
Baada ya wanachama wa CHADEMA wanaotokana na kundi linalojitambulisha kama G55 ndani ya chama hicho kuzungumza na waandishi wa habari, tarehe 22 Aprili 2025, na kueleza kukata tamaa kwao kutokana na kile walichokiita kiburi cha viongozi wao, hasa baada ya viongozi hao kushindwa kusaini kanuni za uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu, hali inayowanyima haki ya kushiriki katika uchaguzi mkuu, Katibu Mkuu wa chama cha NLD, Doyo Hassan Doyo, ametumia nafasi hiyo kuwaalika wanachama hao kujiunga na chama cha NLD.
Akizungumza akiwa mkoani Tanga katika shughuli za kuimarisha uhai wa chama, Doyo alisema kuwa yapo maelfu ya Watanzania, wakiwemo wanachama wa CHADEMA zaidi ya 200 waliokuwa na dhamira ya kugombea nafasi mbalimbali za uwakilishi, lakini sasa wamevunjika moyo kutokana na uamuzi wa chama chao kutosaini kanuni za maadili ya uchaguzi.
Msemaji wa kundi hilo, John Mrema, alieleza kuwa wanachama hao walikuwa na nia ya dhati ya kushiriki katika mchakato wa kidemokrasia kwa kugombea na kuchaguliwa, lakini sasa wamekosa jukwaa la kufanya hivyo. Hali hiyo imewafanya wajisikie kusalitiwa na viongozi wao wa juu.
Kutokana na hali hiyo, Doyo Hassan Doyo amewahimiza wanachama wa kundi la G55 kuchukua hatua madhubuti kwa kujiunga na chama cha NLD ili kutekeleza malengo yao ya kikatiba ya kuchagua na kuchaguliwa, pamoja na dhamira yao ya kuwatumikia Watanzania.
“Siasa inafanyika popote pale. Ni suala la kujiamini,” alisema Doyo na kuongeza: “Mimi mwenyewe nilikuwa katika chama X, nikaondoka na sasa nipo NLD. Nawaomba ndugu zangu wa kundi la G55 wajiunge nasi ili kutimiza malengo yao. Karibuni sana NLD.”
Hayo yalisemwa na Katibu Mkuu wa NLD Taifa, Doyo Hassan Doyo, huku akihitimisha kwa msisitizo wa wazi na kusema kwamba “NLD ni jukwaa la matumaini mapya kwa wote wenye nia njema ya kuleta mabadiliko ya kweli katika taifa letu la Tanzania, wananchi wote mnakaribishwa kwenye jukwaa lenye uzalendo, haki na maendelea, NLD ni Daraja la demokrasia, karibuni sana G55.”