26 views 2 mins 0 comments

WANANCHI LINDI WATAKIWA KUCHANGAMKIA FURSA ZA MADINI

In KITAIFA
May 24, 2025

Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA

· *Waaswa kuacha uvivu*

· *Mgodi wa Elianje, injini ya maendeleo Namungo*


WANANCHI wa Mkoa wa Lindi wametakiwa kuacha uvivu na badala yake wachangamkie fursa zilizopo kwenye sekta ya  madini hususani katika mgodi wa kati  wa Elianje uliopo kitongoji cha Namungo, Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi.

Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti  wa  Kijiji  cha  Chingumbwa, kilichopo Kata ya Namungo, Abdallah Rashid akielezea fursa zilizopo mkoani humo kupitia Sekta ya Madini.

“Fursa zipo nyingi ni uvivu tu wa wananchi wetu, ukiangalia kwenye mgodi huu unaotuzunguka wa Elianje Genesis kuna fursa ya usambazaji vyakula, vinywaji, usafi, kupika, kusambaza vifaa vya usalama migodini, uchimbaji na uchenjuaji lakini ndio hivyo,”amesema Abdallah

Aidha, Mwenyekiti huyo amesema uwepo wa mgodi huo umetoa manufaa makubwa kwa wananchi kwa kuchimbiwa kisima cha maji ambacho kwa sasa kinahudumia kaya 918, awali kulikuwa na shida ya maji na wananchi walilazimika kutembea umbali mrefu kuchota maji.

“Pia, mwekezaji ametujengea shule ambayo kwa sasa ina wanafunzi 79, awali watoto walitembea umbali mrefu zaidi ya kilomita tatu kufuata shule vijiji vya jirani hali iliyopelekea baadhi yao kuacha shule. Pia mwekezaji amekua akitoa chakula kwa wanafunzi kipindi cha mitihani, kuwaletea vifaa vya michezo vya mpira  wa miguu kwa wanaume na netball kwa  wanawake na yupo mbioni kununua basi la shule,”amesema.

Kwa upande wa Mkuu wa shule ya msingi Chingumbwa iliyopo kata ya Mbekenyela mkoani humo, Joseph Raymond amesema mgodi wa Elianje umejenga ofisi za Walimu, kuwawekea umeme  kwa ajili ya kambi kwa darasa la saba na la nne itakayoanza mwenzi ujao wa sita  wakijiandaa na mitihani ya taifa.


Naye, Meneja wa Mgodi wa Elianje, Philibert Masawe akizungumzia mgodi huo amesema wanajishughulisha na  uchenjuaji wa madini ya dhahabu na uchimbaji wa ‘green garnet’,

Amesisitiza pia Kampuni ya Elianje imejenga  kituo cha mfano cha uchenjuaji wa madini ya dhahabu kinachotumia teknolojia ya CIP ambacho kina uwezo wa wa kuchenjua mbale (mwamba) ya dhahabu kiasi cha tani 500 kwa siku.

Amesema pia kiwanda hicho kimeajiri watanzania 300 na kuipongeza Serikali kuweka sera rafiki na sheria nzuri ambazo zinavutia uwekezaji.

/ Published posts: 2108

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram