisema Rais Samia alimuagiza Waziri wa Viwanda na Biashara, Selemani Jafo kuunda tume ya kuchunguza suala hilo.
Alibainisha kuwa tume hiyo ilifanya kazi na baada ya mwenzi ilileta matokeo ambayo hayakuzaa matunda ndipo Jaffo akaamua afike mwenyewe Kariakoo kushughulikia suala hilo.

“Waziri Jafo alipofika alijionea kuwa tulichokitarajia hakijafanyika kabisa, wageni bado wapo na wanaendelea kufanya biashara na akatoa agizo ianze oparesheni wakati tukiendelea kufanya oparesheni hiyo, siku sita zilizopita ilitokea taharuki na alipoona tume ya kwanza matokeo yake hayaridhishi ameunda tume nyingine inayotarajia kutoa majibu mwishoni mwa mwenzi huu,” alisema Kanje.