
Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA
_▪️Asema Rais Dkt. Samia ni alama ya ukuaji wa Sekta ya Madini_
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeamua kuwekeza kwenye sekta ya madini ili kuwawezesha wachimbaji wadogo kupata kipato na kujikwamua kiuchumi.
Amesema Serikali imenunua mitambo 15 ya kisasa ya uchenjuaji ambayo itasambazwa kwenye maeneo ya wachimbaji wadogo hivyo ametoa wito kwa wachimbaji hao kujiunga katika vikundi ili waweze kunufaika na fursa hiyo.
Ameyasema hayo leo Jumapili (Mei 04,2025) wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kijiji cha Chingumbwa kitongoji cha Namungo Wilaya ya Ruangwa Mkoani Lindi.
Kadhalika Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa Afisa Madini wa mkoa kuendelea na mpango wa kubaini maeneo yenye madini yatambulike na kisha kutoa leseni kwa wachimbaji wadogo ili waweze kufanya shughuli za uchimbaji.
“Pamoja na hili tumeamua maeneo yote ya madini yaliyochukuliwa leseni na hayajaendelezwa kwa muda mrefu, tutayachukua, tutayapima upya na kuyagawa kwa wachimbaji wadogo.”
“Serikali yenu inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia imenunua ndege maalum ambayo itasaidia kufanya tafiti ya kujua aina ya madini yaliyopo na kiwango chake na sisi huku Lindi itakuja kuruka, Ruangwa na maeneo ya Nachingwea”.
Akizungumzia sekta ya barabara, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali inaendelea na mipango ya kuziboresha barabara mbalimbali katika wilaya ya Ruangwa ili kuziwezesha kupitika wakati wote na hivyo kuwafanya wakazi wa maeneo hayo kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Naye Kaimu Meneja wa Tanesco Mkoa wa Lindi Emmanuel Sengwaji amesema kuwa Wataalam wa Idara ya Miradi mikubwa kutoka Tanesco wamefanya uhakiki wa mahitaji ya umeme katika mkoa wa Lindi kutokana na ongezeko la wawekezaji katika mkoa huo “Tuliomba tujengewe laini la gridi ya Taifa itakayotoa umeme kutoka Masasi hadi Ruangwa katika eneo la Kitandi ili umeme huo uweze kusambazwa maeneo ya uwekezaji ikiwemo kwenye migodi ya iliyopo Kitongoji cha Namungo”.
Mheshimiwa Majaliwa pia alitembelea mgodi wa Elianje Genesis uliopo Namungo wilayani Ruangwa na kuona shughuli za uchenjuaji wa madini.