12 views 3 mins 0 comments

SOKO LA KISASA LA NYAMA CHOMA LAZINDULIWA VINGUNGUTI

In BIASHARA
May 25, 2025



Na John Mapepele


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe.Mohamed Mchengerwa   amezindua soko la kisasa la nyama choma la Kumbilamoto vingunguti, Ilala jijini Dar es Salaam na kushuhudia utiaji wa mikataba ya  miradi 6 ya maendeleo  yenye  thamani ya  shilingi bilioni 7.7


Mara baada ya kuzindua soko hilo ambalo limegharimu takribani shilingi milioni 727 amepongeza uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa kufanikisha mradi huo ambapo amezitaka Halmashauri nyingine kuiga  mfano huo.


Aidha, amefafanua kuwa soko hilo litakwenda kuwapatia ajira  wananchi wengi huku akisisitiza  kuendelea kulitunza  ili lisiharibike kwenye kipindi kifupi.


Mhe. Mchengerwa ameongeza kuwa kukamilika kwa soko hilo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na  kufafanua kuwa Serikali ya awamu ya sita tayari imekamilisha  miradi  mingi kama iilivyoahidi.


Wakati  huo huo Waziri Mchengerwa amezitaka Halmashauri zote nchini kutimiza malengo  zilizojiwekea ya ukusanyaji  mapato ili  ziweze kutekeleza  miradi ya  maendeleo huku akizitaka  kuendelea kubuni miradi  mbalimbali ya maendeleo yenye tija kwa wananchi na taifa kwa ujumla.


Akizungumzia kuhusu wakandarasi wazawa, Mhe Mchengerwa  amezitaka Halmashauri na mikoa  yote nchini kuwapa kipaumbele  wakandarasi wazawa huku akitoa wito  kuwachukulia hatua wakandarasi wanaofanya  vibaya  katika  kazi wanazopewa.


Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Edward Mpogole amemhakikishia Mhe. Mchengerwa kuwa  mikataba yote iliyosainiwa inakwenda kukamilika  kabla ya mwisho wa mwaka na kwamba wananchi watakwenda kunufaika  na miradi hiyo.


Katika uzinduzi wa soko hilo Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Zungu ambaye  pia ni Mbunge wa Ilala amewataka watanzania  kutojihusisha na uvunjaji wa amani   katika kipindi hiki  cha kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika  Oktoba  mwaka  huu

Bi. Amina Selemani ambaye  ni miongoni mwa mfanyabiashara  katika soko  hilo amemshukuru  Rais Samia Suluhu Hassan kutoa fedha za kujenga soko  hilo ambalo limetoa ajira  kwa akina mama wengi.


“Kwa kweli tunamshukuru Mheshimiwa Rais  wetu  kwa upendo huu wa kutuletea  mradi huu wa soko ambao  umekuwa ni ukombozi kwa  maisha yetu”. Amefafanua Amina

/ Published posts: 2102

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram