
Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe Albert Chalamila amezindua na kukabidhi magari mapya mawili kwa ajili ya katibu Tawala wa Mkoa huo na Mkuu wa wilaya ya Ilala ambapo amewataka kutumia magari hayo katika kutoa huduma kwa wananchi ili kutatua changamoto zao huku akisisitiza suala la kuhamasisha wananchi kuendelea kuhuisha taarifa zao kwa ajili ya uchaguzi mkuu 2025
Akizungumza leo Mei 20,2025 Jijini Dar es salaam RC Chalamila amesema magari hayo yametolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan ikiwa ni mkakati wa kuendana na Dira ya maendeleo ya Taifa hivyo amewataka viongozi wote waliokabidhiwa magari kufanya kazi ya kuwatumikia watanzania kwa uadilifu ili kubadili hali zao za maisha na kutatua changamoto zao
Aidha RC Chalamila pamoja na kumshukiru Rais Dkt Samia kwa kuendelea kuwezesha upatikanaji wa magari Mkoani humo pia amemshukuru kwa kuidhinisha fedha kiasi kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa katika mwaka huu wa fedha kutokana na uhitaji Mkubwa wa ofisi hiyo ambayo kwa sasa iko pamoja na ofisi ya mkuu wa wilaya ya Ilala
Vilevile RC Chalamila ametumia nafasi hiyo kuwakumbusha viongozi na wananchi wa Mkoa huo kutambua kuwa mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi hivyo ni muhimu kuendelea kuhuisha taarifa zao ili kuweza kushiriki uchaguzi mkuu wa mwezi oktoba mwaka huu ambapo amewataka viongozi kuendelea kuhamasisha wananchi kuhuisha taarifa zao kwa siku zilozobakia
Kwa upande wa Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es salaam Bwana Laurance Malangwa amemhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa magari hayo yatakwenda kutumika kwa kuzingatia taratibu za kisheria za serikali ili yaweze kudumu na kuhudumu kwa muda mrefu huku Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe Edward Mpogolo akiahidi kuwahudumia kwa karibu wananchi ili kutatua kero zao na kuwakumbusha suala la kuhuisha taarifa zao kwa ajili ya uchaguzi mkuu mwaka huu.