




Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Anthony Diallo, ametoa wito kwa wakulima wadogo wa miwa kupima afya ya udongo wa mashamba yao kabla ya kutumia mbolea, ili kuhakikisha wanatumia mbolea sahihi na kuongeza tija ya uzalishaji.
Dkt. Diallo amesema, “Ili kupata matokeo bora, ni muhimu kila mkulima kupima afya ya udongo wa shamba lake binafsi badala ya kuchukua sampuli za jumla ili kumsaidia mkulima kufanya maamuzi sahihi na kuepusha hasara.”
Kauli hiyo ameitoa tarehe 26 Mei, 2025, katika mkutano na wakulima wa Chama cha Msingi cha Ushirika wa Wakulima wa Miwa (AMCOS) cha Mkula, Halmashauri ya Wilaya ya Ifakara, mkoani Morogoro, wakati wa ziara ya kikazi ya Bodi na Menejimenti ya TFRA.
Dkt. Diallo amesema lengo la ziara hiyo ni kujifunza, kupokea changamoto za wakulima na kuzitafutia ufumbuzi pamoja na kuwahimiza kupima afya ya udongo ili kuongeza mavuno na kupunguza gharama zisizo za lazima.
Kwa upande wake, Meneja wa AMCOS hiyo, Clemency Mjami, ameishukuru serikali kwa kutoa ruzuku ya mbolea, akieleza jinsi ilivyosaidia kupunguza gharama kwa wakulima.
“Kupitia ruzuku hii, bei ya mbolea imepungua kutoka shilingi 120,000 hadi 68,000 kwa mfuko.
Wakulima wa AMCOS yetu wamepata jumla ya mifuko 11,740 ya mbolea sawa na tani 587, yenye thamani ya ruzuku ya shilingi 182,707,521 kwa kipindi cha miaka mitatu tangu 2022/2023,” amesema Mjami.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti Wakulima wameelekeza shukrani zao kwa serikali na kueleza kuwa Ruzuku hiyo imewasaidia sana na kuiomba serikali iendelee kutoa ruzuku hii kwani bila hiyo, wengi wao hawawezi kumudu gharama za pembejeo.
Mkulima mwingine kutoka Kijiji cha Msofini, Kata ya Mkula, Amanda Punguti, amesema ruzuku imewasaidia wakulima wenye hali duni kupata pembejeo na kuongeza uzalishaji.
“Ruzuku ya mbolea imekuwa mkombozi kwa wakulima wadogo. Tunaiomba serikali iendelee kutupa moyo huu wa kusaidia wakulima.”
Mara baada ya kikao hicho wajumbe na menejimenti ya TFRA walitembelea kiwanda cha sukari Kilombero kujifunza na kushauri namna bora ya kuongeza mashirikiano baina yao na wakulima wadogo wa miwa wanaowazunguka.